SIKU moja baada ya wabunge wa Chadema, kutoka nje ya Bunge na kutoshiriki mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011, wabunge wa CCM na CUF wamepinga hatua hiyo na kusema wenzao hao wana kusudio la kuchochea vurugu na kuvunja Muungano.
Pia wengi wa wabunge hao waliochangia wamemnyooshea kidole Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, kuwa amewapotosha Watanzania na ni mwanasheria na mwanaharakati anayepaswa kurudi shule kusoma na pia ni mchochezi wa kutotaka Muungano na Wazanzibari.
Sambamba na hilo, wabunge hao waliochangia Muswada huo juzi na jana, walitetea madaraka aliyonayo Rais wakisema si makubwa na anastahili kuwa nayo kama kiongozi wa nchi.
Tofauti na wabunge hao wa CCM na CUF, Mbunge wa NCCR-Mageuzi wa Kasulu Mjini, Moses Machali, alikuwa pekee aliyewatetea Chadema kwa uamuzi wao wa kususia majadiliano hayo akisema wametekeleza matakwa ya wananchi.
Miongoni mwa waliochangia mjadala huo ni Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed (CUF) aliyesema “ni dhambi isiyosameheka kudharau Wazanzibari waliopiga kura ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa halafu unajifanya wewe (Chadema) ni mkombozi wa watu, Lissu anasema Bunge la kikatiba halitakuwa na haki kwa sababu wabunge wa Zanzibar watashiriki !
“Mna ajenda yenu (Chadema) ya siri, mnaleta ubaguzi ndani ya Bunge, sisi (CUF) ndio tuliandamana kudai Katiba na tulipeleka rasimu ya Katiba, Watanzania wenzangu tusishawishike, maoni ya mabadiliko ya Muswada yametokana na wananchi, taasisi na Kamati ya Bunge, tuaminiane na tupendane,” alisema na kupinga wananchi kuandamana nchi nzima kupinga Muswada huo.
Alihoji kauli ya maoni ya Kambi ya Upinzani kuwa Rais ni dikteta wakati Rais huyo ndiye aliyeleta Katiba hiyo na kufafanua kuwa tangu mwaka 1977 hakuwahi kuona Muswada ulioshirikisha wananchi kama huo.
Alisema madaraka ya Rais yameshapunguzwa vya kutosha kama rasimu ya Katiba kupelekwa kwa wananchi kujadiliwa kabla ya kupitishwa, pamoja na hadidu za rejea kutotungwa na Rais isipokuwa zimeshawekwa kwenye Muswada kitendo ambacho Rais amekikubali.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, alilalamikia wanasheria na wanaharakati bungeni kwamba ndio wanapotosha ukweli kwa makusudi na kuwataka kuacha kupinga madaraka ya Rais kwa kumwangalia kama Mwenyekiti wa CCM, bali kama taasisi yenye madaraka na Katiba ya sasa na kuacha kumwita Rais dikteta.
“Mimi nimekuwa mwanaharakati, najua siasa za uanaharakati, waseme huko nyuma kuna maslahi ya nani...wakasome tena wanasheria hawa, si kuleta uchochezi katika nchi yetu,” alisema. Alisema Rais amefanya uungwana kuwaheshimu na kuleta Muswada huo bungeni kwa ajili ya kuunda Tume hiyo, vinginevyo Katiba iliyopo inamruhusu kuunda Tume bila hata kushirikisha wabunge.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) pamoja na kutaka mamlaka ya Rais yasiingiliwe, alimtaka Lissu anayejiita mwanasheria na mwanaharakati kurudi darasani kuelimika kutokana na kupotosha historia ya nchi kwamba Mwalimu Julius Nyerere alihusika kumomonyoa Muungano kwa kutofuata haki za binadamu, wakati kipengele hicho kiliingizwa kwenye Katiba wakati wa utawala wake na Zanzibar kushirikishwa.
Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), alisema Chadema wakipata Dola hawatautaka Muungano wala Wazanzibari. Mbunge wa Viti Maalumu, Angela Kairuki (CCM), alishauri wajumbe wa Tume itakayoundwa walipwe kwa mujibu wa kanuni na malipo ya Serikali na si Waziri wa Katiba apange.
Pia Mwenyekiti wa Tume awasilishe ripoti bungeni na si Waziri wa Katiba na misingi na gharama za Bunge la Katiba ziainishwe kwa uwazi kwenye sheria.
Mbunge wa Tabora, Ismail Aden Rage (CCM) alisema wasiokubaliana na Muswada huo wanatafuta mwanya wa kuleta vurugu na kuongeza: “Wanaotaka kuhoji madaraka ya Rais ni wahuni … nimekerwa na kauli ya wenzetu wa Chadema, taarifa ya Lissu inalenga kuvunja Muungano”.
Hata hivyo, Mbunge Machali tofauti na wenzake, aliwatetea akisema “watakaopitisha Muswada huu laana za Watanzania ziwe juu yenu kwa sababu hamkutaka usomwe mara ya pili”.
Alisema wabunge kujikita katika malumbano kunazidi kujenga chuki na aliwatetea Chadema kutoka ukumbi wa Bunge kutokana na kushindwa kuvumilia na walifanya hivyo kupinga mwenendo mzima wa kuwasilishwa Muswada huo.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), aliomba mwongozo wa Spika wa kitendo cha Chadema kutoka nje na kama vyama vingine vitatoka nje, mjadala wa Bunge utaendeleaje. Spika, Anne Makinda alijibu:
“Tumekubaliana mikutano yote ya vyama ifanyike saa 7 mchana na watakaotoka katikati ya mjadala waombe ruhusa, Katibu wa Chadema hajaniomba wakutane baada ya kipindi cha maswali, nami nilivyowaona nimewachukulia kama wengine wanavyokwenda kunywa chai”.
Wednesday, November 16, 2011
Wabunge: Chadema wanachochea vurugu
Posted by
Mafia Kisiwani
at
1:36 PM
0
comments
Mfanyabiashara kigagula!

Mfanyabiashara maarufu wa mjini Iringa, Mama Mbilinyi akiingizwa ndani ya gari la Polisi kabla ya wananchi wenye hasira kali hawajamjeruhi kwa tuhuma za kufuga misukule. (Picha na Frank Leonard).
Posted by
Mafia Kisiwani
at
12:48 PM
0
comments
Tanzania Yafungwa na Chad, Yapita Kwa Goli la Ugenini

Taifa Stars ambayo wiki iliyopita iliizamisha Chad 2-1 kwenye uwanja wake nchini Chad, imeshindwa kuwika nyumbani na kukubali kipigo cha bao 1-0.
Katika mechi iliyochezwa jioni hii kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar esa Salaam, Taifa Stars ilifanikiwa kusonga mbele kwa faida ya goli la ugenini.
Chad walipata goli lao la ushindi kwenye kipindi cha pili dakika ya 48, mfungaji akiwa ni Mahamat Labbo ambaye ndiye aliyeipatia Chad goli lake la kufutia machozi kwenye mechi ya awali mjini N'Djaména.
Kwa matokeo haya, Taifa Stars imefanikiwa kuingia hatua ya makundi ambapo itashiriki katika kundi C lenye jumla ya timu nne zikiwemo Ivory Coast, Morocco na Gambia.
Fainali za Kombe la Dunia zinatarajiwa kufanyika mwaka 2014 nchini Brazil.
Posted by
Mafia Kisiwani
at
12:44 PM
0
comments
Friday, November 11, 2011
KAFARA NZITO


Na Luqman Maloto
VIONGOZI wakuu wa Dini ya Shetani, Freemasons, wamefanya kafara nzito kuadhimisha kukamatwa, kuteswa kisha kuuawa kwa aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.
Vyanzo vimesema kuwa ni kawaida kwa Freemasons kufanya sherehe yenye mrengo wa kafara kila mara, mpango wao unapofanikiwa sehemu yoyote ile.
Kwa mujibu wa mitandao kadhaa inayojihusisha na utoaji wa habari za jamii ya Freemasons, kafara ambayo hufanywa ni ile ya mnyama hususan mbuzi mwenye pembe zinazofanana na zile za jini anayeitwa Lucifer (jini mkuu) ambaye huabudiwa na wafuasi wa Dini ya Shetani.
Mnyama huyo huchinjwa kisha damu na kichwa chake huhifadhiwa kwenye chombo chochote chenye muundo wa ndoo ili pembe zitokeze kwa juu na kutengeneza alama maarufu ya Freemasons ambayo wafuasi wake huitumia kwa njia ya vidole kutoa salamu.
Habari zinasema Freemasons walifanya kafara hiyo usiku wa manane kwenye hekalu moja kubwa lililojengwa kwenye eneo la jangwa lililopo ndani ya Jiji la Misrata, Libya.
Inabainishwa kuwa viongozi mbalimbali wakubwa kwenye nchi zilizoendelea kiuchumi ambao wana vyeo vikubwa ndani ya jamii ya Freemasons, walihudhuria kafara hiyo.
MKAKATI HATARI
Habari zinabainisha kuwa Freemasons ipo kwenye mkakati thabiti wa kuitawala dunia kabla ya Desemba 2012.
Kutokana na mkakati huo, imebainishwa kuwa Freemasons wamekuwa wakiratibu sera zao kwa kuangusha utawala wa nchi mbalimbali ambao viongozi wake wameshindwa kuendana na matakwa yake.
Inaelezwa kuwa Gaddafi alikuwa kiongozi mwenye mrengo wa Kiislam japo alikuwa haweki wazi kwenye utawala wake na kwamba alikuwa anapingana vikali na Freemasons.
Kwa mujibu wa mnajimu msomi, Maalim Hassan Yahya Hussein, Jeshi la Kujihami la Umoja wa Nchi za Magharibi (Nato), hutekeleza mipango ya Freemasons kama lilivyofanya Libya kumng’oa Gaddafi.
Maalim Hassan ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mnajimu maarufu barani Afrika, marehemu Sheikh Yahya Hussein, alisema kuwa dhumuni kuu la Freemasons ni kuzipiga vita dini za Kiislam na Kikristo.
“Ipo wazi kuwa wao lengo lao ni kuitawala dunia, kwa hiyo wanahakikisha hilo linawezekana kwa kudhoofisha Uislam na Ukristo ili ufe kisha Shetani ashinde hapa duniani,” alisema Maalim Hassan ambaye ni mrithi wa kazi za unajimu za marehemu Sheikh Yahya.
Aliongeza: “Mkakati mkubwa zaidi ni kuhakikisha dunia inaabudu Dini ya Shetani, wanataka kila mtu awe chini ya mamlaka ya jini mkuu (Lucifer). Dunia nzima itawaliwe na serikali moja na iwe na sarafu moja.”
Kauli ya Maalim Hassan inashabihiana na ile iliyopo kwenye maandiko kwamba zama za Dini ya Shetani kuishika dunia, kutakuwa na mfumo ambao utazuia mtu yeyote kupata huduma za kijamii mpaka awe mwanachama na atatambulika kwa chapa 666.
Habari zaidi zinaeleza kuwa Freemasons wanatumia njia mbalimbali kuhakikisha ulimwengu mzima hakuna anayeamini dini za Mungu na wanapambana kuhakikisha hata Yesu (Nabii Isa) atakaporejea akute hakuna aliye tayari kukombolewa.
Katika kuhakikisha wanapambana na nguvu ya Yesu, Freemasons wamekuwa wakitumia damu ndiyo maana hutoa kafara kwa kuchinja mnyama hasa mbuzi au kondoo wenye pembe kwa imani kwamba huwaongezea nguvu ya kuishika dunia.
Kutokana na tishio la Freemasons, viongozi wa kidini hususan wale wa Mashariki ya Kati, wamekuwa wakiwataka Waislam na Wakristo kwa imani zao, kufunga na kusali ili Dini ya Shetani isipate mafanikio inayoyataka.
SAKATA LA USHOGA
Habari zinasema kuwa Serikali ya Uingereza imekuwa ya kwanza kutumiwa na Freemasons katika kuhakikisha nchi zote zinazounda Jumuiya ya Madola zinapitisha sheria zinazokinzana na maandiko matakatifu yanayoaminiwa na waumini wa Dini za Kiislam na Kikristo.
Ushoga na usagaji ni vitendo ambavyo vinakemewa na dini hizo lakini hivi sasa, Freemasons wanadaiwa kuchochea mabadiliko ili watu wanaojihusisha na hulka hizo wawe huru kikatiba duniani.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, alitangaza kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Madola ili apate misaada inabidi kwanza aruhusu ndoa za jinsi moja (ushoga na usagaji) kwenye katiba ya nchi yake.
Tanzania ikiwa moja ya wanachama wa Jumuiya ya Madola, inapitiwa kwenye rungu hili, ingawa Balozi wa Uingereza nchini, Diana Corner alisema nchi yetu haihusiki.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alishatoa tamko kwamba Tanzania haipo tayari kuruhusu ndoa za mashoga na wasagaji kisha akaonya kuwa kauli ya Cameron inaweza kuivunja Jumuiya ya Madola.
SIYO FREEMASONS PEKE YAKE
Mbali na Freemasons, dini nyingine zenye mrengo wa Shetani ni Illuminati na Skull & Bones ambazo zinavuma zaidi Marekani.
VIGOGO WA FREEMASONS
Viongozi wanaotajwa kuwa vigogo wa jamii hiyo ni marais wa 43 na 44 wa Marekani, Barack Obama na George Bush, Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy ambao wanaonesha alama za vidole ukurasa wa kwanza. Yupo pia Cameron na wengine wengi.
Posted by
Mafia Kisiwani
at
4:06 PM
0
comments
Malema 'avuliwa gamba' ANC
Friday, 11 November 2011
Mashirika ya habari, JOBURG, Afrika Kusini
KIONGOZI wa Umoja Vijana wa chama cha ANC kinachotawala nchini Afrika Kusini, Julius Malema (30) amesimamishwa wadhifa huo kwa miaka mitano .
Hatua hiyo imefikiwa jana, baada ya kamati ya nidhamu ya chama hicho kutoa hukumu dhidi ya kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa kwa vijana wa chama hicho.
Malema ambaye siku za nyuma alikuwa mshirika mkubwa wa kisiasa wa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma lakini baadaye akamuasi, amekuwa katika malumbano makali na uongozi wa chama hicho na rais wake (Zuma).
Hata hivyo, katika kile kinachoonekana ni hatua mahususi ya kuzima uasi unaoweza kufanywa na Malema ndani ya ANC kutokana na nguvu na ushawishi aliyonayo kwa vijana, kiongozi huyo amesimamishwa na kuonywa kuwa iwapo ataonyesha kwenda kinyume na adhabu hiyo anaweza kufukuzwa katika chama hicho.
Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya ANC, Derek Hanekom alisema tabia ya Malema imekishushia hadhi chama hicho na kwamba tabia yake siyo njia sahihi ya kuelezea hisia za kutoridhika na sera za chama.
Katika tuhuma hizo, Malema alishtakiwa pamoja na maofisa wengine watano, akishutumiwa kuchochea mgawanyiko na kuvunjia heshima ya chama hicho.
Habari zaidi zilizopatikana jana zilidai kuwa, huenda Malema akaondolewa katika chama cha ANC.
Hata hivyo, inasemekana kuwa iwapo Malema atatimuliwa huenda ushawishi wake kuhusu atakayekuwa kiongozi wa nchi hiyo mwakani ukadidimizwa.
Malema ambaye hakuwepo kwenye makao makuu ya chama chake wakati hukumu hiyo ilipotolewa, amepewa siku 14 kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Kamati hiyo ya ANC imempata Malema na hatia ya kuvuruga mkutano wa ANC, kukivunjia hadhi chama hicho kwa kudai mageuzi ya utawala nchini Botswana na kuchochea migawanyiko ndani ya chama hicho.
Viongozi wengine wa Umoja wa Vijana wa ANC, akiwemo msemaji wake Floyd Shivambu, wamesimamishwa katika nyadhifa zao kwa muda wa miaka mitatu.
Hata hivyo, kamati hiyo haikumpata Malema na hatia kwenye kosa la kuchochea ubaguzi wa rangi.
Posted by
Mafia Kisiwani
at
3:27 PM
0
comments
Stars leo mashambulizi mwanzo mwisho Inakamuana na Chad

*Inakamuana na Chad
Na Edo Kumwembe, N’djamena, Chad
TAIFA Stars leo itacheza staili ya kushambulia mwanzo-mwisho dhidi ya wenyeji wao timu ya taifa ya Chad katika pambano muhimu la awali kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia. Mechi inapigwa kwenye Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya jijini N’Djamena.
Kocha wa Stars, Jan Poulsen amekumbushia falsafa yake ya kucheza kwa kushambulia, ambapo atawatumia viungo wawili na kujaza washambuliaji mbele Abdi Kassim, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa na Mbwana Samata.
Stars iliyoingia jijini N’dJamena saa saba usiku juzi kwa ndege ya shirika la ndege la Kenya itaingia uwanjani ugenini kusaka matokeo bora katika pambano hilo la awali kabla ya kurudiana na wenyeji wao katika uwanja wa taifa Jumanne jioni.
Kabla ya pambano la leo, jana Stars walifanya mazoezi yao jioni katika uwanja wa Idriss Mahamat Ouya huku wakimkosa mlinzi wa kulia wa timu hiyo, Erasto Nyoni ambaye alianza kusumbuliwa na malaria tangu alipotua jijini N’Djamena.
Kwa mujibu wa Poulsen, kiungo chipukizi, Shomari Kapombe anatazamiwa kuziba nafasi ya Nyoni huku winga mahiri Mrisho Ngassa akitazamiwa kuanza pambano hilo baada ya kukosekana katika vikosi vya kwanza vya kocha Poulsen katika mechi za karibuni.
Kurudi kikosini kwa Ngassa kunatokana na kujitoa kwa mshambuliaji Danny Mrwanda ambaye amekuwa akianza katika mechi za karibuni kama mshambuliaji anayesaidia mashambulizi kuanzia upande wa kushoto.
Poulsen ameimbia Mwananchi, haifahamu timu ya Chad lakini akaahidi kubadili fomesheni ya Stars dakika kadhaa baada ya kuanza kwa pambano hilo kutokana na jinsi atakavyowasoma wapinzani wake.
“Siijui vizuri Chad. Nitawaangalia katika dakika 20 za mwanzo na kama kuna uwezekano wa kubadili fomesheni basi nitafanya hivyo. Lakini kama ilivyo kawaida yangu, asilimia 95 ya mchezo wa timu yangu unategemea zaidi na jinsi tunavyocheza wenyewe kuliko ambavyo mpinzani wetu anacheza.” alisema Poulsen.
Hata hivyo, Poulsen alisema atafurahi zaidi kucheza soka la kushambulia kwa ajili ya kupata matokeo mazuri badala ya kucheza soka la kujihami ambalo haliisaidii timu.
Naye kocha wa Chad ambaye kikosi chake kilifanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wa Idriss Mahamat Ouya, Mohamed Omary alisema dakika tisini ndio zitaaamua mshindi wa leo na si vinginevyo.
“Sichezi mpira nje ya uwanja. Nacheza ndani ya uwanja. Dakika tisini ndio zitaamua matokeo ya mechi ya kesho (leo).” Alisema Omary
Endapo Stars itapata matokeo mazuri katika mechi zake mbili dhidi ya Chad ambazo zinachezwa ndani ya siku nne, itapata nafasi ya kucheza kundi la kufuzu kwenda kombe la dunia ikipangwa pamoja na Gambia, Ivory Coast na Morocco
Mwamuzi wa pambano la leo ni Ogunkolade Bunmi wa Nigeria akisaidiwa na Abidoye Tunde na Baba Abel ambao wote pia ni Wanigeria.
Kwa mujibu wa Poulsen kikosi kamili cha Stars leo ni Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Juma Nyoso, Idrisa Rajab, Shaabani Nditi, Henry Joseph,
Abdi Kassim, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa na Mbwana Samata
Posted by
Mafia Kisiwani
at
3:25 PM
0
comments
Mamlaka ya rais yagawa Kamati ya Katiba

KAMATI ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala imeshindwa kufikia mwafaka kuhusu muswada wa Sheria ya Mapitio na Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011 unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni Jumatatu ijayo.
Habari kutoka ndani ya kikao cha kamati hiyo, jana zinasema wajumbe hao bado wamegawanyika kuhusu suala la sheria inayokusudiwa kutungwa kumpa Rais mamlaka makubwa katika mchakato huo wa kupatikana kwa katiba mpya.
Habari hizo zinaeleza kwamba wanabishania wanachodai kuwa ni muswada huo kumpa Rais madaraka makubwa ambayo ni pamoja na kuteua wajumbe wa tume ya Kukusanya Maoni, sekretarieti ya Tume hiyo na wabunge 116 kuingia katika Bunge la Katiba.
“Kwa hali hii Katiba inaweza kuwa ni mali ya Rais, maana hata wajumbe wa sekretarieti anatakiwa kuteua yeye! Hii ni 'too much' (imezidi). Kwa maana hiyo, mchakato mzima unashikwa na Rais mwenyewe,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.
Taarifa zaidi zinasema kutokana na mvutano huo, suala hilo sasa limechukua mtizamo wa itikadi za vyama, na kwamba wajumbe ambao ni wabunge wa CCM katika kamati hiyo wameanza kulegeza msimamo na kukubaliana na mapendekezo ya Serikali, huku wabunge wa upinzani wakitaka kufanywa kwa marekebisho.
Kwa mujibu wa habari hizo, wajumbe hasa wale kutoka upinzani wanataka madaraka ya Rais yapunguzwe kwa kuipa Tume ya Kukusanya Maoni kutoka kwa wananchi ndiyo ipewe mamlaka ya kuteua sekretarieti yake badala ya suala hilo kufanywa pia na Rais.
Juzi, Waziri wa Katiba na Sheria, Celine Kombani aliliambia Mwananchi kuwa tatizo la wanaodai kuwa Rais ana madaraka makubwa hawatoi mapendekezo mbadala na jinsi ya kurekebisha pendekezo hilo.
“Sasa Rais ndiye aliyepo, kwa nini hawataki kumwamini wakati alipigiwa kura na wananchi wengi? Lakini, basi waseme wao wanatakaje,” alisema Kombani.
Mmoja wa wajumbe alisema: “Mahali tunapofika, ni kama kila mmoja ataondoka na msimamo wake kwenda nao bungeni. Hata leo, mbele ya Waziri (Kombani) tumeshindwa kufikia mwafaka, sasa hiyo siyo dalili njema."
Hali hiyo ya kutoafikiana miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo inatoa ahueni kwa Serikali kuweza kupitisha mapendekezo yake bila kupata upinzani mkubwa kutoka kwa kamati hiyo kama ilivyokuwa awali.
Vikao vya Kamati hiyo vimekuwa vikivuta wabunge wengi hata ambao si wajumbe wake, ili kufuatilia kinachoendelea kwenye meza ya majadiliano baina ya wajumbe husika kwa upande mmoja, kamati na Serikali kwa upande mwingine.
Kutokana na unyeti wa suala la katiba, Spika wa Bunge Anne Makinda aliongeza wajumbe watano katika Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ili kupanua wigo wa mjadala wa suala hilo.
Makinda aliliambia Mwananchi mwanzoni mwa wiki hii kuwa wabunge hao watano wanaruhusiwa kupiga kura kwenye uamuzi. “Kikanuni hawa niliowateua mimi wanaruhusiwa kupiga kura na nimefanya hivyo kutokana na unyeti wa suala lenyewe,” alisema Makinda.
Wajumbe hao ni Mwanasheria Mkuu wa zamani na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila, Mbunge wa Simanjiro (CCM) Christopher Ole Sendeka, Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed pamoja na Deogratius Ntukamazina ambaye ni Mbunge wa Ngara (CCM).
Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011, sasa utasomwa bungeni kwa mara ya pili na umetengewa siku tatu kwa ajili ya kujadiliwa kabla ya kupitishwa na Bunge.
Muswada huo ulisomwa kwa mara ya kwanza Bungeni Aprili 5, mwaka huu, lakini, ukarejeshwa Serikalini ili kufanyiwa marekebisho kadhaa na kuandikwa kwa Kiswahili kabla ya kurejeshwa tena Bungeni.
Kutokana na hali hiyo Serikali ilipata upinzani mkali kutoka kwa wabunge na wanaharakati ambao walidai kwamba muswada huo ulipaswa usomwe kwa mara ya kwanza kutokana na kufanyiwa marekebisho makubwa tofauti na ule wa awali.
Hata hivyo Kombani alisema juzi kuwa: “Muswada huu uliposomwa kwa mara ya kwanza haukuondolewa, bali ulipelekwa kwa umma ili ukajadiliwe”.
“Mabadiliko mengi yanayolalamikiwa yalitokana na hoja za wananchi, hii ni ishara kwamba tulizingatia hizo hoja, sasa kwa mujibu wa taratibu za miswada ni kwamba utasomwa kwa mara ya pili, kama mnavyoona kwenye ratiba,” alisema Kombani.
Mkurugenzi wa Huduma za Bunge, John Joel aliliambia Mwananchi kuwa kwa mujibu wa taratibu, muswada huo hauwezi kutangazwa tena katika Gazeti la Serikali wakati ulishatangazwa Machi mwaka huu.
Ratiba ya Mkutano wa Tano wa Bunge inaonyesha kuwa Muswada huo utasomwa kwa mara ya pili Jumatatu, Novemba 14 mwaka huu na kuendelea kujadiliwa na Jumanne, Novemba 15 na Jumatano Novemba 16 mwaka huu.
Hatua ya muswada huo kupangwa kusomwa kwa mara ya pili, inatafsiriwa kuwa ni “ushindi” kwa Serikali dhidi ya waliokuwa wakipinga hatua hiyo kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikiwa ni wananchi kupewa muda zaidi kwa ajili ya kuujadili.
Mjadala wa muswada huo utatanguliwa na semina kwa wabunge wote itakayofanyika kesho Jumamosi hatua inayotafsiriwa kuwa ni kujaribu kupunguza hoja ambazo zinaweza kujitokeza na pengine kuukwamisha.
Baadhi ya wanaharakati wanaopinga muswada huo kusomwa kwa mara ya pili ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Jukwaa la Katiba ambao wameenda mbali na kudai kuwa Waziri Kombani, amechakachua muswada huo.
Posted by
Mafia Kisiwani
at
3:21 PM
0
comments
Mbowe apandishwa kizimbani

PINDA ASEMA MAANDAMANO CHADEMA YANATUNYIMA USINGIZI
MWENYEKITI wa Taifa Chadema, Freeman Mbowe, amepandishwa kizimbani katika Mahakamani ya Hakimu Mkazi Arusha na kusomewa mashtaka mawili ya kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria na kukataa kutii amri halali ya polisi iliyowataka kutawanyika.
Kutokana na mashitaka hayo, Mbowe ameunganishwa na washtakiwa wengine 27 wanachama wa chama hicho, waliofikishwa mahakamani hapo Jumanne iliyopita wakikabiliwa na mashtaka kama hayo, akiwemo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu .
Mbowe ambaye pia Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzania Bungeni, ameunganishwa kwenye kesi hiyo ya jinai namba 454/2011 ambapo watuhumiwa wote kwa kwa pamoja, wanadaiwa kufanya kusanyiko isivyo halali katika viwanja vya NMC, eneo la Unga Ltd, Manispaa ya Arusha Novemba 7 mwaka huu.
Hata hivyo Mbowe ambaye anakuwa mshitakiwa wa 28 kwenye kesi hiyo, alikana mashitaka yote mawili yaliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Haruna Matagane akisaidiwa na mwenzake, Agustino Kombe.
Upande wa utetezi ukiongozwa na mawakili Method Kimomogoro na Issa Rajabu, uliiomba mahakama hiyo kumpa dhamana mteja wao kwa masharti sawa na wenzake.
Hakimu Devotha Kamuzora anayesikiliza kesi hiyo, alikubaliana na maombi hayo na kumpa dhamana Mbowe, kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho na barua ya utambulisho kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ambao walitia saini hati ya dhamana ya Sh milioni tano kila mmoja.
Mwenyekiti huyo aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti . Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 22, mwaka huu itakapotajwa.
Maelezo ya wakili
Katika maelezo ya hati ya mashitaka, Wakili Matagane alidai washitakiwa wote kwa pamoja walikusanyika isivyo halali kwenye viwanja vya NMC usiku wa Novemba 7 hadi Novemba 8 mwaka huu saa 12.00 asubuhi kwa lengo la kutenda kosa wakati shtaka la pili, ni kukataa kutii amri halalii ya polisi iliyotolewa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Peter Mvulla, kuwataka watawanyike.
Mbowe aliyejisalimisha mwenyewe polisi saa 5:45 juzi baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Kaimu Kamanda wa Polisi, Akili Mpwapwa, alifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi akiwa ndani ya gari namba PT 1844 aina ya Toyota Land Cruiser, lililosindikizwa na gari jingine lililojaa askari waliovalia sare za jeshi hilo huku wakiwa wakiwa wamebeba silaha.
Mwenyekiti huyo aliyefika eneo la viwanja vya Mahakama Saa 3:45 asubuhi, aliongozwa moja kwa moja kwenye chumba maalumu cha kusubiria kabla ya kufikishwa mbele ya hakimu kusomewa mashtaka yake saa 4:00 huku umati mkubwa wa wafuasi wa Chadema ukiwa umefurika ndani na nje ya mahakama hiyo.
Kauli ya Pinda kuhusu Chadema
Wakati hayo yakiendelea Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametoboa siri kuhusu maandamano ya mara kwa mara yanayofanywa na Chadema kwa kutamka kwamba yanaiumiza kichwa serikali.
Akijibu maswali papo kwa papo bungeni jana, Pinda alisema ; "Staili yenu hiyo (Chadema) ya maandamano, inatupa shida sana, tunapata taabu kila wakati kufikiria maandamano badala ya mambo ya msingi.”
Waziri mkuu alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, aliyetaka kujua, pamoja na mambo mengine dhamira na msimamo wa serikali ya kutatua mgogoro wa umeya wa Arusha.
Mnyika alisema tatizo kubwa la mgogoro wa Arusha ni uchaguzi wa meya ambao Chadema imeonyesha dhamira ya dhati kutafuta suluhu hivyo, akataka msimamo Pinda kwa maelezo kuwa mgogoro huo umesambaa nchi nzima na kama haiwezekani kupatikana suluhu Chadema watajua cha kuwaeleza wanachama wao.
Katika jibu lake Pinda aliitaka Chadema kutokuza jambo hilo kwa namna Inavyolichukulia ,“Tusikuze sana mambo kwamba mgogoro huo sasa umesambaa, wapi Mnyika? Wapi? Kwa staili yenu (Chadema) ya maandamano kila mahali, sisi serikalini tuna mengi ya kufanya, hatuwezi kila siku tuwe tunashughulikia matatizo yenu tu. 'People's Power' kila kukicha, haileti suluhu ya matatizo yenu, mnahitaji kubadilika,” alisema Pinda
Alisema wakati mwingine serikali inaacha kufikiria mambo ya maendeleo kwa wananchi na kujikuta inafikiria maandamano ambayo yamekuwa yakishinikizwa mara kwa mara na Chadema nchi nzima.
Pinda alisema staili hiyo ya Chadema kufanya maandamano kwa kile inachoiita, kutegemea nguvu ya umma, imekuwa ikimuuza zaidi yeye binafasi, "kwa kweli mimi naumizwa na hili".
Aliongeza kwamba, maandamano hayo wakati mwingine yanaonyesha namna chama hicho kisivyo na dhamira ya kweli katika kupata suluhu ya matatizo mbalimbali ikiwemo ya mgogoro wa umeya wa Jiji la Arusha.
“ Staili yenu ya 'People's Power, People's Power !' kila kukicha, inatunyima usingizi. Tunashindwa kufanya shughuli nyingine kwa sababu ya kuifikiria Chadema,” alisema Pinda.
Alisema katika suala la Arusha, imeonekana ni jambo la kisiasa ambalo alimweleza Msajili wa Vyama awasiliane na pande zote mbili ikiwemo CCM ili kuona namna ya kukaa meza moja na kulimaliza .
Awali, Waziri Mkuu akijibu swali kama hilo kutoka kwa Mbunge wa Korogwe, Stephen Ngonyani, aliitaka Chadema kujitathmini ili kuona kama kweli kinahitaji suluhu katika mgogoro wa Arusha badala ya kuilaumu serikali.
Katika swali lake la msingi, Ngonyani alionesha wasiwasi wake kwamba mgogoro wa umeya wa Arusha hivi sasa unatishia hata biashara ya utalii katika jiji hilo na kutaka Mbunge wa Arusha Lema apewe dhamana kama njia ya kupunguza mvutano.
"Mheshimiwa Waziri Mkuu, siku hizi kila kukicha ni vurugu na migogoro Arusha. Sasa hivi Arusha utalii hakuna na biashara hazifanyiki. Kwa nini serikali inazuia dhamana ya Lema?”
Akijibu swali hilo, mbali na kukiri kwamba migogoro jijini Arusha inaathiri sekta ya biashara na utalii, Waziri Mkuu Pinda, alikanusha fikra kwamba serikali inahusika kwa namna yoyote katika kupalilia vurugu hizo, ikiwamo kuzuia dhamana ya mbunge huyo wa Arusha Mjini.
“Ni kweli Arusha kuna migogoro mingi lakini, bado ni tulivu. Ila kama Watanzania, lazima tuzingatie unalolisema. Sio kweli kwamba serikali inazuia dhamana ya Mheshimiwa Lema. Vurugu zote hizo, mara nyingi zinazaa kesi,” alisema Pinda na kuendelea;
“Tarehe Oktoba 28, 2011 Lema na wenzake kadhaa walikamatwa, wakafikishwa mahakamani na kupewa dhamana hadi Oktoba 31, 2011 walipotakiwa kufika tena mahakamani. Kimsingi mashtaka yale yote, yanastahili dhamana na mahakama ilikubali watuhumiwa wote wadhaminiwe.”
“Kilichotokea kwa Lema kwa sababu ambazo mimi sizijui, alikataa dhamana, akisema anataka kubaki gerezani. Wenzake walidhaminiwa na Lema alipelekwa gerezani kama alivyotaka hadi Novemba 14.”
“Ilipofika Novemba 7 (2011), Chadema walikubaliana na mawakili wao kupeleka maombi maalumu mahakamani ili wakamtoe Lema. lakini hakimu akawaambia kesi tumeiahirisha hadi Novemba 14. Sasa hii ni Mamlaka ya Mahakama sio serikali. Tutegemee tu kwamba siku hiyo yanaweza kutoka maamuzi ya kumtoa Lema garezani.”
Pinda alisema kwa mazingira yalivyo, hayuko tayari kutoa maagizo mapya juu ya mgogoro wa Arusha kwa kuwa haoni nia ya dhati ya Chadema kutaka suluhu.
Maandamano Dar
Jijini Dar es Salaam, maandamano yaliyopangwa kufanywa na Baraza la Vijana la Chama hicho (Bavicha) Mkoa, kupinga kile walichokiita kukamatwa na kunyanyaswa kwa viongozi wao wa kitaifa, yamesitishwa.
Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche alitangaza kusitishwa maandamano hayo baada ya kuwasili eneo lililopangwa kufanyika maandamano hayo.
Katika utekelezaji wa kusitisha maandamano hayo, viongozi wengine wa chama hicho waliwasili eneo hilo na nakulazimika kuwaomba wafuasi wa chama hicho kutawanyika kutokana na kwamba mpango huo umesitishwa.
Mnamo saa 3:00 asubuhi, umati mkubwa wa wafuasi wa chama hicho ulitanda eneo la Kimara Kona pamoja na Ubungo, yalipopangwa kuanzia maandamano hayo.
Akizungumzia kusitishwa kwa maandamano hayo, Heche alisema wamefikia uamuzi huo baada viongozi wakuu wa chama hicho kufanya majadiliano na maofisa wa Jeshi la
Polisi kuhusu madai ya kero zao.
“Tumepata maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wetu Mbowe na Katibu Mkuu Dk Slaa ya kwamba tusitishe maandamano kwa sababu kuna majadiliano yanaendelea kati yao na maofisa wa Jeshi la Polisi,” alisema Heche.
Aliongeza kuwa kama hakutakuwa na muafaka katika majadiliano hayo, wataingia tena mtaani na kuandamana mpaka kero zao zitakapopatiwa ufumbuzi.
Hali ya ulinzi
Hata hivyo, Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi katika maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam huku kamatakamata ikiwakumba baadhi ya wafuasi wa chama hicho waliovalia mavazi ya chama hicho.
Saa 5: 10 katika eneo la Ubungo gari la polisi lenye namba PT 1818 ambalo lilikuwa limebeba askari waliokuwa na silaha za moto, walikuwa wakiwatangazia wananchi waliokuwa wamekaa katika makundi kutawanyika .
Watu saba waliokuwa wamevalia mavazi ya chama hicho walikamatwa na kufikishwa katika kituo kidogo cha Polisi Urafiki, huku wengine wakiwa wamekamatwa na kubebwa kwenye magari ya polisi ambayo yalikuwa yakizunguka mitaani .
Baadhi ya viongozi wa chadema, walifika katika kituo cha polisi urafiki ambako wafuasi hao saba waliokuwa wamewekwa rumande kwa muda wa saa mbili.
Viongozi hao walifanikiwa kuwatoa kwa dhamana na walitakiwa kubadilisha mavazi hayo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Suleimani Kova alisema hali ya usalama katika jiji la Dar es Salaam ni shwari na hakuna tukio lolote la uvunjivu amani ambalo limejitokeza.
“Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kwamba hakuna tukio lolote la uvunjifu amani ambalo limejitokeza “ alisema Kova.
Kova alisema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha linaimarisha ulinzi katika maeneo yote ya jiji.
Posted by
Mafia Kisiwani
at
3:17 PM
0
comments
Sunday, July 24, 2011
Nishati wafanya ufisadi kwa miaka minne
YABAINIKA JAIRO ALIHUSIKA MIAKA MIWILI, KAFULILA AWASHTAKI KWA JK
Neville Meena, Dodoma
IMEBAINIKA uchotaji wa mamilioni ya fedha katika Idara na taasisi za umma zilizoko chini ya Wizara ya Nishati na Madini kugharamia shughuli zinazohusiana na gharama za bajeti ya wizara hiyo, ulianza mwaka 2004.
Kuanzia Julai 2008, kila mwaka Ofisi ya Katibu Mkuu katika wizara hiyo imekuwa ikiandika barua kwa wakuu wa taasisi hizo kutaka fedha ambazo kwa namna moja au nyingine zinahusishwa na shughuli za bajeti ya wizara kusomwa bungeni au kughramia sherehe ambazo hufanyika baada ya kupitishwa kwa bajeti husika.
Fedha hizo kwa mujibu wa nyaraka husika, zimekuwa zikitumika kugharamia tafrija mara baada ya bajeti kupitishwa na bunge, posho za vikao, posho za kujikimu, vyakula, vinywaji na mafuta ya magari.
Hata hivyo mmoja wa watumishi wa idara ambazo zimekuwa vinara wa kudaiwa fedha wakati wa bajeti alilithibitishia Mwananchi Jumalipi kwamba, wakati wa vikao vyote vya Bunge kila taasisi huwagharamia watumishi wake wanaokwenda Dodoma.
"Mara nyingi wakati wa vikao vya bajeti huwa nakuja hapa Dodoma, lakini utaratibu wa kukaa hapa lazima nijaze fomu ofisini na ipitishwe kwa mabosi wangu ndipo napewa fedha za kuishi, wizara hawawezi kukupa hela," alisema mtumishi huyo na kuongeza:
"Sana sana hapa tukiwa na kazi huwa tunakunywa chai na luch (chakula cha mchana) na hii siyo kila siku, ni kama tuna kazi zinazotuunganisha na wenzetu kutoka ofisi nyingine na maofisa wa wizara."
Matumizi mabaya ya fedha hizo za umma yamebainika kipindi ambacho Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara hiyo, David Jairo, amesimamishwa na Ikulu kwa kupewa likizo ya malipo, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa bungeni dhidi yake.
Jairo anakabiliwa na tuhuma za kuwaandikia barua wakuu wa idara zote zilizoko chini ya wizara yake, ili watoe fedha kwa ajili ya kusaidia kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo, fedha ambazo zinatafsiriwa kwamba zilikuwa ni kwa lengo la kutoa rushwa kwa wabunge.
Kafulila ashtaki kwa JK
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila(NCCR - Mageuzi), jana aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa amemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete akitaka uchunguzi utakaofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali katika Wizara ya Nishati na Madini uanzie miaka ya mitano iliyopita.
"Nimemwandikia barua Rais Kikwete, maana inaonekana kuwa huu mchezo wa kuchota fedha za Umma katika wizara hii umeanza tangu 2008," alisema Kafulila ambaye pia aliwahi kuwalipua baadhi ya wabunge wenzake, akiwatuhumu kwamba waliomba rushwa katika
Halmashauri ya Handeni, mkoani Tanga.
Kafulila katika barua yake ambayo pia Mwananchi limeiona, alisema anakubaliana na hatua za awali za kumchunguza Jairo, lakini anapendekeza ufanyike uchunguzi mpana kwani mtindo si kwa mwaka huu pekee bali hata miaka iliyopita katika wizara hiyo na nyingine nchini.
"Napenda kupendekeza kwako kuwa suala hili lifanyiwe uchunguzi mpana kwa kuwa upana wa kashfa hii ni zaidi ya mwaka mmoja wa fedha 2011/2012, ni zaidi ya Katibu Mkuu mmoja, David Jairo na pengine ni zaidi ya wizara moja ya Nishati na Madini, katika hicho kinachoelezwa kuwa ni kusaidia uwasilishaji wa bajeti," inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Katika barua yake kwa Rais na kutoa nakala kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Uttoh na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), Kafulila anasema ana ushahidi unaothibitisha baadhi ya tuhuma hizo.
Uzoefu wa Jairo
Kwa mujibu wa nyaraka ambazo Mwananchi limeziona, hii ni mara ya pili kwa Jairo akiwa Katibu Mkuu katika wizara hiyo kuandika waraka wa kuomba fedha kutoka kwenye idara husika kwa ajili ya kusaidia mchakato wa maandalizi na uwasilishaji wa bajeti bungeni.
Kwa mujibu wa nyaraka hizo, Mei 12, mwaka jana Jairo akiwa Katibu Mkuu, aliandika waraka kwenda kwa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Stephen Mabada akitaka lichangie Sh20 milioni ili kusaidia kile alichokiita, ‘Gharama za kukamilisha mpango na bajeti ya wizara 2010/2011 na uwasilishaji wake bungeni."
Barua kama hiyo pia iliandikwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura), Haruna Masebu, ambaye taasisi yake iliombwa kuchangia Sh25 milioni, wakati Yona Killagane ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), taasisi yake ilitakiwa kuchangia Sh20 milioni.
Kwa mujibu wa barua hizo, gharama husika kwa ajili ya kazi hiyo ya kibajeti ilikuwa ni Sh186.6 milioni hivyo kuzitaka idara zote kwa pamoja kuchangia kiasi cha Sh90 milioni, wakati wizara ilibaki na jukumu la kuchangia kiasi cha Sh96.6 milioni.
Hata hivyo jumla ya fedha zilizoombwa kutoka Ewura, Tanesco na TPDC ni Sh65 milioni, ikimaanisha kuwa ipo idara au taasisi nyingine ambayo pia iliombwa kuchangia kiasi kilichobaki cha Sh25 milioni.
"Gharama hizi kubwa zimesababishwa na kupanda kwa gharama za posho kutoka Sh60,000 mpaka Sh200,000, Sh50,000 hadi Sh150,000 na Sh30,000 hadi Sh100,000 kwa wenyeviti na makatibu, wajumbe na sekretarieti sawia," inaeleza sehemu ya waraka huo uliondikwa na Jairo na kuongeza:
"Kwa kuwa bajeti ya wizara ya 2009/2010 ilikadiriwa kwa viwango vya zamani, ni dhahiri wizara haiwezi kubeba gharama hizi peke yake. Hivyo inashauriwa Wizara igharamie 96,626,000 na wadau muhimu wa wizara wagharamie 90,000,000".
Barua hiyo haifafanui kuhusu wenyeviti, makatibu, wajumbe na sekretarieti ambao wanapaswa kulipwa posho hizo.
Miaka iliyopita
Mwananchi limethibtisha kuwa "utaratibu" huo wa kuchota fedha umekuwepo kwa muda mrefu, kwani mwaka 2008 na 2009 Wizara hiyo iliandika barua kwa ajilia kutaka "ichangiwe" ili kughramia shughuli za kibajeti.
Julai 5, 2008 aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi, aliandika wakara kwa Dk Idris Rashid, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Lutengano Mwakahesya na Killagane wa TPDC akitaka mchango wa kile alichoeleza kuwa ni
"Kuchangia gharama za hafla fupi baada ya mawasilisho ya bajeti ya wizara bungeni Dodoma".
Katika waraka wake huo, Mwakapugi alitaka kila taasisi kuchangia kiasi cha Sh5 milioni, hivyo kufanya jumla yake kuwa Sh15 milioni kwa lengo la kugharamia tafrija husika.
Juni 19, 2009 Mwakapugi aliandika waraka mwingine kwenda Tanesco, REA na TPDC akitaka michango kwa ajili ya kile alichokieleza katika barua yake kuwa ni "Fedha kwa ajili ya kuwezesha uwasilishaji wa hotuba ya bajeti ya 2009/2010 bungeni Dodoma, kazi ambayo anasema katika barua hizo kwamba, gharama zake ni Sh170,461,500.
"Kama ilivyo desturi, maofisa, taasisi na mashirika yaliyo chini ya wizara hujumuika katika kutoa michango yao hasa katika hoja zote zinazojitokeza katika maeneo husika. Ili kufanikisha zoezi hilo, gharama mbalimbali huhitajika zikijumuisha, posho za vikao, uchapishaji wa vitabu, uchapishaji kwenye magazeti, vyakula na vinywaji posho za safari na mafuta kwa washiriki," inaeleza sehemu ya barua.
Barua hiyo inabainisha kuwa msingi wa kutaka kuchangiwa ni kutokana na hali mbaya kifedha katika wizara hivyo na kuwataka Tanesco kuchangi Sh40 milioni, REA Sh30 milioni na TPDC Sh40 milioni.
Likizo ya Jairo
Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo ambaye ni Mkuu wa Utumishi wa Umma aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma Alhamisi wiki hii kuwa Jairo ambaye yuko chini yake, analazimika kwenda likizo kuanzia juzi ili kupisha uchunguzi wa awali ambao unalenga kubaini iwapo ametenda kosa la kinidhamu kwa mujibu wa sheria zinazoongoza Utumishi wa Mmma.
Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo ndiye aliyemlipua Jairo Bungeni Julai 18, 2011 wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini akisema amekusanya fedha kiasi cha Sh1 bilioni kutoka idara 21 zilizopo chini ya Wizara yake, fedha zisizo na maelezo.
"Nimeanzisha uchunguzi wa awali kwa lengo la kupata ukweli kuhusu tuhuma hizo. Wakati uchunguzi huo ukiendelea, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini amepewa likizo ya malipo kupisha uchunguzi wa awali," alisema Luhanjo na kuongeza:
"Hatua zitakazochukuliwa hapo baadaye zitategemea matokeo ya uchunguzi wa awali".
Licha ya mchakato wa hatua dhidi ya mtumishi huyo wa umma ambaye ni mteule wa Rais kupitia katika mchakato mrefu, mwishoni mwa mchakato huo anaweza kushushwa cheo, kupunguzwa mshahara, kufukuzwa kazi, kuachishwa kazi au kurejeshwa kazini kwa kutegemea matokeo ya taratibu zitakazofuatwa.
Luhanjo alisema Jairo analazimika kwenda likizo kwa kuwa tuhuma dhidi yake ni nzito. "Zingekuwa tuhuma nyepesi ningeruhusu aendelee na kazi wakati uchunguzi huo wa awali ukifanyika, lakini tuhuma hizi ni nzito mno. Hivyo lazima aende likizo ili kupisha uchunguzi huo," alisema Luhanjo.
Alisema uchunguzi dhidi ya Jairo kwa kuwa unahusu masuala ya fedha, utafanywa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo inatakiwa kikamilisha kazi yake katika muda wa siku kumi kisha kuiwasilisha kwake kwa hatua zaidi.
Taarifa ya Luhanjo ambayo ni taarifa rasmi ya Serikali inatofautina na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwamba suala la kuchukua kwa hatua dhidi ya Jairo linamsubiri Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Afrika ya Kusini.
Posted by
Mafia Kisiwani
at
10:16 AM
0
comments
Seneta wa Marekani aahidi kusaidia wafugaji

Joseph Lyimo,Simanjiro
SENETA wa Jimbo la Oregon, nchini Marekani, Jacks Winter, ameahidi kuboresha miundombinu katika Kijiji cha Lengasti, wilayani Simanjiro,ili kuziwezesha jamii za wafugaji kuondokana na matatizo yanayowakabili.
Seneta Winter alitoa ahadi hiyo juzi alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji hicho, kilichoko katika Kata ya Naisinyai.
Alisema kwa kushirikiana na watu wa jimbo lake, atahakikisha kuwa wananchi wa Lengasti wengi wao wakiwa ni jamii ya wafugaji, wanapiga hatua za kimaendeleo.
Winter alisema lengo la ziara yake katika Wilaya ya Simanjiro, lilikuwa ni kujifunza mambo mbalimbali ya jamii na kutambua matatizo yanayowakabili wananchi wake.
Alisema tayari ameshajifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na namna ya kuwasaidia wananchi wa eneo hilo, kuondokana na matatizo.Seneta Winter alisema kwa kushirikiana na watu wa Jimbo la Oregon, atahakikisha wananchi wa Lengasti wanatengenezewa miundombinu bora.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Naisinyai, Kilempu Ole Kinoka, alimshukuru seneta huyo kwa kuwachimbia wananchi mabwawa mawili yanayoyatumiwa kwa shughuli za jamii na mifugo.
Alisema kwa sasa wakazi wa kijiji hicho, wanakabiliwa na tatizola ukosefu wa nishati ya umeme kwa ajili ya kuendeshea mtambo wa kuvutia maji ya kunywa na matumizi mengine.
"Huko nyuma wanawake katika kijiji hiki walikuwa wanasafiri kwa umbali wa kilometa 15 wakitafuta maji, lakini sasa maji tatizo hio limepungua hasa baada ya kuchimbiwa mabwawa mawili,"aisema.
Posted by
Mafia Kisiwani
at
10:15 AM
0
comments
Kenya yaomba Tz iruhusu usafirishaji wa mahindi
Rehema Matowo, Moshi
WAKUU wa Wilaya za Taveta na Lotokitok, nchini Kenya, wameiomba Serikali ya Tanzania kuruhusu wafanyabiashara wa mazao ya chakula wa nchi hiyo jirani, kuingia nchini kwa lengo la kununua chakula ili kukabiliana na upungufu mkubwa chakula unaoikumba Kenya kwa sasa.
Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Taveta, Nkaduda Hiribae, alipokuwa akizungumza katika kikao cha ujirani mwema, kilichofanyika mjini Moshi.
Kikao hicho kiliwahusha wakuu wa wilaya hizo za Kenya na wakuu wa wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro, ambao kwa pamoja, walisaini maazimio yanayotokana na kikao cha kudhibiti uhalifu mipakani, kilichofanyika Julai 13 mwaka huu, katika eneo la Holili, wilayani Rombo.
Hiribae alisema Serikali ya Kenya inaunga mkono agizo la Serikali ya Tanzania kuhusu kudhibiti usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi, lakini ni vyema serikali hiyo ikaona umuhimu wa kusaidia majirani pale wanapokabiliwa na baa la njaa.
Alisema kwa sasa Kenya inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula uliofikia kiwango cha asilimia 70, hali ambayo ni tishio kwa usalama wa maisha ya wananchi.
Aliiomba Serikali ya Tanzania, kufungua milango kwa wafanyabiashara wa Kenya, kuingia nchini na kununua chakula kwa njia halali, jambo ambalo pia litaipatia mapato serikali.
Akizungumzia ombi lililotolewa na Hiribae ,Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaji Musa Samizi, alisema wao kama wakuu wa wilaya, hawana mamlaka ya kutoa vibali vya kuruhusu wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania kununua chakula na kukiuza Kenya.
Alisema wanachoweza kukifanya ni kuwasiliana na ofisi ya Waziri Mkuu na kufikisha ombi hilo kwa utekelezaji.
Kuhusu maazimio waliyoyaazimia mwenyekiti wa kikao hicho, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Peter Toima, alisema ni pamoja na pande zote mbili kushirikiana katika kutoa taarifa zitakazosaidia kuzuia uvushaji haramu wa chakula na uhalifu mwingine.
Alisema azimio lingine ni kuangalia namna wakuu wa wilaya hizo watakavyowasiliana na wizara za Chakula katika pande zote mbili, ili kuona ni jinsi Serikali ya Tanzania inavyowaruhusu Wakenya kununua chakula kutika nchini hata kwa muda mfupi ili kutatua tatizo la njaa linalokabili Kenya.
Mwenyekiti huyo alisema maazimio mengine ni kuanzishwa kwa soko la mazao katika maeneo ya karibu na mpaka wa Holili na Himo ili kuwezesha wafanyabiashara kutoka Kenya, kuja kununua mazao kwa kupitia njia halali na kulipa kodi.
Alisema pamoja na kuazimia kuanzishwa kwa soko la mazao pia wameazimia kufuatilia kwa pamoja maghala yote yaliyoko katika maeneo ya mipakani na kuyachunguza kwani mengi yamekuwa yakitumika kuhifadhia magendo na hata wahalifu.
Posted by
Mafia Kisiwani
at
10:14 AM
0
comments
Warioba asema Bunge limekosa nidhamu
Mwandishi wetu
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba, amesema Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekosa nidhamu na kwamba, linahitaji kuchukua uamuzi mgumu kurejesha hadhi yake.
Warioba alisema hivi sasa chombo hicho cha kutunga sheria kimegeuka kuwa sehemu vichekesho badala ya kujadili masuala muhimu ya kitaifa.
“Bunge limegeuka kuwa sehemu ya vichekesho, limekosa nidhamu linahitaji kuchukua uamuzi mgumu,” alisema Warioba.
Warioba ambaye alikuwa akizungumza na Televisheni ya Taifa (TBC1) jana asubuhi hakueleza kwa undani ukosefu wa nidhamu wa Bunge hilo.
Hata hivyo, matukio ya kila mara yanayoendelea kutokea bungeni ikiwamo kuzomeana, kuzungumza ovyo bila mpango na kuwapo kwa madai ya rushwa ni moja ya mambo yalimfanya atoe kauli hiyo.
Vurugu zinazotokea bungeni mara kadhaa zimekuwa zikimfanya Spika na wenyeviti wa vikao vya Bunge kuwa katika wakati mgumu kusimamia mijadala.
Mara kadhaa Spika amekuwa akisikika akikemea tabia hiyo hadi wakati fulani alifikia kuwalingananisha na watu wa sokoni Kariakoo.
Hata hivyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema wabunge kusingana bungeni si jambo la jabu sana na kwamba ni dalili ya kuelekea kwenye demokrasia kamili bungeni.
Warioba ni Waziri Mkuu Mstaafu wa kwanza kulinyoshea kidole moja kwa moja Bunge katika siku za hivi karibuni.
Moja ya kashfa ambazo hivi karibuni zimelighubika Bunge ni pamoja na baadhi ya wabunge kutuhumiwa kuchukua rushwa ili waweze kupitisha bajeti na miongoni mwa zilizotajwa ni ya Wizara ya Nishati na Madini.
Kashfa hiyo ndiyo iliyosababisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, David Jairo, kuingia katika kitanzi cha kuhusishwa kwake na kuandika barua kwenye taasisi zilizo chini ya wizara yake kuomba fedha za kupitisha bajeti hiyo.
Kashfa nyingine ya Bunge ni lile tukio la wabunge kuzomeana na kumfanya kila mbunge kuwasha kipaza sauti kuongea bila ya kufuata taratibu.
Lawama nyingine dhidi ya Bunge ni ile iliyoibuliwa na Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje ya kutuhumu Kamati ya Bunge kuwa ilifanya mambo kinyume cha taratibu.
Zipo hoja nyingine ambazo ziliibuliwa na kusemwa bungeni zikionya kuwa, Bunge limekuwa likitumika kama ‘rubber Stump’ (mhuri) ya kupitisha mambo mbalimbali bila kuyafanyia uchunguzi wa kina na kujiridhisha.
Warioba akizungumzia Katiba Mpya alisema muswada uliopo katika mchakato umesahau mambo muhimu, kama vile ya uchumi na maendeleo ya jamii badala yake una mambo mengi ya kisiasa.
Alisema masuala mengi yaliyomo ndani ya muswada huo yanalenga kulinda maslahi ya wanasiasa na kuacha kuzungumzia masuala muhimu kwa maendeleo ya wananchi.
Warioba ambaye pia ni Jaji Mstaafu, mara kwa mara amekuwa akitoa kauli nzito za kuishauri Serikali katika masuala ya rushwa na utawala bora.
Mwaka jana, Jaji Warioba alionya dhidi ya mwelekeo wa uongozi nchini kununuliwa kama bidhaa kutokana na vitendo vya rushwa vilivyokuwa vikifanyika karibu na Uchaguzi Mkuu.
Alisema: “Kwa jumla sasa uongozi wa nchi unaanza kubinafsishwa kama biashara ambayo wenye fedha ndiyo watafaulu. Kwa kifupi fedha
SOURCE:Mwananchi
Posted by
Mafia Kisiwani
at
10:11 AM
0
comments
IGP Mwema apangua makamanda
Na Daniel Mjema
INSPEKTA Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, amefanya mabadiliko ya safu ya uongozi wa makamanda wa polisi kwa baadhi ya mikoa ya Tanzania bara.
Katika mabadiliko hayo, baadhi ya makamanda wa mikoa wamehamishwa huku maofia 122 wakipandishwa vyeo.
Mabadiliko hayo yameambatana na uteuzi wa vyeo vya juu ambapo Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, Rais Jakaya Kikwete, amewapandisha vyeo maofisa watano na kuwa Manaibu Kamishina.
Miongoni mwa waliopandishwa vyeo kutoka kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi(SACP) kuwa Manaibu Kamishina ni pamoja na Kamanda Simon Sirro.
Habari za uhakika ambazo Mwananchi Jumapili inazo zimesema katika mabadiliko hayo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Sirro amehamishiwa makao makuu ya Polisi Jijini Dar kuwa mkuu wa operesheni maalumu za Jeshi hilo.
Nafasi ya Kamanda Sirro imechukuliwa na aliyekuwa kamanda wa Polisi mkoa Tabora, Leberatus Lyimo, huku Ofisa Mnadhimu wa Polisi namba moja wa mkoa huo, Anthony Rutashugurugukwa, akiteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Tabora(OCD), Yusuph Mruma, ameteuliwa kuwa Ofisa Mnadhimu namba moja wa Mkoa wa Tabora kuchukua nafasi ya Rutashugurugukwa.
Taarifakuhusu mabadiliko hayo iliyotolewa na IGP Mwema Julai 22 mwaka huu ambayo Mwananchi Jumapili imefanikiwa kuiona, inaeleza pia kuwa tume ya utumishi wa polisi na Magereza imewapandisha vyeo maofisa 117.
Kulingana na taarifa hiyo, maofisa 21 waliokuwa na vyeo vya warakibu wasaidizi waandamizi wa jeshi hilo (SSP), wamepandishwa vyeo na kuwa makamishina wasaidizi wa polisi(ACP) na kuwahamisha vituo vyao vya kazi.
Halikadhalika maofisa 96 waliokuwa na vyeo vya Mrakibu wa Polisi (SP) wamepandishwa vyeo na kuwa warakibu waandamizi wa polisi (SSP).
Baadhi ya waliohamishwa ni OCD Monduli, Contantine Maganga na Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Moshi, Zakaria Benard, wanaohamishiwa ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro ambapo watapangiwa majukumu mapya.
Wengine ni Kihenya Kihenya, ambaye ni OCD Kasulu aliyehamishiwa Mkoa wa Kigoma kuwa Ofisa Mnadhimu namba moja na Alicheus Mtalemwa, ambaye ni Ofisa Mnadhimu namba moja wa Kigoma anakuwa Ofisa Polisi Jamii mkoa Rukwa.
Katika taarifa hiyo ya kipolisi, IGP Mwema amewapongeza maofisa wote waliopandishwa vyeo na Tume ya polisi na Magereza na kwamba upandishwaji huo wa vyeo ulianza rasmi Juni 30 mwaka huu.
Msemaji wa jsehi hilo, Advera Sinso alithibitisha taarifa hizo, lakiniakasema: "Mi mabadiliko ya kawaida tu ya ndani."
Hakuweza kuweka wazi juu ya mabadiliko hayo kwa kile alichodai yuko Dodoma, nje ya makao makuu ya polisi ambayo yapo Dar es Salaa, hivyo akashauri afuatwe kesho.
Posted by
Mafia Kisiwani
at
10:09 AM
0
comments
Mandojo na Domokaya Baada ya kimya kingi, waibukia Fiesta 2011

Herieth Makwetta,
WASANII wakongwe wa muziki wa kizazi kipya, Joseph Francis Michael 'Mandojo' na Precioust Juma 'Domokaya', walikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa burudani ya muziki mjini Moshi na Arusha kwenye tamasha la Serengeti Fiesta wiki iliyopita.
Pamoja na kuwepo kwa idadi kubwa ya wasanii waliopanda jukwaani kwenye tamasha hilo, Wawili hao ambao waliwahi kutamba na kibao cha Wanokonoko mwanzoni mwa miaka ya 2000 walichomshirikisha Lady Jay Dee, walitumbuiza jukwaani kwa muda wa dakika 45 pasipo kuwachosha mashabiki.
Hii ni nadra sana hasa kwa wasanii wetu wa hapa nchini kwani wengi wao wamekuwa ni wavivu pindi wawapo jukwaani na wengine wamediriki kuimba bila hisia wala hamasa kwa mashabiki wanaowapenda.
Inaweza ikawa ni dalili kwamba muziki wa kizazi kipya unapoteza mwelekeo, kwani umahiri wa wasanii wakongwe unajionyesha hadharani na kupendwa zaidi na mashabiki ukitofautisha na ule wa chipukizi.
Katika mahojiano na wasanii hawa waliweza kunieleza mawili matatu ambayo huenda ni maswali ambayo msomaji ulikuwa ukijiuliza kwa muda mrefu.
Mwandishi: Imekuwa ni kama 'suprise' kuwaona hapa jukwaani ilikuwaje mbona ni kama mlipotea kwenye fani?
Domokaya: Ni muda mrefu sasa hatujawa kwenye fani, lakini si kwamba tumeacha muziki, bado tunafanya vema. Imekuwa kama kuwashtua mashabiki lakini si kwamba hatuwezi tena muziki ni wazi tumefanya vizuri na nadhani wengi wameona nini tumefanya.
Mwandishi: Lakini ni kweli kwamba bado mna nguvu za kupambana na wasanii chipukizi?
Mandojo: Ng'ombe hazeeki maini. Bado tuna nguvu na kuhitajika na mashabiki. Chipukizi wana nafasi yao lakini hata sisi pia tuna nafasi zetu. Inapopatikana nafasi kama hii lazima tuhakikishe tunafanya kile ambacho tumekubaliana kimkataba na si lelemama.
Domokaya: Unajua linapofikia suala kama hili, bila shaka hatuachi nafasi kubwa kati yetu na promota ambaye ametupa kazi. Hili ni tatizo ambalo wasanii wengi chipukizi wanalo, hawathamini ile nafasi wanayopewa na mapromota hawa wanaoandaa matamasha likiwemo hili la Fiesta, ni heshima kubwa. Hivyo lazima uhakikishe unawafanya mashabiki wako wakuone unafaa na kukonya nyoyo zao.
Mwandishi: Mnadhani muziki wa bongofleva kwa sasa umepoteza mwelekeo?
Domokaya: nadhani ni wakati mzuri kwa wapembuzi wa masuala ya burudani ya muziki kutambua kwamba wakongwe wana nafasi kubwa sana kuliko chipukizi kwa sasa, kwani bongo fleva ya zamani zi ile ya sasa kwani inadumu na haipotezi ladha.
Mandojo: Kwa upande wangu naona umepoteza mwelekeo, kwani sisi tuliimba mapenzi lakini yenye kufundisha na hata nyimbo zingine hazikuwa mapenzi lakini zilielimisha na kufundisha lakini kwa sasa mtu akiimba wimbo mapenzi yanazidi sana, licha ya hivyo bado hazikai zinachuja mapema.
Mwandishi: Mmesema kuwa mmerudi tena kwenye fani mmejipanga vipi.
Mandojo: Tuliwahi kuimba na Lady Jay Dee mwanzoni mwa miaka ya 2000 wimbo wa wanoknok, lakini hivi sasa tutarudi tena tukiwa na Jide na tunategemea kutoa kazi ambayo itakonga nyoyo za mashabiki.
Mwandishi: Bado mnaimba kwa vinanda kama zamani au?
Domokaya:Hapana kwa sasa tunafanya 'live band', kila siku ya Alhamisi tupo pale Nyumbani Loung kwa Jay Dee. Muda mwingi tumekuwa tukiandaa kazi zetu ambazo tunatarajia kuziachia mapema mwaka huu, kwa hiyo mashabiki wakae mkao wa kula.
Mandojo: Tumeandaa nyimbo kama 'Baba Kidawa' ambao tumetengeneza katika studio ya 'Marko Chali' tukiwa katika kundi la Wamandavaku ambalo tumewaingiza vijana wawili.
Mwandishi: Hii inamaanisha kwamba kwa sasa kundi la Mandojo na Domokaya halipo na badala yake kuna Wamandavaku?
Mandojo: Hapana, sisi tutabaki kuwa kama sisi na kundi ni baadaye.
Mwandishi: Je mna lolote la nyongeza?.
Man na Domo: Zaidi ni kuwajulisha washabiki wetu kuwa tumerudi upya waje washuhudie mambo yetu.
Mwandishi: Kazi njema
Man na Domo: Pamoja
Posted by
Mafia Kisiwani
at
10:07 AM
0
comments
Ripoti Maalumu:Tuhuma za rushwa zaivuruga Kamati ya Mrema
Neville Meena, Dodoma
RUSHWA inayodaiwa kupenyezwa kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeathiri uamuzi wa baadhi ya hatua ambazo kamati hiyo inapaswa kuchukua dhidi ya udhaifu uliobainika katika hesabu za fedha na miradi inayotekelezwa na halmashauri ambazo tayari zimefanyiwa ukaguzi.
Kwa kawaida kamati hiyo inapofanya ziara katika halmashauri kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake, hubainisha udhaifu katika maeneo husika na kutoa mapendekezo au hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya udhaifu husika na wakati mwingine hutoa au kupendekeza adhabu wanazopaswa kupewa wahusika.
Sehemu ya tatu ya nyongeza ya nane ya Kanuni za Bunge, toleo la mwaka 2007 inabainisha kuwa LAAC ina wajibu wa kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali za Mitaa yaliyoainishwa katika taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
"Kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali za Mitaa yaliyoainishwa katika Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali," kinaeleza kipengele cha 12(a) cha sehemu hiyo.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa taarifa ya Kamati ndogo ya LAAC, iliyokuwa mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, Mei 22- 28, 2011 inatia shaka kutokana na tofauti kubwa ya mapendekezo yaliyotolewa dhidi ya udhaifu uliobainishwa katika muhtasari wa kumbukumbu za kamati hiyo.
Kutokana na udhaifu wa taarifa hiyo, baadhi ya wajumbe ambao walikuwa katika msafara huo wa Tanga wameikana wakidai kwamba wajumbe waliopewa kazi ya kuiandika, 'waliichakachua'.
"Hii ripoti iliandikwa na (anawataja wabunge wawili), nasikia hata Mwenyekiti (Augustino Mrema) hakuwapo kutokana na dharura lakini tuliwaamini, ila walichoandika wanakijua wenyewe," alilalamika mmoja wa wajumbe wa kamati.
Kwa mujibu wa muhtasari huo, kamati hiyo ndogo iliyoongozwa na Mrema kwenda Tanga ilibainisha udhaifu katika vipengele kumi na moja kwenye miradi ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na kutoa mapendekezo 10 ya namna ya kuchukua hatua.
Kadhalika, kamati hiyo inatoa maelekezo kwa lugha kali na kupendekeza hatua za kinidhamu kwa baadhi ya watendaji wa halmashauri za wilaya Muheza na Jiji la Tanga kutokana na kubaini uzembe katika usimamizi wa baadhi ya miradi ya maendeleo inayosimamiwa na mamlaka hizo. Lakini, jambo linalotia shaka ni jinsi kamati hiyohiyo ilivyoshughulikia matatizo yaliyojitokeza katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwani ilibainisha upungufu uliowekwa katika vipengele 12, lakini ikatoa mapendekezo matatu tu ya jumla ya jinsi ya kukabiliana na kasoro hizo.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alisema "udhaifu" unaobainika katika uandishi wa hatua za kuchukua dhidi ya watendaji wa Handeni, unaweza kuwa uthibitisho wa tuhuma zilizotolewa dhidi ya baadhi ya wajumbe wa LAAC kwamba waliomba rushwa kwa uongozi wa halmashauri hiyo.
Tuhuma hizo ni zile zilizotolewa Juni 13, mwaka huu na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo kwamba aliwakamata wajumbe wenzake watatu wakiomba rushwa kwa viongozi wa Halmashauri ya Handeni.
Katika maelezo yake bungeni, Kafulila aliwataja wabunge wawili kati ya watatu anaowatuhumu kuwa ni Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi na Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Badwel na kwamba taarifa za tukio hilo alikuwa amekwishaziwasilisha kwa Mrema na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Yaliyojiri Lushoto, Handeni
Taarifa ya kamati hiyo ndogo ya LAAC kuhusu Halmashauri za Mkoa wa Tanga inaweka bayana kwamba katika ziara yake wilayani Lushoto Mei 23, mwaka huu kamati hiyo ndogo ilijadili hesabu za halmashauri hiyo na kubaini kuwa kwa miaka mitatu mfululizo, imekuwa ikipata hati zenye shaka za ukaguzi wa CAG.
Miongoni mwa udhaifu mkubwa uliobanishwa ni malipo ya Sh117 milioni ya mishahara kwa watumishi hewa, kiasi cha Sh15 milioni kutumika nje ya bajeti, Sh65 milioni kukusanywa kwa kutumia stakabadhi za kughushi, uchache wa fedha zilizopelekwa katika shule za msingi ikilinganishwa na kiasi kilichotolewa na Hazina na kutopelekwa kwa Sh75 milioni ambazo ni ruzuku ya lazima ya Serikali Kuu kwa ajili ya maendeleo vijijini.
Wilayani Handeni, kamati hiyo pia ilibaini udhaifu kadhaa ikiwa ni pamoja na kiasi cha Sh18 milioni cha malipo ya mishahara kwa watumishi hewa, kutoonekana kwa lambo la kunyweshea maji mifugo lililodaiwa kujengwa eneo la Madebe kwa gharama ya Sh35.5 milioni na kutokuwapo kwa vitasa pia sakafu kubomoka katika soko la Sindeni ambalo limegharimu Sh24.5 milioni.
Udhaifu mwingine katika Halmashauri ya Handeni ni kutopeleka vijijini kiasi cha Sh105 milioni kwa ajili ya kufidia kodi zilizofutwa na matumizi ya mabati 466 ambayo yanadaiwa kutumika kujenga vyumba vinne tu vya madarasa ya Shule ya Sekondari Segera.
Hatua zilizochukuliwa
Pamoja na udhaifu huo, Kamati hiyo ndogo inatoa mapendekezo ambayo mmoja wa wajumbe wake anayaita kuwa ni "dhaifu" yasiyolingana na uzito wa kasoro zilizobainishwa katika Halmashauri ya Handeni.
Mapendekezo hayo ni matatu ambayo yanaitaka ofisi ya ukaguzi ya halmashauri hiyo kujadiliana kuhusu kufungwa au kutofungwa kwa hoja ya uchakavu wa mali mbalimbali zenye thamani ya Sh520 milioni, halmashauri kuongeza bidii kudai fedha zake kiasi cha Sh133.3 milioni katika taasisi tatu tofauti na kuitaka kuweka wazi kwa madiwani na wananchi gharama zitakazotumika kujenga Bwawa la Kidereko.
"Unaona! Hii ina maanisha nini? Taarifa haisemi kitu kuhusu malipo ya watumishi hewa, wala lambo ambalo halikuonekana, wala haimwajibishi mtu yeyote hata kwa kumpa barua ya onyo. Hapa lazima kuna kitu si bure," alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye alisema hakwenda Tanga wala Pwani kwa kuwa alipata dharura wakati wa ziara hizo.
Lakini, kwa upande wa Lushoto, tofauti na Handeni, kamati hiyo ilitaka ipatiwe majina ya watumishi hewa waliolipwa mishahara husika, nyaraka za fedha na taarifa za kibenki (bank statements) pia kuagiza Mkurugenzi Mtendaji apewe barua ya onyo na mamlaka yake ya kinidhamu kutokana na uzembe uliosababisha halmashauri yake kupata hati yenye mashaka.
Pia kamati hiyo iliagiza Halmashari ya Lushoto kupeleka mara moja fedha za maendeleo vijijini ili kufidia kodi zilizofutwa na kuhakikisha makato ya malipo ya pensheni yanapelekwa katika mamlaka husika.
Makundi ya wabunge
Kwa mujibu wa muhtasari wa kumbukumbu husika, kamati ndogo iliyokuwa mkoani Tanga ilikuwa na wabunge ambao ni Mrema, Kafulila, Badwel, Zambi, Mbunge wa Kondoa Kaskazini (CCM), Zabein Mhita na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Kiwanga.
Wengine ni Katibu wa Kamati hiyo, Mswige Dickson Aswile, Mwakilishi wa Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesebu za Serikali (CAG), Denis Mbilinyi na Mary Assey ambaye alikuwa katika msafara wa wabunge hao akimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga (RAS). Kwa mujibu wa toleo la 10 la kitabu cha orodha ya wabunge cha Juni mwaka huu, LAAC ina wajumbe 17.
Mbali na wajumbe waliokwenda Tanga, wengine katika Kamati hiyo ni Makamu Mwenyekiti wa LAAC ambaye pia ni Mbunge wa Kinondoni (CCM), Iddi Azzan, Riziki Lulida (Viti Maalumu, CCM), Subira Mgalu (Viti Maalumu, CCM), Hasnain Mohamed Murji (Mtwara Mjini, CCM), Abdul Mteketa (Kilombero, CCM), Tauhida Nyimbo (Viti Maalumu, CCM), Joseph Selasini (Rombo, Chadema) na Kurthumu Mchuchuli (Viti Maalumu, CUF).
Kwa mujibu wa kitabu hicho, makatibu wengine wa kamati hiyo mbali na Aswile ni Edwin Tongora na Chipanda Chilemeji. Hata hivyo, taarifa ya ziara ya kamati ndogo ya LAAC iliyofanya ziara mkoani Pwani haikuweka bayana majina ya wajumbe waliokuwa katika msafara mkoani humo.
LAAC ni kamati ambayo ilijizolea sifa nyingi kwa jinsi ilivyoanza kazi yake kwa kasi na kuwachukulia hatua watendaji wa halmashauri kadhaa nchini ambao walithibitika kuwa dhaifu katika usimamizi wa rasilimali za maeneo yao ya kazi kiasi kwamba baadhi yao walikatwa asilimia 15 ya mishahara yao kama adhabu mojawapo.
Tuhuma za rushwa
Mbali na tuhuma zilizotolewa na Kafulila kwa wajumbe waliokuwa ziarani Tanga, pia zimetolewa tuhuma mpya kwa baadhi ya wajumbe wa kamati ndogo iliyokuwa mkoani Pwani ambako inadaiwa kuwa kiongozi wa kamati hiyo, Azzan alikuwa akikumbana na upinzani mkali pale alipokuwa akijaribu kuhoji baadhi ya mambo katika halmashauri husika.
Habari zaidi zinadai kwamba hata kamati iliyokwenda Pwani baadhi ya wajumbe wake wanatuhumiwa kuomba rushwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, ambaye baada ya kumpigia simu alitoa taarifa kwa kiongozi wa timu hiyo, Azzan.
Hali hiyo inadaiwa kuitafuna Kamati hiyo kiasi kwamba imeshindwa kukutana tangu kuanza kwa mkutano wa nne wa Bunge la bajeti, licha ya Mwenyekiti Mrema kuitisha vikao mara tatu kwa nyakati tofauti.
Mrema aliliambia Mwananchi kuwa atamweleleza Spika kuhusu hali ya kamati yake ili kupata mwongozo wa nini kinachotakiwa kufanywa. Vikao vilivyokwama ni vile vilivyotishwa Juni 16, Juni 20 na Julai 19, mwaka huu na ajenda saba zilizokuwa zimepangwa kujadiliwa zimeendelea kuwekwa kiporo.
Kikao cha Julai 19, kilikuwa kimepanga pamoja na mambo mengine, kupitia kumbukumbu ya yaliyojiri katika ziara za Tanga na Pwani, makubaliano ya kujadili taarifa za hesabu za baadhi ya halmashauri wakati kamati ikiwa bungeni, makubaliano kuhusu mwaka wa hesabu (2008/09) au 2009/10) zitakazoendelea kujadiliwa katika kipindi kijacho na Taarifa ya Katibu wa Kamati kuhusu barua kutoka kwenye halmashauri kwenda kwa Katibu wa Bunge.
Mrema katika mazungumzo yake na gazeti hili alisema: "Nikiwaita akija Kafulila baadhi yao hawaji, lakini Kafulila asipokuwepo, wengine utawaona wamefika na hapo unakuwa huwezi kuwa na kikao kinachoweza kufanya uamuzi kwa manufaa ya nchi yetu".
Habari zaidi zinadai kwamba, tuhuma za Kafulila bungeni dhidi ya Zambi na Badwel zinawatisha hata baadhi ya wale waliokuwa katika kamati ya mkoani Pwani kwani wanahofu kwamba huenda nao wakaanikwa ndani ya kikao cha kamati hiyo ya LAAC. Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aanasema ili kuinusuru kamati hiyo, ipo haja ya kuvunjwa na kuundwa upya kwani hivi sasa ni kama imesambaratika kwani wajumbe husika hawaaminiani.
"Ni bora ikaundwa upya, kazi hazifanyiki na sasa tuna viporo kwa sababu hesabu za mwaka 2009/2010 bado kabisa hatujazigusa na mwezi Aprili mwakani lazima tuwasilishe taarifa bungeni, sasa tutawasilisha nini kama kazi hazifanyiki?" Alihoji mjumbe huyo.
Kanuni za Bunge
Pamoja na Kanuni ya 114 (3) kusema kwamba kamati zinaweza kukutana kila itakapotakiwa kufanya hivyo na Spika, Naibu Spika au Mwenyekiti wa Kamati husika kwa idhini ya Spika, kanuni hizo haziweki wazi hatua zitakazochukuliwa ikiwa wajumbe wa kamati watashindwa kukutana kama ilivyotokea kwa LAAC.
Ama kanuni za 113 (6) na (7) zinaeleza kuwa ujumbe wa mbunge katika kamati unaweza kukoma ifikapo mwishoni mwa mkutano wa kumi wa uhai wa bunge, ikimaanisha kuwa hakuna mbunge anayeweza kuodoka katika kamati yake ya sasa hadi mkutano wa kumi utakapofikia ukomo.
Huu ni Mkutano wa Nne wa Bunge la 10 na Mkutano wa 10 unatarajiwa kufanyika ifikapo Oktoba 2012, wakati kamati za kudumu za bunge zitakapopangwa upya.
Kwa maana hiyo ni vigumu kwa sasa LAAC kufanyiwa marekebisho kwa mujibu wa kanuni au kuundwa upya, isipokuwa Spika aamue kutumia vifungu vingine vya kanuni vinavyompa mamlaka ya kifanya jambo kadri anavyoona yafaa.
Posted by
Mafia Kisiwani
at
10:05 AM
0
comments
Madiwani Chadema 'ngangari'
Moses Mashalla, Arusha
MADIWANI watatu wa Chadema waliotakiwa kujiuzulu nyadhifa zao katika Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kufikia saa 7:02 mchana jana, wamegoma kufanya hivyo na badala yake wameutaka uongozi wa taifa wa chama hicho kuwasafisha kwa kuwataka radhi.
Kauli hiyo ya madiwani hao akiwamo Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Estomi Mallah imekuja siku chache baada ya kuvuja kwa ripoti ya kamati iliyoundwa na Chadema kuchunguza mwafaka wa madiwani wake, wa CCM na TLP katika kumpata Meya wa jiji hilo ikibainisha kuwa hakukuwa na tuhuma za rushwa katika mchakato huo.
Badala ya kujiuzulu, madiwani hao wametoa masharti magumu kwa chama hicho, licha ya kutaka kusafishwa, pia wamemtaka Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuwasafisha kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kueleza umma kwamba hawakuhongwa.
Mallah ambaye ni mwenyekiti wa madiwani hao alisema jana kuwa wamekitaka chama chao kuwaomba radhi kupitia vyombo vya habari kwa kuwa ripoti hiyo imebainisha ukweli wa mambo. Alisema taarifa za wao kuhongwa zilizotolewa na uongozi wa chama chao ziliwasababishia usumbufu mkubwa ndani ya jamii zao kiasi cha kufanya baadhi yao kunusurika kupigwa mawe.
Akizungumzia agizo la kujiuzulu nyadhifa ndani ya manispaa hadi kufikia jana saa 7:02, alisema wamepanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwa kuwa hawakutendewa haki. Mallah aliutaka uongozi wa Chadema kutambua misingi ya haki huku akibanisha kuwa migogoro ya ndani kwa ndani huenda ikakipeleka mahali kubaya akisema kama kuna tatizo, linapaswa kutatuliwa kupitia vikao na si vinginevyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Uchumi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Elerai (Chadema), John Bayo alikwenda mbali akimtaka Lema kupita katika maeneo yote ya Jiji la Arusha kuwasafisha mbele ya wananchi kutokana na tuhuma alizozitoa kuwa walipokea rushwa.
Chadema kimetofautiana na madiwani hao kwa kile inachoeleza kuwa wamepingana na msimamo wa chama hicho kutotambua mwafaka katika mgogoro wa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinapinga jinsi muafaka huo ulivyofikiwa kikisema haukufuata misingi ya kisheria ba kwamba ili mwafaka upatikane mambo kadhaa yalipaswa kujadiliwa kwa pamoja ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wa chama hicho kutokana na maandamano yaliyofanyika mapema mwaka huu kupinga matokeo ya uchaguzi wa meya, kulipwa fidia kwa familia za marehemu waliokufa kwenye maandamano hayo na uchaguzi wa meya wa jiji hilo kurudiwa.
Uongozi wa taifa wa chama hicho unaona kwamba kitendo cha madiwani hao kukubali nyadhifa ndani ya Baraza la Madiwani wa Jiji la Arusha kabla mambo hayo hayajatekelezwa, kimetafsiriwa na Kamati Kuu ya Chama hicho kuwa ni usaliti uliotokana na rushwa.
Wahudhuria kikao cha halmashauri ya jiji
Licha ya madiwani hao kupuuza agizo hilo la makao makuu ya Chadema, jana walihudhuria kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa kikifanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kama kawaida huku baadhi yao wakisema sasa wameamua kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi waliowachagua ili kuwaletea maendeleo na kuweka pembeni tofauti za kisiasa.
Dk Slaa alipoulizwa jana kuhusu msimamo wa madiwani hao, alisema Katiba ya Chadema itachukua nafasi yake katika kuamua suala hilo akisema asingependa kuibua malumbano katika suala hilo wala kutunishiana misuli. Alisema diwani yoyote anayeona kwamba hakutendewa haki ana haki ya kwenda mahakamani.
"Katiba ya Chadema itakwenda kufanya kazi, kamati kuu iliwataka wajiuzulu mara moja kama wamekataa sasa katiba itachukua mkondo wake na yoyote anayeona alichafuliwa yuko tayari kwenda mahakamani," alisema.
Mgogoro huo wa umeya Arusha ulisababisha mauaji ya watu watatu katika maandamano yaliyofanyika Aprili mwaka huu, mmoja wao akiwa ni raia wa Kenya baada ya Chadema kuamua kuandamana kwa nguvu bila kibali cha polisi.
SOURCE:Mwananchi
Posted by
Mafia Kisiwani
at
10:01 AM
0
comments
Friday, July 15, 2011
Lowassa: Nimeshtushwa

Leon Bahati, Dodoma, Ramadhan Semtawa, Dar
WAKATI uamuzi wa Rostam Aziz kung'atuka ubunge wa Igunga na ujumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) ndani ya chama chake cha CCM ukiibua gumzo kubwa karibu kila kona nchini, mshirika wake mkubwa kisiasa, Edward Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli ameeleza kushtushwa na tukio hilo.Juzi, Rostam, mmoja wa watu muhimu ndani ya CCM aliyeshiriki vyema katika mtandao uliomwingiza madarakani Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005, alitangaza uamuzi mzito wa kung'atuka siasa akipinga kile alichokiita siasa uchwara za baadhi ya viongozi wake.
Uamuzi huo mzito wa Rostam uliibua kwikwi na vilio kutoka kwa wapigakura jimboni kwake Igunga, wakiwamo wale waliomchagua kwa vipindi vitatu mfululizo tangu mwaka 1994 ulipofanyika uchaguzi mdogo kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Charles Kabeho. Jana, Lowassa alisema: "Kwa kweli nimeshtushwa, nimesikitishwa...kilichonishtua zaidi ni vilio. Namna wananchi wa Igunga walivyokuwa wanalia na kusikitika."
Hata hivyo, Lowassa ambaye naye amekuwa akitajwa katika orodha ya watu watatu wanaopaswa kuachia nafasi zao za uongozi CCM katika kile kinachoitwa chama kujivua gamba, alipoulizwa kuhusu taarifa za yeye kufuata njia ya mshirika wake huyo alijibu: "Siku ikifika nitatoa uamuzi na nitajibu wakati ukifika."
Lowassa alikuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari katika Viwanja vya Bunge mjini Dodoma, kuhusu alivyopokea uamuzi huo wa Rostam na kama yuko tayari kufuata mfano na njia hiyo ya kujiuzulu nyadhifa zote ndani ya CCM.
Lakini, juzi Rostam aliweka bayana kwamba uamuzi wake wa kujiuzulu hautokani na shinikizo lolote ikiwamo kile kinachoitwa mpango wa kujivua gamba, bali aliufanya uamuzi huo kuepuka kuathiri biashara zake kutokana na kuchafuliwa na siasa uchwara akieleza kuwa yeye ni mfanyabiashara wa kimataifa, lakini akaahidi kuendelea kuwa mwanachama mtiifu wa CCM.
Hata hivyo, Lowassa jana hakutaka kufafanua kuhusu kauli yake hiyo ya "Nitajibu wakati ukifika," ingawa alionyesha tabasamu wakati akiulizwa na kujibu swali hilo la iwapo atafuata nyayo za Rostam au la.
Mshirika wao mwingine, Andrew Chenge, jana alivumishiwa kuandaa mkutano na waandishi wa habari ili naye atangaze uamuzi wa kujiuzulu nafasi zake zote kama hatua ya kutekeleza azimio la Nec la kujivua gamba.
Lakini, alipotafutwa kwa simu na kuulizwa kuhusu taarifa za yeye kutaka kujiuzulu, Chenge alijibu kwa kifupi kuwa alikuwa Uingereza, kitu kilichothibitisha kuwa hakukuwa na mpango huo wa kujiuzulu huku akisisitiza: "Mimi niko nje ya nchi, nipo Uingereza."
Hivi karibuni, Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi, maarufu kama Mzee wa Vijisenti, aliwahi kuliambia gazeti hili: "Sijui kama mimi ni gamba CCM," huku akisisitiza kwamba anaheshimu taratibu za chama na asingeweza kukurupuka na kuanza kuzungumza mambo ya chama nje ya utaratibu.
Chenge alisema chama kina utaratibu wake wa kufanya maamuzi, hivyo kuanza kutoka nje ya taratibu na kuzungumzia mambo ya ndani ya chama isingekuwa rahisi kwake kwani anaheshimu taratibu zilizopo.
..Sendeka asifu ujasiri wa Rostam
Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole-Sendeka, ambaye amekuwa akijipambanua kama mpambanaji wa ufisadi, alisema kujivua kofia zote alizokuwa nazo Rostam ni kitendo cha kuletea afya chama tawala.Sendeka alifafanua kwamba kuwapo kwa vigogo wanaotuhumiwa kwa rushwa ndani ya CCM ni sawa na mtu anayeugua na ili apone lazima waondoke ili chama kipate afya njema.
Alisema kutokana na sababu hiyo, anamuunga mkono Rostam kwa uamuzi wake aliochukua wa kutii uamuzi wa chama wa kujivua gamba, kwani ni hatua moja ya kukiboresha chama na kuongeza: "Unaposhauriwa kwa afya ya chama chako na ukakubali ni uamuzi wa kijasiri."
Hata hivyo, alionya kwamba mkakati huo wa kujivua gamba ni zaidi ya vigogo watatu ambao wamekuwa wakitajwa mara kwa mara.Sendeka alisema wote wakifuata mkondo wa Rostam, chama kitajijengea taswira nzuri ya kupendwa na watu ambao tayari wameanza kukata tamaa kutokana na kuona haya kutokana na tuhuma zinazowahusu.
Kuhusu wale ambao bado hawajatekeleza hilo, ole-Sendeka alisema: "Cheo ni dhamana, uongozi ni utumishi, kama wale waliokupa dhamana wanakushauri uondoke, huna haja ya kubishana, tekeleza."Naye Ally Mohamed (Nkasi Kaskazini-CCM), alisema amefurahishwa na hatua ambayo Rostam ameichukua kwa lengo la kusafisha chama.
Lakini, akasema ni wakati mwafaka wa kuhakikisha CCM inasafishika mbele ya Watanzania kwa sababu, kuwapo kwa watuhumiwa hao wa ufisadi wanaozungumzwa mara kwa mara, kulionekana kuchafua chama chote."Sasa ni wakati wengine nao wachukue uamuzi kama huo. Tunajua wako wengi, waondoke chama kiimarike," alisema Mohamed.
Tundu Lisu azungumzia uamuzi wa Rostam
Tundu Lissu (Singida Mashariki-Chadema), alisema bado gamba la CCM halijavulika kwa sababu Rostam ni mmoja wa watuhumiwa 11, ambao walitajwa na Chadema kwenye orodha ya mafisadi, Mwembeyanga, Temeke mwaka 2007.
"Bado kumi," alisema Lissu huku akijigamba kuwa mafanikio hayo ni juhudi zilizofanywa na Chadema ili kulinda rasilimali za Watanzania ili zitumike vizuri.
Kuhusu kauli ya Rostam kuwa amejing'oa kwenye nyadhifa zake kutokana na "siasa uchwara", Lissu alijibu: "Kama kweli siasa uchwara ndizo zimemwondoa Rostam, basi ndizo zinazofaa kuendelezwa hapa nchini."
Ingawa Rostam alikataa kuhusisha uamuzi wake na kujivua gamba, tangu kikao cha Nec cha Aprili, Sekretarieti mpya ya CCM imekuwa ikitangazia umma orodha ya makada wake watatu ambao wanapaswa kujiuzulu ili kuleta kile inachokiita heshima kwa chama na kukisafisha.
Posted by
Mafia Kisiwani
at
9:53 AM
0
comments
Uamuzi wa Rostam kung'atuka watikisa nchi

Waandishi Wetu
TUKIO la Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kuachia nyadhifa zote za uongozi ndani ya CCM, limepokelewa kwa hisia tofauti baada ya watu wa kada mbalimbali kutoa maoni tofauti huku baadhi yao wakimsifu na wengine kumponda.
Hata hivyo, chama hicho tawala kimeeleza kuwa hakijapata taarifa rasmi za uamuzi huo wa Rostam ingawa yeye alisema jana kuwa, barua yake ya kujiuzulu aliikabidhi kwa mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Baadhi ya wanasiasa wamemponda mwanasiasa huyo, huku wasomi na baadhi ya viongozi wa dini wakisema kuwa hatua yake hiyo ni sahihi katika mwenendo wa sasa wa siasa ndani ya chama hicho.
Kwa mujibu wa wasomi na viongozi hao wa dini, hatua hiyo ya Rostam imeelezwa kuwa ni mfano kwa viongozi wengine wa chama na Serikali yake wanaojiona kuwa wanaelemewa na tuhuma mbalimbali.
Mwanasheria maarufu nchini, Profesa Abdallah Safari alisema kuwa, uamuzi huo ni ujumbe kwa viongozi wengine wa CCM wanaonyoshewa kidole kila kukicha.
“Kwa maoni yangu, uamuzi huo umemsaidia Rais Kikwete kwani kati ya watu waliokuwa wakinyoshewa sana vidole, mmoja wao ameamua kujiondoa, kwa kweli amemwondolea mtihani, lakini pia itasaidia chama ambacho nacho kilikuwa kikinyooshewa sana vidole,” alisema Profesa Safari.Hata hivyo, alisema hatua hiyo ya viongozi kujivua nyadhifa zao haitatosha kukisafisha chama hicho dhidi ya maovu.
“Kuna ubadhirifu mwingi ambao unatakiwa ufanyiwe kazi, mambo mengine kama EPA na Richmond hayawezi kumalizwa kwa watu kujivua nyadhifa zao,” alisema msomi huyo.Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally, alisema hotuba ya Rostam aliyoisoma mbele ya wazee wa Igunga, inaonyesha kwamba amejiuzulu kwa shingo upande.
“Nimesoma hotuba yake yote, lakini inaonyesha wazi kwamba ameachia nyadhifa ndani ya chama hicho ikiwa ni kutekeleza kauli ya CCM ya kujivua gamba, inaonyesha kwamba amechukua uamuzi huo kwa shingo upande,” alisema Bashiru,
CCM: Hatujapata barua yake
Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alilieleza Mwananchi jana kuwa mpaka wakati huo chama hicho hakikuwa kimepokea taarifa hizo rasmi na kwamba hata wao walizipata kupitia vyombo vya habari jana, hivyo hawapo katika nafasi nzuri ya kutoa tamko linaloweza kuwa msimamo chama.
"Hata sisi (CCM) tumepata taarifa hizo kupitia vyombo vya habari kama nyinyi, hivyo hatuwezi kutoa msimamo wa chama kwa sasa," alisema Mukama.
Rostam: Barua yangu ipo kwa Mwenyekiti
Hata hivyo, Rostam mwenyewe akizungumza na Mwananchi jana, alisema tayari alishamwandikia barua Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kuhusu uamuzi wake huo.
Alifafanua kwamba, CCM ndiyo yenye mamlaka na inayopaswa kulieleza Bunge kwamba kiti hicho kiko wazi.
Alisema tangu kutangaza uamuzi huo, hadi jana mchana tayari alikuwa amepata salamu na ujumbe mfupi (sms) kutoka kwa wanachama 11,872, wa CCM ambao walimpongeza kutokana na hotuba yake.
Kwa mujibu wa Rostam, wanachama hao walikubaliana naye kuhusu siasa uchwara zinazoendeshwa na chama hicho katika kipindi hiki, hadi kuamua kuchukua uamuzi huo.
Rostam alisema mbali na ujumbe wa simu, pia alipata simu kutoka kwa wanaCCM wengi Kanda ya Ziwa ambapo waliunga mkono hotuba yake. Inaelezwa kuwa Rostam ana ngome kubwa ya wafuasi kwenye mikoa ya Kigoma, Mara, Mwanza, Tabora na Shinyanga.
Nape akwepa
Kwa upande wake, Katibu wa Idara ya Itikadi ya Uenezi, Nape Nnauye, alisema hakuwa na la kusema juu ya tuhuma ambazo ametupiwa na Rostam kupitia hotuba yake ya kujivua nyadhifa zake.
Wakati akizungumza na aliowaita wazee wake juzi, Rostam alituhumu Sekretarieti ya CCM kwamba ilieneza kwa kupotosha nia njema ya Mwenyekiti wao (Rais Kikwete) katika dhana ya chama hicho kujivua gamba akisema kuwa, ilienezwa kwa tafsiri na mwelekeo tofauti na ule wa awali.
"Wajumbe wawili wa Sekretarieti, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), John Chiligati na Katibu wa Idara ya Uenezi, Nape Nnauye, walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ilifikia uamuzi wa kuwapa siku 90 wale walioitwa watuhumiwa wa ufisadi kujitoa katika nafasi zao za uongozi vinginevyo watafukuzwa na chama," inaeleza sehemu ya hotuba hiyo ya Rostam.
Hotuba hiyo ilieleza kuwa viongozi hao walikaririwa na vyombo vya habari wakieleza kuwa majina ya watuhumiwa hao yalikuwa yakifahamika kutokana na kuhusishwa katika kashfa za Richmond, EPA na ununuzi wa rada na hatimaye walitaja majina ya wanasiasa watatu kuwa ndiyo ambao walilengwa na uamuzi huo.
Rostam Aziz alisema kuwa jina lake kutajwa katika orodha ya watuhumiwa hao ni ufinyanzi wa porojo na fitina za kisiasa, ambao ulimshangaza, kutokana na namna uamuzi halisi wa Nec, hususan kuhusu 'kujivua gamba'¯ ulivyopindishwa na wajanja wachache kwa maslahi binafsi ya kikundi fulani cha watu.
Alisema mshtuko na mshangao wake umejikita katika viongozi wa chama hicho alichotumikia kwa bidii na uaminifu mkubwa, kufanya juhudi kubwa hata kufikia hatua ya kukivisha kikao alichokiita kitukufu cha Nec uamuzi ambao msingi wa hoja zake ni vita vya kimakundi ya siasa ndani ya CCM, propaganda za vyama vya siasa vya upinzani na vyombo vya habari kwa upande mwingine.
Katika hotuba yake, Rostam alieleza kushangazwa na kushtushwa kwake na ujasiri ambao viongozi wa Sekretarieti mpya ya CCM wamekuwa nao, kiasi cha kutaja jina lake kwa kulihusisha na kile wanachokiita ufisadi ambao hata kimsingi ushahidi wa wazi umethibitisha kuwa ni porojo za kisiasa zinazotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule ujao wa 2015.
Mkoani Kilimanjaro
Askofu Msaidizi wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo, alisema hakuamini aliposikia taarifa hizo, lakini baadaye aliamini na kusema mbunge huyo amesoma alama za nyakati.
“Ni uamuzi mgumu aliouchukua, lakini ulistahili kwa mazingira ya siasa za Tanzania na amesoma vizuri alama za nyakati…na wengine wote wanaotajwa kuwa na tuhuma nao wafuate nyayo hata kama hazijathibitishwa,”alisema Shoo.
Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri, Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi (MUCCoBS), Michael Tiruhungwa, alisema Rostam angewatendea haki Watanzania kama angejielekeza zaidi kwenye tuhuma anazohusishwa nazo.
Naye Mtaalamu Mshauri wa Huduma za Biashara, Akwiline Kinabo, alisema kujiuzulu kwa Rostam ni mwanzo tu na kama kweli CCM imedhamiria kujivua gamba, basi Watanzania watarajie mengi makubwa zaidi ya kujiuzulu.
Kutoka Mwanza
Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Wilson Mushumbusi, alisema uamuzi wa Rostam kujiuzulu umetokana na wakati mgumu wa kisiasa alionao.
Mushumbusi alifafanua kwamba mbunge huyo amekuwa akituhumiwa kwa kashfa nyingi, kujiuzulu kwake ni mwanzo wa mafanikio ya Chadema juu ya madai ya ufisadi ambayo yanamkabili.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) Mkoa wa Mwanza, Josephat Ngolangwa alisema Rostam ameonyesha ukomavu wa kisiasa na uamuzi wake umekinusuru chama.
Alifafanua kwamba, hatua hiyo inadhihirisha Rostam ni muumini wa dhati wa chama chake na kuwataka wengine waliotuhumiwa ndani ya chama na hata katika Serikali, wafuate nyayo za Rostam ili kurejesha imani kwa chama.
Alisema CCM kama taasisi ya kisiasa inafanya uamuzi kutokana na vikao na haya yote yanayotendeka ni uamuzi wa vikao vya chama wa kuwataka viongozi wote kusimamia uamuzi wa vikao vya chama ngazi ya juu.
Kwa msisitizo, alisema kwa sasa viongozi wana kazi kubwa ya kuimarisha chama na siyo wakati wa kujadili nani atakuwa rais katika kipindi kijacho cha mwaka 2015 kwa kusema kuwa 2015 ni mbali sana.
Mkoani Tanga
Nako mkoani Tanga watu wamepokea uamuzi huo wa Mbunge wa Igunga kwa mitazamo tofauti, huku wengine wakitaka mapacha wenzake ambao wamekuwa wakitajwa na viongozi wa CCM kuhusika na tuhuma za ufisadi wafuate nyayo zake.
Wasomi na wanasiasa waliozungumza na gazeti hili jana walisema kung’atuka kwa Rostam Aziz ni tukio ambalo lilitarajiwa.
Mkereketwa wa CCM, Tarafa ya Mlalo, Wilayani Lushoto, Zahabu Mjata alisema kitendo cha Rostam kuachia ngazi ni cha kiungwana na kwa hiyo hastahili kusakamwa kama inavyofanywa na baadhi ya watu.
Posted by
Mafia Kisiwani
at
9:51 AM
0
comments
Mtei amshika pabaya Wassira
Moses Mashalla, Arusha
MUASISI wa Chadema hapa nchini, Edwin Mtei "amemshika pabaya" Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais (mahusiano na uratibu) ,Stephen Wassira akitaka ajiuzulu kwa kulala bungeni.
Pamoja na kupongeza picha ilivyotoka gazetini, alisema kitendo cha kigogo huyo kuuchapa usingizi bungeni kimedhibitisha jinsi Serikali ya Rais Jakaya Kikwete isivyokuwa makini na kumtaka Wassira ajiuzulu mara moja.
Mtei,alitoa kauli hiyo siku moja kupita baada ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro wakiwamo wasomi kuunga mkono hatua ya gazeti hili kumpiga picha waziri huyo akiwa amelala bungeni huku wakisema kuwa ni sahihi na kubeza kauli ya waziri huyo kuwa kitendo hicho ni uchochezi.
Akizungumza na gazeti hili, Mtei alisema kitendo cha waziri huyo kusinzia bungeni kimemdhalilisha yeye mwenyewe pamoja na Serikali ya Rais Kikwete na kusisitiza kwamba Serikali haiko makini kutatua kero za umma.
"Kitendo cha Wassira kusinzia bungeni kimetuonyesha ni jinsi gani Serikali ya CCM isivyokuwa makini kutatua kero za umma,amejidhalilisha
kwanza yeye mwenyewe, lakini pia wananchi anakotoka na Serikali nzima mimi namshauri aachie ngazi tu"alisema Mtei.
Alisema mara kwa mara chama chao kimekuwa kikiilaumu Serikali kwa kutokuwa makini na kero zinazoligusa taifa hivyo kitendo cha waziri huyo kuuchapa usingizi bungeni kimetoa majibu ya madai yao.
Hatahivyo, alipuuza vikali hoja ya Wassira kuwa kitendo cha gazeti hilo kumpiga picha akiwa amelala kuwa ni uchochezi huku akisema kuwa
kama alikuwa mgonjwa angeenda kupumzika nyumbani kwake na sio kusinzia bungeni.
Mtei,ambaye pia aliwahi kuwa gavana wa Benki Kuu hapa nchini alilipongeza gazeti la Mwananchi kwa kuwafichua wabunge wanaolala bungeni huku akisema kwamba kamwe lisirudi nyuma katika kusimamia maadili ya taaluma ya habari.
"Mwananchi lisirudi nyuma, mnatusaidia sana kuwafichua viongozi wanaolala bungeni bila nyie sisi tusingejua endeleeni na msiogope"alisisitiza Mtei.
Pia alizungumzia kero ya mgao wa umeme uliolikumba taifa na kusema kuwa Serikali ya Rais Kikwete imeshindwa kutatua kero za taifa hali ambayo imesababisha taifa kuendelea kuwa maskini.
Alisema kuwa kero ya mgao wa umeme ni mzigo mkubwa wa Watanzania ambao hauvumiliki huku akionya ya kuwa endapo hali hiyo isipotatuliwa mara moja huenda nchi ikaingia katika matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na vijana kukosa ajira,viwanda kufungwa kwa kushindwa kufanya kazi na uchumi kuporomoka.
SOUCE:MWANANCHI
Posted by
Mafia Kisiwani
at
9:49 AM
0
comments





