Monday, January 21, 2013

Gesi kuiangusha CCM

• WABUNGE WAKAMIA MJADALA BUNGENI na Mwandishi wetu NEEMA ya gesi iliyovumbuliwa Mtwara, na wananchi kutaka ibaki mkoani humo badala ya kuisafirisha kwenda jijini Dar es Salaam, imegeuka laana, na sasa inaweza kukiangusha Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015 baada ya wananchi kuanza kupoteza imani nacho, Tanzania Daima Jumapili limebaini. Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji (CCM) na Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Mikindani, Ali Chinkawene ndio vinara wa kampeni za kupinga gesi hiyo kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, na wamejitokeza hadharani kupinga kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba wakazi wa Mkoa wa Mtwara hawapaswi kuzuia. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa wiki nzima sasa, umebaini kuwa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ambao wengi ni wafuasi wa CCM, wamepoteza imani na chama hicho. Baadhi ya wabunge wa mikoa ya Mtwara na Lindi ambao wako jijini Dar es Salaam wakihudhuria vikao vya kamati za Bunge, waliliambia Tanzania Daima Jumapili kwamba wana-CCM katika mikoa hiyo, wamepoteza imani na chama hicho kutokana na kauli za viongozi wao wanaotumia vitisho kutaka gesi hiyo isafirishwe kwenda Dar es Salaam. Mbunge wa Mtwara Mjini, Murji, alisema juzi kuwa msimamo wake wa kupingana na Rais Kikwete uko pale pale na kusisitiza kuwa yuko tayari kutimuliwa ubunge kuliko kuachia mradi huo wa gesi upelekwe Dar es Salaam. Rais Kikwete katika salamu zake za mwaka mpya wa 2013, alisema Mtwara hawana haki kuzuia gesi hiyo kwani rasilimali inayopatikana popote katika nchi hii ni mali ya taifa, na hutumika kwa manufaa ya taifa na si mali ya watu wa pale ilipogundulika au pale shughuli inapofanyika. Akionesha dhahiri kupingana na Rais Kikwete, Murji alisema serikali inapaswa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme mkoani Mtwara badala ya Dar es Salaam. Alisema: “Tulipoona hali inakuwa tete, niliitisha kikao cha Kamati ya Siasa kujadili nini msimamo wa chama katika hili. Kamati ya Siasa wakasema hawawezi kukisemea chama kwa sababu chama ni wanachama, hivyo nikaitisha kikao cha Halmashauri Kuu ambapo pia tuliwaalika mabalozi wa mitaa. “Katika kikao hicho, wajumbe walipinga kwa nguvu zote suala la gesi kupelekwa Dar es Salaam. Wakaniambia niseme msimamo wao kuwa hawataki gesi iende Dar es Salaam hadi pale masilahi ya wana-Mtwara yatakapowekwa wazi na serikali na huo ndio msimamo.” Alisema msimamo huo si wake binafsi, bali ni maazimio ya vikao halali vya chama hicho vinavyowakilisha wanachama, na kwamba historia ya mikoa ya kusini jinsi ilivyonyimwa maendeleo, ilitumiwa na wajumbe kujenga hoja hiyo. “Wakati sisi hatuna umeme, hakuna aliyefikiria kutuunganisha kwenye gridi ya taifa… Barabara ya kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam miaka 51 ya uhuru sasa haijakamilika. Lakini bomba wanataka kujenga kwa miezi 18. Hivi kuna Watanzania muhimu zaidi ya wengine?” alihoji mbunge huyo. Duru za siasa zilidokeza kuwa, kauli za viongozi hao ndio msimamo wa wana CCM ambao baadhi wameapa kwamba kama serikali haitabadilisha msimamo wake, chama hicho kisahau kushinda uchaguzi wowote katika mikoa hiyo. Wabunge wengine ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, walisema wanasubiri kwa hamu mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza hivi karibuni mjini Dodoma, kwani wamepanga kuzungumzia msimamo wao kuhusu suala hilo. “Sisi wengine mtatusikia Dodoma. Tumeamua kutetea maslahi yetu na kizazi chetu kijacho kwani kusini hatukuwa na cha kuwaachia, lakini leo tuna gesi. Haitoki Mtwara,” alisema mbunge huyo. Wakati wabunge hao wakiweka msimamo huo, jana na juzi, wananchi wa wilaya zote za Mkoa wa Mtwara walifanya maandamano kwa lengo la kuendeleza kilio chao cha kupinga gesi yao kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam. Akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Kigamboni, Dar es Salaam, Faustine Ndungulile, alisema kuwa lilionekana dogo, lakini kadiri muda unavyokwenda, badala ya kuwa kipele linaekelea kuwa jipu na mwisho linaweza kusababisha kansa itakayosambaa mwili mzima. Alisema: “Nimefuatilia kwa makini kuhusu hoja ya wananchi wa Mtwara, lakini vile vile nimefuatilia kwa makini majibu yanayotolewa na viongozi mbalimbali. Kinachoonekana ni kwamba, viongozi hawajipanga vizuri. Kila mtu anasema lake na kila mtu anafanya lake. “Kwa mtazamo wangu, katika sakata hili kuna mambo mawili makubwa ya msingi. Mosi, maendeleo duni katika mikoa ya kusini ikiwa ni pamoja na Mtwara. Pili, tatizo la ajira kwa vijana,” alisema Ndungulile. Mbunge huyo alishauri elimu itolewe kuwashibisha wananchi wa Mtwara jinsi gani watanufaika kimaendeleo na kwa upande wa ajira kwa vijana. “Kubeza na kutumia hoja za nguvu havitasaidia, badala yake tunahitaji nguvu za hoja zitakazowaelimisha na kuwashawishi wananchi wa Mtwara katika maeneo yafuatayo: “Ni vigezo gani vilitumika kufikia uamuzi wa kujenga bomba la gesi toka Mtwara hadi Dar es Salaam? Kwanini mtambo wa kuzalisha umeme usijengwe Mtwara na kusambazwa kuja Dar es Salaam? Je, mchanganuo wa gharama ukoje? “Je, upatikanaji wa gesi hii utakuwa na manufaa gani kwa wananchi wa eneo husika? Je, kutakuwa na viwanda vya kusindika gesi vitakavyojengwa huko Mtwara? Je, mikoa inayozalisha itapata asilimia ya mapato ya gesi inayozalishwa katika eneo hilo? “Je, ajira ngapi zitakazozalishwa na sekta hii, na asilimia ngapi ya ajira zitakuwa kwa ajili ya wakazi wa eneo hili?” Mbunge huyo alisema suala hili linapaswa kushughulikiwa mapema na kwa haraka wakati likiwa bado ni kipele kwani likishakuwa jipu au kansa, gharama za kulishughulikia zitakuwa kubwa. Alisema wananchi kuhoji si dhambi wala uhaini kwani uelewa wao umekua na wanahitaji kushirikishwa na kupewa majibu ya kina.

No comments: