Monday, January 21, 2013

Dk. Slaa alipua bomu

• ADAI SERIKALI IMEAGIZA MTAMBO WA KUHUJUMU MAWASILIANO YA WAPINZANI na Abdallah Khamis KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema kuwa amebaini kuwapo mpango wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuingiza mtambo wa kuingilia mawasiliano ya wapinzani kwa ajili ya kuhujumu uchaguzi mkuu mwaka 2015. Dk. Slaa ambaye ni mara yake ya pili kutoa tuhuma za CCM kuingiza mtambo wa kuingilia mawasiliano ya CHADEMA, alisema tayari ameshapata e-mail yenye kuonyesha thamani ya mtambo huo na kwamba utagharimu dola 850,000 za Marekani, karibu sawa na sh bil. 1.3. Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua kongamano la vijana wa vyuo vikuu wa CHADEMA (Chaso), jijini Dar es Salaam, lililokuwa na lengo la kujitathmini na kupanga mikakati ya kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015 pamoja na kuwaapisha viongozi wapya wa shirikisho hilo. Alisema tayari ameshaandika barua kwa mamlaka husika kuwajulisha hilo, lakini hadi sasa hawajajibu. “Tuna ‘details’ na nyaraka nyingi zinazoonesha namna mtambo utakavyotumika kwa ajili ya kuwahujumu wapinzani na kwa kuwa tumeshaandika barua kwa mamlaka husika na hawajatujibu, kwa sasa sitaenda kwa undani zaidi juu ya hili. Subirini siku ifike nitaweka kila kitu hadharani,” alisema Dk. Slaa. Alisema CCM kwa kushirikiana na Idara ya Usalama wa Taifa, wamekuwa wakitengeneza propaganda mbalimbali za kutaka kumchafua yeye pamoja na CHADEMA, lengo likiwa kuwaondoa Watanzania katika ajenda za msingi za kupigania ukombozi. Aliongeza kuwa, awali mahasimu wake kisiasa walikuja na propaganda kuwa amechukua mke wa mtu, kisha wakasema amedhulumu viwanja huko Mabwepande na sasa wameanzisha suala la kukopa sh milioni 140 ambalo alifafanua kwamba halina ukweli wowote. “Wanawalisha maneno wale wanaokubali kununulika, msifikiri yale yanatoka midomoni mwao hapana, lakini watambue leo hakuna Mtanzania atakayehangaika na uongo unaotengenezwa kwa ajili ya kuwafanya wazidi kutawaliwa,” alisema Dk. Slaa. Akizungumzia tuhuma za CCM na serikali kushirikiana kuingiza mtambo wa kuhujumu mawasiliano ya wapinzani, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye alisema madai hayo ni ya uongo. Akizungumzia vita dhidi ya ufisadi nchini Dk Slaa, alisema wanaojidanganya kwa kusema kwamba kwa sasa siyo agenda ya Watanzania, wamefilisika kimawazo kwa kuwa suala hilo halitanyamaziwa na CHADEMA mpaka wahusika watakapotiwa mbaroni. “Kama wanataka tunyamaze kuhusu ufisadi basi waturudishie twiga waliowatorosha, fedha za EPA, mabilioni ya Uswisi na pia watuambie ni kina nani wanawaua tembo walio katika hifadhi zetu na kisha kusafirisha pembe kupitia bandari zinazolindwa na watu wanaolipwa kwa kodi za Watanzania… vinginevyo hakuna wa kutunyamazisha zaidi ya Mwenyezi Mungu,” alisema Dk. Slaa. Akielezea sera ya majimbo na mafanikio ya mikutano ya chama hicho kwa mwaka 2012, Dk. Slaa, alisema imekuwa na mafanikio makubwa hasa baada ya wananchi kuzinduka na kuamua kudai haki za kutaka kunufaishwa na rasilimali zinazowazunguka. Alisema miaka minane iliyopita wakati CHADEMA waliposema rasilimali za nchi zianze kunufaisha eneo husika kwanza, watu wengi hawakuelewa, lakini leo baada ya kufikiwa na ufahamu kupitia Operersheni za CHADEMA, maarufu kwa jina la M4C, kila eneo limezinduka na sasa serikali inaanza kuwaona watu hao kuwa maadui kwa kuwa wanadai kuthaminiwa. “Nchi yetu kila eneo kuna rasilimali na hatusemi ziwanufaishe watu wa eneo husika tu, bali tunataka waanze wao na ziada ndiyo iende maeneo mengine, leo mnawaona Mtwara na Lindi wanapigania haki hiyo na maeneo mengine hivyo hivyo, kwa hiyo tuna haki ya kujivunia mafanikio ya kuwaelewesha wananchi juu ya kudai haki zao,” alisema Dk. Slaa. Aliongeza kuwa, mwaka huu watahakikisha suala la mauaji holela ya raia wasio na hatia, halijirudii ikiwa ni pamoja na kuishinikiza serikali iunde tume huru ya kimahakama kufuatilia matukio yote ya mauaji yenye utata yanayohusishwa na harakati za kisiasa mwaka 2012. Akizungumzia suala la kufukuzana ndani ya CHADEMA, Dk Slaa alisema hawataogopa kumfukuza mwanachama yeyote msaliti anayeenda kinyume na katiba ya chama hicho na kutolea mfano madiwani waliofukuzwa mkoani Arusha na wanachama wengine. Alisema licha ya madiwani wa Arusha kujua walifukuzwa kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, waliamua kwenda mahakamani kutaka kukisumbua chama, hali aliyosema mahakama haikuweza kukubaliana nao na sasa wanawajibika kulipa gharama za kesi na wakishindwa wataenda gerezani. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, aliitaka CCM imshauri Rais Jakaya Kikwete aunde tume huru kuchunguza mauaji mbalimbali ya kisiasa yanayotokea nchini badala ya kupanda jukwaani na kusema CHADEMA ndio wauaji. Alisema kuwa kila siku Nape Nnauye, Mwigulu Nchemba na viongozi wengine ndani ya chama chao wamekuwa wakitaka kuwaaminisha wananchi kuwa CHADEMA inahusika na mauaji ya kisiasa. “Nape anasema CHADEMA wanahusika na mauaji ya kisiasa, Mwigulu naye hivyo hivyo, viongozi wengine ndani ya chama chao nao wanapiga kelele hizo hizo, sisi CHADEMA tunasema iundwe tume huru ya kimahakama wao wanaogopa, wanajua wataumbuka juu ya ufedhuli wao,” alisema Mnyika. Aidha, alisema wamebaini CCM inachapisha kadi za CHADEMA na kisha kuwagawia wanachama wao ili kuwahadaa wananchi kuwa chama hichi kinakimbiwa. “Unajua ukiona mtu anajidanganya mwenyewe, huyo inabidi umsikitikie kwa kuwa kila njia ya udanganyifu wao sasa imeshabainika katika mioyo ya Watanzania, na sasa wameona wajaribu kujiridhisha katika nafsi zao wakiwa katika mikutano ya hadhara kwa kupeana kadi walizochapisha wenyewe huku wakishangiliana,” alisema Mnyika.

No comments: