Friday, November 11, 2011

Malema 'avuliwa gamba' ANC

Friday, 11 November 2011



Mashirika ya habari, JOBURG, Afrika Kusini
KIONGOZI wa Umoja Vijana wa chama cha ANC kinachotawala nchini Afrika Kusini, Julius Malema (30) amesimamishwa wadhifa huo kwa miaka mitano .
Hatua hiyo imefikiwa jana, baada ya kamati ya nidhamu ya chama hicho kutoa hukumu dhidi ya kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa kwa vijana wa chama hicho.

Malema ambaye siku za nyuma alikuwa mshirika mkubwa wa kisiasa wa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma lakini baadaye akamuasi, amekuwa katika malumbano makali na uongozi wa chama hicho na rais wake (Zuma).

Hata hivyo, katika kile kinachoonekana ni hatua mahususi ya kuzima uasi unaoweza kufanywa na Malema ndani ya ANC kutokana na nguvu na ushawishi aliyonayo kwa vijana, kiongozi huyo amesimamishwa na kuonywa kuwa iwapo ataonyesha kwenda kinyume na adhabu hiyo anaweza kufukuzwa katika chama hicho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya ANC, Derek Hanekom alisema tabia ya Malema imekishushia hadhi chama hicho na kwamba tabia yake siyo njia sahihi ya kuelezea hisia za kutoridhika na sera za chama.

Katika tuhuma hizo, Malema alishtakiwa pamoja na maofisa wengine watano, akishutumiwa kuchochea mgawanyiko na kuvunjia heshima ya chama hicho.

Habari zaidi zilizopatikana jana zilidai kuwa, huenda Malema akaondolewa katika chama cha ANC.
Hata hivyo, inasemekana kuwa iwapo Malema atatimuliwa huenda ushawishi wake kuhusu atakayekuwa kiongozi wa nchi hiyo mwakani ukadidimizwa.
Malema ambaye hakuwepo kwenye makao makuu ya chama chake wakati hukumu hiyo ilipotolewa, amepewa siku 14 kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Kamati hiyo ya ANC imempata Malema na hatia ya kuvuruga mkutano wa ANC, kukivunjia hadhi chama hicho kwa kudai mageuzi ya utawala nchini Botswana na kuchochea migawanyiko ndani ya chama hicho.

Viongozi wengine wa Umoja wa Vijana wa ANC, akiwemo msemaji wake Floyd Shivambu, wamesimamishwa katika nyadhifa zao kwa muda wa miaka mitatu.

Hata hivyo, kamati hiyo haikumpata Malema na hatia kwenye kosa la kuchochea ubaguzi wa rangi.

No comments: