Sunday, July 24, 2011

Seneta wa Marekani aahidi kusaidia wafugaji


Joseph Lyimo,Simanjiro
SENETA wa Jimbo la Oregon, nchini Marekani, Jacks Winter, ameahidi kuboresha miundombinu katika Kijiji cha Lengasti, wilayani Simanjiro,ili kuziwezesha jamii za wafugaji kuondokana na matatizo yanayowakabili.

Seneta Winter alitoa ahadi hiyo juzi alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji hicho, kilichoko katika Kata ya Naisinyai.

Alisema kwa kushirikiana na watu wa jimbo lake, atahakikisha kuwa wananchi wa Lengasti wengi wao wakiwa ni jamii ya wafugaji, wanapiga hatua za kimaendeleo.

Winter alisema lengo la ziara yake katika Wilaya ya Simanjiro, lilikuwa ni kujifunza mambo mbalimbali ya jamii na kutambua matatizo yanayowakabili wananchi wake.

Alisema tayari ameshajifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na namna ya kuwasaidia wananchi wa eneo hilo, kuondokana na matatizo.Seneta Winter alisema kwa kushirikiana na watu wa Jimbo la Oregon, atahakikisha wananchi wa Lengasti wanatengenezewa miundombinu bora.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Naisinyai, Kilempu Ole Kinoka, alimshukuru seneta huyo kwa kuwachimbia wananchi mabwawa mawili yanayoyatumiwa kwa shughuli za jamii na mifugo.

Alisema kwa sasa wakazi wa kijiji hicho, wanakabiliwa na tatizola ukosefu wa nishati ya umeme kwa ajili ya kuendeshea mtambo wa kuvutia maji ya kunywa na matumizi mengine.

"Huko nyuma wanawake katika kijiji hiki walikuwa wanasafiri kwa umbali wa kilometa 15 wakitafuta maji, lakini sasa maji tatizo hio limepungua hasa baada ya kuchimbiwa mabwawa mawili,"aisema.

No comments: