Sunday, July 24, 2011

Nishati wafanya ufisadi kwa miaka minne

YABAINIKA JAIRO ALIHUSIKA MIAKA MIWILI, KAFULILA AWASHTAKI KWA JK
Neville Meena, Dodoma
IMEBAINIKA uchotaji wa mamilioni ya fedha katika Idara na taasisi za umma zilizoko chini ya Wizara ya Nishati na Madini kugharamia shughuli zinazohusiana na gharama za bajeti ya wizara hiyo, ulianza mwaka 2004.

Kuanzia Julai 2008, kila mwaka Ofisi ya Katibu Mkuu katika wizara hiyo imekuwa ikiandika barua kwa wakuu wa taasisi hizo kutaka fedha ambazo kwa namna moja au nyingine zinahusishwa na shughuli za bajeti ya wizara kusomwa bungeni au kughramia sherehe ambazo hufanyika baada ya kupitishwa kwa bajeti husika.

Fedha hizo kwa mujibu wa nyaraka husika, zimekuwa zikitumika kugharamia tafrija mara baada ya bajeti kupitishwa na bunge, posho za vikao, posho za kujikimu, vyakula, vinywaji na mafuta ya magari.

Hata hivyo mmoja wa watumishi wa idara ambazo zimekuwa vinara wa kudaiwa fedha wakati wa bajeti alilithibitishia Mwananchi Jumalipi kwamba, wakati wa vikao vyote vya Bunge kila taasisi huwagharamia watumishi wake wanaokwenda Dodoma.

"Mara nyingi wakati wa vikao vya bajeti huwa nakuja hapa Dodoma, lakini utaratibu wa kukaa hapa lazima nijaze fomu ofisini na ipitishwe kwa mabosi wangu ndipo napewa fedha za kuishi, wizara hawawezi kukupa hela," alisema mtumishi huyo na kuongeza:

"Sana sana hapa tukiwa na kazi huwa tunakunywa chai na luch (chakula cha mchana) na hii siyo kila siku, ni kama tuna kazi zinazotuunganisha na wenzetu kutoka ofisi nyingine na maofisa wa wizara."

Matumizi mabaya ya fedha hizo za umma yamebainika kipindi ambacho Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara hiyo, David Jairo, amesimamishwa na Ikulu kwa kupewa likizo ya malipo, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa bungeni dhidi yake.

Jairo anakabiliwa na tuhuma za kuwaandikia barua wakuu wa idara zote zilizoko chini ya wizara yake, ili watoe fedha kwa ajili ya kusaidia kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo, fedha ambazo zinatafsiriwa kwamba zilikuwa ni kwa lengo la kutoa rushwa kwa wabunge.

Kafulila ashtaki kwa JK
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila(NCCR - Mageuzi), jana aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa amemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete akitaka uchunguzi utakaofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali katika Wizara ya Nishati na Madini uanzie miaka ya mitano iliyopita.

"Nimemwandikia barua Rais Kikwete, maana inaonekana kuwa huu mchezo wa kuchota fedha za Umma katika wizara hii umeanza tangu 2008," alisema Kafulila ambaye pia aliwahi kuwalipua baadhi ya wabunge wenzake, akiwatuhumu kwamba waliomba rushwa katika
Halmashauri ya Handeni, mkoani Tanga.

Kafulila katika barua yake ambayo pia Mwananchi limeiona, alisema anakubaliana na hatua za awali za kumchunguza Jairo, lakini anapendekeza ufanyike uchunguzi mpana kwani mtindo si kwa mwaka huu pekee bali hata miaka iliyopita katika wizara hiyo na nyingine nchini.

"Napenda kupendekeza kwako kuwa suala hili lifanyiwe uchunguzi mpana kwa kuwa upana wa kashfa hii ni zaidi ya mwaka mmoja wa fedha 2011/2012, ni zaidi ya Katibu Mkuu mmoja, David Jairo na pengine ni zaidi ya wizara moja ya Nishati na Madini, katika hicho kinachoelezwa kuwa ni kusaidia uwasilishaji wa bajeti," inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Katika barua yake kwa Rais na kutoa nakala kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Uttoh na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), Kafulila anasema ana ushahidi unaothibitisha baadhi ya tuhuma hizo.

Uzoefu wa Jairo
Kwa mujibu wa nyaraka ambazo Mwananchi limeziona, hii ni mara ya pili kwa Jairo akiwa Katibu Mkuu katika wizara hiyo kuandika waraka wa kuomba fedha kutoka kwenye idara husika kwa ajili ya kusaidia mchakato wa maandalizi na uwasilishaji wa bajeti bungeni.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, Mei 12, mwaka jana Jairo akiwa Katibu Mkuu, aliandika waraka kwenda kwa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Stephen Mabada akitaka lichangie Sh20 milioni ili kusaidia kile alichokiita, ‘Gharama za kukamilisha mpango na bajeti ya wizara 2010/2011 na uwasilishaji wake bungeni."

Barua kama hiyo pia iliandikwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura), Haruna Masebu, ambaye taasisi yake iliombwa kuchangia Sh25 milioni, wakati Yona Killagane ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), taasisi yake ilitakiwa kuchangia Sh20 milioni.

Kwa mujibu wa barua hizo, gharama husika kwa ajili ya kazi hiyo ya kibajeti ilikuwa ni Sh186.6 milioni hivyo kuzitaka idara zote kwa pamoja kuchangia kiasi cha Sh90 milioni, wakati wizara ilibaki na jukumu la kuchangia kiasi cha Sh96.6 milioni.

Hata hivyo jumla ya fedha zilizoombwa kutoka Ewura, Tanesco na TPDC ni Sh65 milioni, ikimaanisha kuwa ipo idara au taasisi nyingine ambayo pia iliombwa kuchangia kiasi kilichobaki cha Sh25 milioni.

"Gharama hizi kubwa zimesababishwa na kupanda kwa gharama za posho kutoka Sh60,000 mpaka Sh200,000, Sh50,000 hadi Sh150,000 na Sh30,000 hadi Sh100,000 kwa wenyeviti na makatibu, wajumbe na sekretarieti sawia," inaeleza sehemu ya waraka huo uliondikwa na Jairo na kuongeza:

"Kwa kuwa bajeti ya wizara ya 2009/2010 ilikadiriwa kwa viwango vya zamani, ni dhahiri wizara haiwezi kubeba gharama hizi peke yake. Hivyo inashauriwa Wizara igharamie 96,626,000 na wadau muhimu wa wizara wagharamie 90,000,000".

Barua hiyo haifafanui kuhusu wenyeviti, makatibu, wajumbe na sekretarieti ambao wanapaswa kulipwa posho hizo.

Miaka iliyopita
Mwananchi limethibtisha kuwa "utaratibu" huo wa kuchota fedha umekuwepo kwa muda mrefu, kwani mwaka 2008 na 2009 Wizara hiyo iliandika barua kwa ajilia kutaka "ichangiwe" ili kughramia shughuli za kibajeti.

Julai 5, 2008 aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi, aliandika wakara kwa Dk Idris Rashid, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Lutengano Mwakahesya na Killagane wa TPDC akitaka mchango wa kile alichoeleza kuwa ni
"Kuchangia gharama za hafla fupi baada ya mawasilisho ya bajeti ya wizara bungeni Dodoma".

Katika waraka wake huo, Mwakapugi alitaka kila taasisi kuchangia kiasi cha Sh5 milioni, hivyo kufanya jumla yake kuwa Sh15 milioni kwa lengo la kugharamia tafrija husika.

Juni 19, 2009 Mwakapugi aliandika waraka mwingine kwenda Tanesco, REA na TPDC akitaka michango kwa ajili ya kile alichokieleza katika barua yake kuwa ni "Fedha kwa ajili ya kuwezesha uwasilishaji wa hotuba ya bajeti ya 2009/2010 bungeni Dodoma, kazi ambayo anasema katika barua hizo kwamba, gharama zake ni Sh170,461,500.

"Kama ilivyo desturi, maofisa, taasisi na mashirika yaliyo chini ya wizara hujumuika katika kutoa michango yao hasa katika hoja zote zinazojitokeza katika maeneo husika. Ili kufanikisha zoezi hilo, gharama mbalimbali huhitajika zikijumuisha, posho za vikao, uchapishaji wa vitabu, uchapishaji kwenye magazeti, vyakula na vinywaji posho za safari na mafuta kwa washiriki," inaeleza sehemu ya barua.

Barua hiyo inabainisha kuwa msingi wa kutaka kuchangiwa ni kutokana na hali mbaya kifedha katika wizara hivyo na kuwataka Tanesco kuchangi Sh40 milioni, REA Sh30 milioni na TPDC Sh40 milioni.

Likizo ya Jairo
Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo ambaye ni Mkuu wa Utumishi wa Umma aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma Alhamisi wiki hii kuwa Jairo ambaye yuko chini yake, analazimika kwenda likizo kuanzia juzi ili kupisha uchunguzi wa awali ambao unalenga kubaini iwapo ametenda kosa la kinidhamu kwa mujibu wa sheria zinazoongoza Utumishi wa Mmma.

Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo ndiye aliyemlipua Jairo Bungeni Julai 18, 2011 wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini akisema amekusanya fedha kiasi cha Sh1 bilioni kutoka idara 21 zilizopo chini ya Wizara yake, fedha zisizo na maelezo.

"Nimeanzisha uchunguzi wa awali kwa lengo la kupata ukweli kuhusu tuhuma hizo. Wakati uchunguzi huo ukiendelea, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini amepewa likizo ya malipo kupisha uchunguzi wa awali," alisema Luhanjo na kuongeza:

"Hatua zitakazochukuliwa hapo baadaye zitategemea matokeo ya uchunguzi wa awali".

Licha ya mchakato wa hatua dhidi ya mtumishi huyo wa umma ambaye ni mteule wa Rais kupitia katika mchakato mrefu, mwishoni mwa mchakato huo anaweza kushushwa cheo, kupunguzwa mshahara, kufukuzwa kazi, kuachishwa kazi au kurejeshwa kazini kwa kutegemea matokeo ya taratibu zitakazofuatwa.

Luhanjo alisema Jairo analazimika kwenda likizo kwa kuwa tuhuma dhidi yake ni nzito. "Zingekuwa tuhuma nyepesi ningeruhusu aendelee na kazi wakati uchunguzi huo wa awali ukifanyika, lakini tuhuma hizi ni nzito mno. Hivyo lazima aende likizo ili kupisha uchunguzi huo," alisema Luhanjo.

Alisema uchunguzi dhidi ya Jairo kwa kuwa unahusu masuala ya fedha, utafanywa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo inatakiwa kikamilisha kazi yake katika muda wa siku kumi kisha kuiwasilisha kwake kwa hatua zaidi.

Taarifa ya Luhanjo ambayo ni taarifa rasmi ya Serikali inatofautina na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwamba suala la kuchukua kwa hatua dhidi ya Jairo linamsubiri Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Afrika ya Kusini.

No comments: