Friday, November 11, 2011

Mamlaka ya rais yagawa Kamati ya Katiba


KAMATI ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala imeshindwa kufikia mwafaka kuhusu muswada wa Sheria ya Mapitio na Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011 unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni Jumatatu ijayo.

Habari kutoka ndani ya kikao cha kamati hiyo, jana zinasema wajumbe hao bado wamegawanyika kuhusu suala la sheria inayokusudiwa kutungwa kumpa Rais mamlaka makubwa katika mchakato huo wa kupatikana kwa katiba mpya.

Habari hizo zinaeleza kwamba wanabishania wanachodai kuwa ni muswada huo kumpa Rais madaraka makubwa ambayo ni pamoja na kuteua wajumbe wa tume ya Kukusanya Maoni, sekretarieti ya Tume hiyo na wabunge 116 kuingia katika Bunge la Katiba.

“Kwa hali hii Katiba inaweza kuwa ni mali ya Rais, maana hata wajumbe wa sekretarieti anatakiwa kuteua yeye! Hii ni 'too much' (imezidi). Kwa maana hiyo, mchakato mzima unashikwa na Rais mwenyewe,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.

Taarifa zaidi zinasema kutokana na mvutano huo, suala hilo sasa limechukua mtizamo wa itikadi za vyama, na kwamba wajumbe ambao ni wabunge wa CCM katika kamati hiyo wameanza kulegeza msimamo na kukubaliana na mapendekezo ya Serikali, huku wabunge wa upinzani wakitaka kufanywa kwa marekebisho.

Kwa mujibu wa habari hizo, wajumbe hasa wale kutoka upinzani wanataka madaraka ya Rais yapunguzwe kwa kuipa Tume ya Kukusanya Maoni kutoka kwa wananchi ndiyo ipewe mamlaka ya kuteua sekretarieti yake badala ya suala hilo kufanywa pia na Rais.

Juzi, Waziri wa Katiba na Sheria, Celine Kombani aliliambia Mwananchi kuwa tatizo la wanaodai kuwa Rais ana madaraka makubwa hawatoi mapendekezo mbadala na jinsi ya kurekebisha pendekezo hilo.

“Sasa Rais ndiye aliyepo, kwa nini hawataki kumwamini wakati alipigiwa kura na wananchi wengi? Lakini, basi waseme wao wanatakaje,” alisema Kombani.

Mmoja wa wajumbe alisema: “Mahali tunapofika, ni kama kila mmoja ataondoka na msimamo wake kwenda nao bungeni. Hata leo, mbele ya Waziri (Kombani) tumeshindwa kufikia mwafaka, sasa hiyo siyo dalili njema."

Hali hiyo ya kutoafikiana miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo inatoa ahueni kwa Serikali kuweza kupitisha mapendekezo yake bila kupata upinzani mkubwa kutoka kwa kamati hiyo kama ilivyokuwa awali.

Vikao vya Kamati hiyo vimekuwa vikivuta wabunge wengi hata ambao si wajumbe wake, ili kufuatilia kinachoendelea kwenye meza ya majadiliano baina ya wajumbe husika kwa upande mmoja, kamati na Serikali kwa upande mwingine.

Kutokana na unyeti wa suala la katiba, Spika wa Bunge Anne Makinda aliongeza wajumbe watano katika Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ili kupanua wigo wa mjadala wa suala hilo.

Makinda aliliambia Mwananchi mwanzoni mwa wiki hii kuwa wabunge hao watano wanaruhusiwa kupiga kura kwenye uamuzi. “Kikanuni hawa niliowateua mimi wanaruhusiwa kupiga kura na nimefanya hivyo kutokana na unyeti wa suala lenyewe,” alisema Makinda.

Wajumbe hao ni Mwanasheria Mkuu wa zamani na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila, Mbunge wa Simanjiro (CCM) Christopher Ole Sendeka, Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed pamoja na Deogratius Ntukamazina ambaye ni Mbunge wa Ngara (CCM).

Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011, sasa utasomwa bungeni kwa mara ya pili na umetengewa siku tatu kwa ajili ya kujadiliwa kabla ya kupitishwa na Bunge.

Muswada huo ulisomwa kwa mara ya kwanza Bungeni Aprili 5, mwaka huu, lakini, ukarejeshwa Serikalini ili kufanyiwa marekebisho kadhaa na kuandikwa kwa Kiswahili kabla ya kurejeshwa tena Bungeni.

Kutokana na hali hiyo Serikali ilipata upinzani mkali kutoka kwa wabunge na wanaharakati ambao walidai kwamba muswada huo ulipaswa usomwe kwa mara ya kwanza kutokana na kufanyiwa marekebisho makubwa tofauti na ule wa awali.

Hata hivyo Kombani alisema juzi kuwa: “Muswada huu uliposomwa kwa mara ya kwanza haukuondolewa, bali ulipelekwa kwa umma ili ukajadiliwe”.

“Mabadiliko mengi yanayolalamikiwa yalitokana na hoja za wananchi, hii ni ishara kwamba tulizingatia hizo hoja, sasa kwa mujibu wa taratibu za miswada ni kwamba utasomwa kwa mara ya pili, kama mnavyoona kwenye ratiba,” alisema Kombani.

Mkurugenzi wa Huduma za Bunge, John Joel aliliambia Mwananchi kuwa kwa mujibu wa taratibu, muswada huo hauwezi kutangazwa tena katika Gazeti la Serikali wakati ulishatangazwa Machi mwaka huu.

Ratiba ya Mkutano wa Tano wa Bunge inaonyesha kuwa Muswada huo utasomwa kwa mara ya pili Jumatatu, Novemba 14 mwaka huu na kuendelea kujadiliwa na Jumanne, Novemba 15 na Jumatano Novemba 16 mwaka huu.

Hatua ya muswada huo kupangwa kusomwa kwa mara ya pili, inatafsiriwa kuwa ni “ushindi” kwa Serikali dhidi ya waliokuwa wakipinga hatua hiyo kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikiwa ni wananchi kupewa muda zaidi kwa ajili ya kuujadili.

Mjadala wa muswada huo utatanguliwa na semina kwa wabunge wote itakayofanyika kesho Jumamosi hatua inayotafsiriwa kuwa ni kujaribu kupunguza hoja ambazo zinaweza kujitokeza na pengine kuukwamisha.

Baadhi ya wanaharakati wanaopinga muswada huo kusomwa kwa mara ya pili ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Jukwaa la Katiba ambao wameenda mbali na kudai kuwa Waziri Kombani, amechakachua muswada huo.

No comments: