Waandishi Wetu
TUKIO la Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kuachia nyadhifa zote za uongozi ndani ya CCM, limepokelewa kwa hisia tofauti baada ya watu wa kada mbalimbali kutoa maoni tofauti huku baadhi yao wakimsifu na wengine kumponda.
Hata hivyo, chama hicho tawala kimeeleza kuwa hakijapata taarifa rasmi za uamuzi huo wa Rostam ingawa yeye alisema jana kuwa, barua yake ya kujiuzulu aliikabidhi kwa mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Baadhi ya wanasiasa wamemponda mwanasiasa huyo, huku wasomi na baadhi ya viongozi wa dini wakisema kuwa hatua yake hiyo ni sahihi katika mwenendo wa sasa wa siasa ndani ya chama hicho.
Kwa mujibu wa wasomi na viongozi hao wa dini, hatua hiyo ya Rostam imeelezwa kuwa ni mfano kwa viongozi wengine wa chama na Serikali yake wanaojiona kuwa wanaelemewa na tuhuma mbalimbali.
Mwanasheria maarufu nchini, Profesa Abdallah Safari alisema kuwa, uamuzi huo ni ujumbe kwa viongozi wengine wa CCM wanaonyoshewa kidole kila kukicha.
“Kwa maoni yangu, uamuzi huo umemsaidia Rais Kikwete kwani kati ya watu waliokuwa wakinyoshewa sana vidole, mmoja wao ameamua kujiondoa, kwa kweli amemwondolea mtihani, lakini pia itasaidia chama ambacho nacho kilikuwa kikinyooshewa sana vidole,” alisema Profesa Safari.Hata hivyo, alisema hatua hiyo ya viongozi kujivua nyadhifa zao haitatosha kukisafisha chama hicho dhidi ya maovu.
“Kuna ubadhirifu mwingi ambao unatakiwa ufanyiwe kazi, mambo mengine kama EPA na Richmond hayawezi kumalizwa kwa watu kujivua nyadhifa zao,” alisema msomi huyo.Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally, alisema hotuba ya Rostam aliyoisoma mbele ya wazee wa Igunga, inaonyesha kwamba amejiuzulu kwa shingo upande.
“Nimesoma hotuba yake yote, lakini inaonyesha wazi kwamba ameachia nyadhifa ndani ya chama hicho ikiwa ni kutekeleza kauli ya CCM ya kujivua gamba, inaonyesha kwamba amechukua uamuzi huo kwa shingo upande,” alisema Bashiru,
CCM: Hatujapata barua yake
Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alilieleza Mwananchi jana kuwa mpaka wakati huo chama hicho hakikuwa kimepokea taarifa hizo rasmi na kwamba hata wao walizipata kupitia vyombo vya habari jana, hivyo hawapo katika nafasi nzuri ya kutoa tamko linaloweza kuwa msimamo chama.
"Hata sisi (CCM) tumepata taarifa hizo kupitia vyombo vya habari kama nyinyi, hivyo hatuwezi kutoa msimamo wa chama kwa sasa," alisema Mukama.
Rostam: Barua yangu ipo kwa Mwenyekiti
Hata hivyo, Rostam mwenyewe akizungumza na Mwananchi jana, alisema tayari alishamwandikia barua Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kuhusu uamuzi wake huo.
Alifafanua kwamba, CCM ndiyo yenye mamlaka na inayopaswa kulieleza Bunge kwamba kiti hicho kiko wazi.
Alisema tangu kutangaza uamuzi huo, hadi jana mchana tayari alikuwa amepata salamu na ujumbe mfupi (sms) kutoka kwa wanachama 11,872, wa CCM ambao walimpongeza kutokana na hotuba yake.
Kwa mujibu wa Rostam, wanachama hao walikubaliana naye kuhusu siasa uchwara zinazoendeshwa na chama hicho katika kipindi hiki, hadi kuamua kuchukua uamuzi huo.
Rostam alisema mbali na ujumbe wa simu, pia alipata simu kutoka kwa wanaCCM wengi Kanda ya Ziwa ambapo waliunga mkono hotuba yake. Inaelezwa kuwa Rostam ana ngome kubwa ya wafuasi kwenye mikoa ya Kigoma, Mara, Mwanza, Tabora na Shinyanga.
Nape akwepa
Kwa upande wake, Katibu wa Idara ya Itikadi ya Uenezi, Nape Nnauye, alisema hakuwa na la kusema juu ya tuhuma ambazo ametupiwa na Rostam kupitia hotuba yake ya kujivua nyadhifa zake.
Wakati akizungumza na aliowaita wazee wake juzi, Rostam alituhumu Sekretarieti ya CCM kwamba ilieneza kwa kupotosha nia njema ya Mwenyekiti wao (Rais Kikwete) katika dhana ya chama hicho kujivua gamba akisema kuwa, ilienezwa kwa tafsiri na mwelekeo tofauti na ule wa awali.
"Wajumbe wawili wa Sekretarieti, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), John Chiligati na Katibu wa Idara ya Uenezi, Nape Nnauye, walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ilifikia uamuzi wa kuwapa siku 90 wale walioitwa watuhumiwa wa ufisadi kujitoa katika nafasi zao za uongozi vinginevyo watafukuzwa na chama," inaeleza sehemu ya hotuba hiyo ya Rostam.
Hotuba hiyo ilieleza kuwa viongozi hao walikaririwa na vyombo vya habari wakieleza kuwa majina ya watuhumiwa hao yalikuwa yakifahamika kutokana na kuhusishwa katika kashfa za Richmond, EPA na ununuzi wa rada na hatimaye walitaja majina ya wanasiasa watatu kuwa ndiyo ambao walilengwa na uamuzi huo.
Rostam Aziz alisema kuwa jina lake kutajwa katika orodha ya watuhumiwa hao ni ufinyanzi wa porojo na fitina za kisiasa, ambao ulimshangaza, kutokana na namna uamuzi halisi wa Nec, hususan kuhusu 'kujivua gamba'¯ ulivyopindishwa na wajanja wachache kwa maslahi binafsi ya kikundi fulani cha watu.
Alisema mshtuko na mshangao wake umejikita katika viongozi wa chama hicho alichotumikia kwa bidii na uaminifu mkubwa, kufanya juhudi kubwa hata kufikia hatua ya kukivisha kikao alichokiita kitukufu cha Nec uamuzi ambao msingi wa hoja zake ni vita vya kimakundi ya siasa ndani ya CCM, propaganda za vyama vya siasa vya upinzani na vyombo vya habari kwa upande mwingine.
Katika hotuba yake, Rostam alieleza kushangazwa na kushtushwa kwake na ujasiri ambao viongozi wa Sekretarieti mpya ya CCM wamekuwa nao, kiasi cha kutaja jina lake kwa kulihusisha na kile wanachokiita ufisadi ambao hata kimsingi ushahidi wa wazi umethibitisha kuwa ni porojo za kisiasa zinazotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule ujao wa 2015.
Mkoani Kilimanjaro
Askofu Msaidizi wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo, alisema hakuamini aliposikia taarifa hizo, lakini baadaye aliamini na kusema mbunge huyo amesoma alama za nyakati.
“Ni uamuzi mgumu aliouchukua, lakini ulistahili kwa mazingira ya siasa za Tanzania na amesoma vizuri alama za nyakati…na wengine wote wanaotajwa kuwa na tuhuma nao wafuate nyayo hata kama hazijathibitishwa,”alisema Shoo.
Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri, Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi (MUCCoBS), Michael Tiruhungwa, alisema Rostam angewatendea haki Watanzania kama angejielekeza zaidi kwenye tuhuma anazohusishwa nazo.
Naye Mtaalamu Mshauri wa Huduma za Biashara, Akwiline Kinabo, alisema kujiuzulu kwa Rostam ni mwanzo tu na kama kweli CCM imedhamiria kujivua gamba, basi Watanzania watarajie mengi makubwa zaidi ya kujiuzulu.
Kutoka Mwanza
Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Wilson Mushumbusi, alisema uamuzi wa Rostam kujiuzulu umetokana na wakati mgumu wa kisiasa alionao.
Mushumbusi alifafanua kwamba mbunge huyo amekuwa akituhumiwa kwa kashfa nyingi, kujiuzulu kwake ni mwanzo wa mafanikio ya Chadema juu ya madai ya ufisadi ambayo yanamkabili.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) Mkoa wa Mwanza, Josephat Ngolangwa alisema Rostam ameonyesha ukomavu wa kisiasa na uamuzi wake umekinusuru chama.
Alifafanua kwamba, hatua hiyo inadhihirisha Rostam ni muumini wa dhati wa chama chake na kuwataka wengine waliotuhumiwa ndani ya chama na hata katika Serikali, wafuate nyayo za Rostam ili kurejesha imani kwa chama.
Alisema CCM kama taasisi ya kisiasa inafanya uamuzi kutokana na vikao na haya yote yanayotendeka ni uamuzi wa vikao vya chama wa kuwataka viongozi wote kusimamia uamuzi wa vikao vya chama ngazi ya juu.
Kwa msisitizo, alisema kwa sasa viongozi wana kazi kubwa ya kuimarisha chama na siyo wakati wa kujadili nani atakuwa rais katika kipindi kijacho cha mwaka 2015 kwa kusema kuwa 2015 ni mbali sana.
Mkoani Tanga
Nako mkoani Tanga watu wamepokea uamuzi huo wa Mbunge wa Igunga kwa mitazamo tofauti, huku wengine wakitaka mapacha wenzake ambao wamekuwa wakitajwa na viongozi wa CCM kuhusika na tuhuma za ufisadi wafuate nyayo zake.
Wasomi na wanasiasa waliozungumza na gazeti hili jana walisema kung’atuka kwa Rostam Aziz ni tukio ambalo lilitarajiwa.
Mkereketwa wa CCM, Tarafa ya Mlalo, Wilayani Lushoto, Zahabu Mjata alisema kitendo cha Rostam kuachia ngazi ni cha kiungwana na kwa hiyo hastahili kusakamwa kama inavyofanywa na baadhi ya watu.
Friday, July 15, 2011
Uamuzi wa Rostam kung'atuka watikisa nchi
Posted by Mafia Kisiwani at 9:51 AM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment