Leon Bahati, Dodoma, Ramadhan Semtawa, Dar
WAKATI uamuzi wa Rostam Aziz kung'atuka ubunge wa Igunga na ujumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) ndani ya chama chake cha CCM ukiibua gumzo kubwa karibu kila kona nchini, mshirika wake mkubwa kisiasa, Edward Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli ameeleza kushtushwa na tukio hilo.Juzi, Rostam, mmoja wa watu muhimu ndani ya CCM aliyeshiriki vyema katika mtandao uliomwingiza madarakani Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005, alitangaza uamuzi mzito wa kung'atuka siasa akipinga kile alichokiita siasa uchwara za baadhi ya viongozi wake.
Uamuzi huo mzito wa Rostam uliibua kwikwi na vilio kutoka kwa wapigakura jimboni kwake Igunga, wakiwamo wale waliomchagua kwa vipindi vitatu mfululizo tangu mwaka 1994 ulipofanyika uchaguzi mdogo kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Charles Kabeho. Jana, Lowassa alisema: "Kwa kweli nimeshtushwa, nimesikitishwa...kilichonishtua zaidi ni vilio. Namna wananchi wa Igunga walivyokuwa wanalia na kusikitika."
Hata hivyo, Lowassa ambaye naye amekuwa akitajwa katika orodha ya watu watatu wanaopaswa kuachia nafasi zao za uongozi CCM katika kile kinachoitwa chama kujivua gamba, alipoulizwa kuhusu taarifa za yeye kufuata njia ya mshirika wake huyo alijibu: "Siku ikifika nitatoa uamuzi na nitajibu wakati ukifika."
Lowassa alikuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari katika Viwanja vya Bunge mjini Dodoma, kuhusu alivyopokea uamuzi huo wa Rostam na kama yuko tayari kufuata mfano na njia hiyo ya kujiuzulu nyadhifa zote ndani ya CCM.
Lakini, juzi Rostam aliweka bayana kwamba uamuzi wake wa kujiuzulu hautokani na shinikizo lolote ikiwamo kile kinachoitwa mpango wa kujivua gamba, bali aliufanya uamuzi huo kuepuka kuathiri biashara zake kutokana na kuchafuliwa na siasa uchwara akieleza kuwa yeye ni mfanyabiashara wa kimataifa, lakini akaahidi kuendelea kuwa mwanachama mtiifu wa CCM.
Hata hivyo, Lowassa jana hakutaka kufafanua kuhusu kauli yake hiyo ya "Nitajibu wakati ukifika," ingawa alionyesha tabasamu wakati akiulizwa na kujibu swali hilo la iwapo atafuata nyayo za Rostam au la.
Mshirika wao mwingine, Andrew Chenge, jana alivumishiwa kuandaa mkutano na waandishi wa habari ili naye atangaze uamuzi wa kujiuzulu nafasi zake zote kama hatua ya kutekeleza azimio la Nec la kujivua gamba.
Lakini, alipotafutwa kwa simu na kuulizwa kuhusu taarifa za yeye kutaka kujiuzulu, Chenge alijibu kwa kifupi kuwa alikuwa Uingereza, kitu kilichothibitisha kuwa hakukuwa na mpango huo wa kujiuzulu huku akisisitiza: "Mimi niko nje ya nchi, nipo Uingereza."
Hivi karibuni, Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi, maarufu kama Mzee wa Vijisenti, aliwahi kuliambia gazeti hili: "Sijui kama mimi ni gamba CCM," huku akisisitiza kwamba anaheshimu taratibu za chama na asingeweza kukurupuka na kuanza kuzungumza mambo ya chama nje ya utaratibu.
Chenge alisema chama kina utaratibu wake wa kufanya maamuzi, hivyo kuanza kutoka nje ya taratibu na kuzungumzia mambo ya ndani ya chama isingekuwa rahisi kwake kwani anaheshimu taratibu zilizopo.
..Sendeka asifu ujasiri wa Rostam
Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole-Sendeka, ambaye amekuwa akijipambanua kama mpambanaji wa ufisadi, alisema kujivua kofia zote alizokuwa nazo Rostam ni kitendo cha kuletea afya chama tawala.Sendeka alifafanua kwamba kuwapo kwa vigogo wanaotuhumiwa kwa rushwa ndani ya CCM ni sawa na mtu anayeugua na ili apone lazima waondoke ili chama kipate afya njema.
Alisema kutokana na sababu hiyo, anamuunga mkono Rostam kwa uamuzi wake aliochukua wa kutii uamuzi wa chama wa kujivua gamba, kwani ni hatua moja ya kukiboresha chama na kuongeza: "Unaposhauriwa kwa afya ya chama chako na ukakubali ni uamuzi wa kijasiri."
Hata hivyo, alionya kwamba mkakati huo wa kujivua gamba ni zaidi ya vigogo watatu ambao wamekuwa wakitajwa mara kwa mara.Sendeka alisema wote wakifuata mkondo wa Rostam, chama kitajijengea taswira nzuri ya kupendwa na watu ambao tayari wameanza kukata tamaa kutokana na kuona haya kutokana na tuhuma zinazowahusu.
Kuhusu wale ambao bado hawajatekeleza hilo, ole-Sendeka alisema: "Cheo ni dhamana, uongozi ni utumishi, kama wale waliokupa dhamana wanakushauri uondoke, huna haja ya kubishana, tekeleza."Naye Ally Mohamed (Nkasi Kaskazini-CCM), alisema amefurahishwa na hatua ambayo Rostam ameichukua kwa lengo la kusafisha chama.
Lakini, akasema ni wakati mwafaka wa kuhakikisha CCM inasafishika mbele ya Watanzania kwa sababu, kuwapo kwa watuhumiwa hao wa ufisadi wanaozungumzwa mara kwa mara, kulionekana kuchafua chama chote."Sasa ni wakati wengine nao wachukue uamuzi kama huo. Tunajua wako wengi, waondoke chama kiimarike," alisema Mohamed.
Tundu Lisu azungumzia uamuzi wa Rostam
Tundu Lissu (Singida Mashariki-Chadema), alisema bado gamba la CCM halijavulika kwa sababu Rostam ni mmoja wa watuhumiwa 11, ambao walitajwa na Chadema kwenye orodha ya mafisadi, Mwembeyanga, Temeke mwaka 2007.
"Bado kumi," alisema Lissu huku akijigamba kuwa mafanikio hayo ni juhudi zilizofanywa na Chadema ili kulinda rasilimali za Watanzania ili zitumike vizuri.
Kuhusu kauli ya Rostam kuwa amejing'oa kwenye nyadhifa zake kutokana na "siasa uchwara", Lissu alijibu: "Kama kweli siasa uchwara ndizo zimemwondoa Rostam, basi ndizo zinazofaa kuendelezwa hapa nchini."
Ingawa Rostam alikataa kuhusisha uamuzi wake na kujivua gamba, tangu kikao cha Nec cha Aprili, Sekretarieti mpya ya CCM imekuwa ikitangazia umma orodha ya makada wake watatu ambao wanapaswa kujiuzulu ili kuleta kile inachokiita heshima kwa chama na kukisafisha.
Friday, July 15, 2011
Lowassa: Nimeshtushwa
Posted by Mafia Kisiwani at 9:53 AM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment