Sunday, July 24, 2011

Madiwani Chadema 'ngangari'

Moses Mashalla, Arusha
MADIWANI watatu wa Chadema waliotakiwa kujiuzulu nyadhifa zao katika Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kufikia saa 7:02 mchana jana, wamegoma kufanya hivyo na badala yake wameutaka uongozi wa taifa wa chama hicho kuwasafisha kwa kuwataka radhi.

Kauli hiyo ya madiwani hao akiwamo Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Estomi Mallah imekuja siku chache baada ya kuvuja kwa ripoti ya kamati iliyoundwa na Chadema kuchunguza mwafaka wa madiwani wake, wa CCM na TLP katika kumpata Meya wa jiji hilo ikibainisha kuwa hakukuwa na tuhuma za rushwa katika mchakato huo.

Badala ya kujiuzulu, madiwani hao wametoa masharti magumu kwa chama hicho, licha ya kutaka kusafishwa, pia wamemtaka Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuwasafisha kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kueleza umma kwamba hawakuhongwa.

Mallah ambaye ni mwenyekiti wa madiwani hao alisema jana kuwa wamekitaka chama chao kuwaomba radhi kupitia vyombo vya habari kwa kuwa ripoti hiyo imebainisha ukweli wa mambo. Alisema taarifa za wao kuhongwa zilizotolewa na uongozi wa chama chao ziliwasababishia usumbufu mkubwa ndani ya jamii zao kiasi cha kufanya baadhi yao kunusurika kupigwa mawe.

Akizungumzia agizo la kujiuzulu nyadhifa ndani ya manispaa hadi kufikia jana saa 7:02, alisema wamepanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwa kuwa hawakutendewa haki. Mallah aliutaka uongozi wa Chadema kutambua misingi ya haki huku akibanisha kuwa migogoro ya ndani kwa ndani huenda ikakipeleka mahali kubaya akisema kama kuna tatizo, linapaswa kutatuliwa kupitia vikao na si vinginevyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Uchumi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Elerai (Chadema), John Bayo alikwenda mbali akimtaka Lema kupita katika maeneo yote ya Jiji la Arusha kuwasafisha mbele ya wananchi kutokana na tuhuma alizozitoa kuwa walipokea rushwa.

Chadema kimetofautiana na madiwani hao kwa kile inachoeleza kuwa wamepingana na msimamo wa chama hicho kutotambua mwafaka katika mgogoro wa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinapinga jinsi muafaka huo ulivyofikiwa kikisema haukufuata misingi ya kisheria ba kwamba ili mwafaka upatikane mambo kadhaa yalipaswa kujadiliwa kwa pamoja ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wa chama hicho kutokana na maandamano yaliyofanyika mapema mwaka huu kupinga matokeo ya uchaguzi wa meya, kulipwa fidia kwa familia za marehemu waliokufa kwenye maandamano hayo na uchaguzi wa meya wa jiji hilo kurudiwa.

Uongozi wa taifa wa chama hicho unaona kwamba kitendo cha madiwani hao kukubali nyadhifa ndani ya Baraza la Madiwani wa Jiji la Arusha kabla mambo hayo hayajatekelezwa, kimetafsiriwa na Kamati Kuu ya Chama hicho kuwa ni usaliti uliotokana na rushwa.

Wahudhuria kikao cha halmashauri ya jiji

Licha ya madiwani hao kupuuza agizo hilo la makao makuu ya Chadema, jana walihudhuria kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa kikifanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kama kawaida huku baadhi yao wakisema sasa wameamua kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi waliowachagua ili kuwaletea maendeleo na kuweka pembeni tofauti za kisiasa.

Dk Slaa alipoulizwa jana kuhusu msimamo wa madiwani hao, alisema Katiba ya Chadema itachukua nafasi yake katika kuamua suala hilo akisema asingependa kuibua malumbano katika suala hilo wala kutunishiana misuli. Alisema diwani yoyote anayeona kwamba hakutendewa haki ana haki ya kwenda mahakamani.

"Katiba ya Chadema itakwenda kufanya kazi, kamati kuu iliwataka wajiuzulu mara moja kama wamekataa sasa katiba itachukua mkondo wake na yoyote anayeona alichafuliwa yuko tayari kwenda mahakamani," alisema.

Mgogoro huo wa umeya Arusha ulisababisha mauaji ya watu watatu katika maandamano yaliyofanyika Aprili mwaka huu, mmoja wao akiwa ni raia wa Kenya baada ya Chadema kuamua kuandamana kwa nguvu bila kibali cha polisi.
SOURCE:Mwananchi

No comments: