Neville Meena, Dodoma
RUSHWA inayodaiwa kupenyezwa kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeathiri uamuzi wa baadhi ya hatua ambazo kamati hiyo inapaswa kuchukua dhidi ya udhaifu uliobainika katika hesabu za fedha na miradi inayotekelezwa na halmashauri ambazo tayari zimefanyiwa ukaguzi.
Kwa kawaida kamati hiyo inapofanya ziara katika halmashauri kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake, hubainisha udhaifu katika maeneo husika na kutoa mapendekezo au hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya udhaifu husika na wakati mwingine hutoa au kupendekeza adhabu wanazopaswa kupewa wahusika.
Sehemu ya tatu ya nyongeza ya nane ya Kanuni za Bunge, toleo la mwaka 2007 inabainisha kuwa LAAC ina wajibu wa kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali za Mitaa yaliyoainishwa katika taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
"Kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali za Mitaa yaliyoainishwa katika Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali," kinaeleza kipengele cha 12(a) cha sehemu hiyo.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa taarifa ya Kamati ndogo ya LAAC, iliyokuwa mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, Mei 22- 28, 2011 inatia shaka kutokana na tofauti kubwa ya mapendekezo yaliyotolewa dhidi ya udhaifu uliobainishwa katika muhtasari wa kumbukumbu za kamati hiyo.
Kutokana na udhaifu wa taarifa hiyo, baadhi ya wajumbe ambao walikuwa katika msafara huo wa Tanga wameikana wakidai kwamba wajumbe waliopewa kazi ya kuiandika, 'waliichakachua'.
"Hii ripoti iliandikwa na (anawataja wabunge wawili), nasikia hata Mwenyekiti (Augustino Mrema) hakuwapo kutokana na dharura lakini tuliwaamini, ila walichoandika wanakijua wenyewe," alilalamika mmoja wa wajumbe wa kamati.
Kwa mujibu wa muhtasari huo, kamati hiyo ndogo iliyoongozwa na Mrema kwenda Tanga ilibainisha udhaifu katika vipengele kumi na moja kwenye miradi ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na kutoa mapendekezo 10 ya namna ya kuchukua hatua.
Kadhalika, kamati hiyo inatoa maelekezo kwa lugha kali na kupendekeza hatua za kinidhamu kwa baadhi ya watendaji wa halmashauri za wilaya Muheza na Jiji la Tanga kutokana na kubaini uzembe katika usimamizi wa baadhi ya miradi ya maendeleo inayosimamiwa na mamlaka hizo. Lakini, jambo linalotia shaka ni jinsi kamati hiyohiyo ilivyoshughulikia matatizo yaliyojitokeza katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwani ilibainisha upungufu uliowekwa katika vipengele 12, lakini ikatoa mapendekezo matatu tu ya jumla ya jinsi ya kukabiliana na kasoro hizo.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alisema "udhaifu" unaobainika katika uandishi wa hatua za kuchukua dhidi ya watendaji wa Handeni, unaweza kuwa uthibitisho wa tuhuma zilizotolewa dhidi ya baadhi ya wajumbe wa LAAC kwamba waliomba rushwa kwa uongozi wa halmashauri hiyo.
Tuhuma hizo ni zile zilizotolewa Juni 13, mwaka huu na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo kwamba aliwakamata wajumbe wenzake watatu wakiomba rushwa kwa viongozi wa Halmashauri ya Handeni.
Katika maelezo yake bungeni, Kafulila aliwataja wabunge wawili kati ya watatu anaowatuhumu kuwa ni Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi na Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Badwel na kwamba taarifa za tukio hilo alikuwa amekwishaziwasilisha kwa Mrema na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Yaliyojiri Lushoto, Handeni
Taarifa ya kamati hiyo ndogo ya LAAC kuhusu Halmashauri za Mkoa wa Tanga inaweka bayana kwamba katika ziara yake wilayani Lushoto Mei 23, mwaka huu kamati hiyo ndogo ilijadili hesabu za halmashauri hiyo na kubaini kuwa kwa miaka mitatu mfululizo, imekuwa ikipata hati zenye shaka za ukaguzi wa CAG.
Miongoni mwa udhaifu mkubwa uliobanishwa ni malipo ya Sh117 milioni ya mishahara kwa watumishi hewa, kiasi cha Sh15 milioni kutumika nje ya bajeti, Sh65 milioni kukusanywa kwa kutumia stakabadhi za kughushi, uchache wa fedha zilizopelekwa katika shule za msingi ikilinganishwa na kiasi kilichotolewa na Hazina na kutopelekwa kwa Sh75 milioni ambazo ni ruzuku ya lazima ya Serikali Kuu kwa ajili ya maendeleo vijijini.
Wilayani Handeni, kamati hiyo pia ilibaini udhaifu kadhaa ikiwa ni pamoja na kiasi cha Sh18 milioni cha malipo ya mishahara kwa watumishi hewa, kutoonekana kwa lambo la kunyweshea maji mifugo lililodaiwa kujengwa eneo la Madebe kwa gharama ya Sh35.5 milioni na kutokuwapo kwa vitasa pia sakafu kubomoka katika soko la Sindeni ambalo limegharimu Sh24.5 milioni.
Udhaifu mwingine katika Halmashauri ya Handeni ni kutopeleka vijijini kiasi cha Sh105 milioni kwa ajili ya kufidia kodi zilizofutwa na matumizi ya mabati 466 ambayo yanadaiwa kutumika kujenga vyumba vinne tu vya madarasa ya Shule ya Sekondari Segera.
Hatua zilizochukuliwa
Pamoja na udhaifu huo, Kamati hiyo ndogo inatoa mapendekezo ambayo mmoja wa wajumbe wake anayaita kuwa ni "dhaifu" yasiyolingana na uzito wa kasoro zilizobainishwa katika Halmashauri ya Handeni.
Mapendekezo hayo ni matatu ambayo yanaitaka ofisi ya ukaguzi ya halmashauri hiyo kujadiliana kuhusu kufungwa au kutofungwa kwa hoja ya uchakavu wa mali mbalimbali zenye thamani ya Sh520 milioni, halmashauri kuongeza bidii kudai fedha zake kiasi cha Sh133.3 milioni katika taasisi tatu tofauti na kuitaka kuweka wazi kwa madiwani na wananchi gharama zitakazotumika kujenga Bwawa la Kidereko.
"Unaona! Hii ina maanisha nini? Taarifa haisemi kitu kuhusu malipo ya watumishi hewa, wala lambo ambalo halikuonekana, wala haimwajibishi mtu yeyote hata kwa kumpa barua ya onyo. Hapa lazima kuna kitu si bure," alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye alisema hakwenda Tanga wala Pwani kwa kuwa alipata dharura wakati wa ziara hizo.
Lakini, kwa upande wa Lushoto, tofauti na Handeni, kamati hiyo ilitaka ipatiwe majina ya watumishi hewa waliolipwa mishahara husika, nyaraka za fedha na taarifa za kibenki (bank statements) pia kuagiza Mkurugenzi Mtendaji apewe barua ya onyo na mamlaka yake ya kinidhamu kutokana na uzembe uliosababisha halmashauri yake kupata hati yenye mashaka.
Pia kamati hiyo iliagiza Halmashari ya Lushoto kupeleka mara moja fedha za maendeleo vijijini ili kufidia kodi zilizofutwa na kuhakikisha makato ya malipo ya pensheni yanapelekwa katika mamlaka husika.
Makundi ya wabunge
Kwa mujibu wa muhtasari wa kumbukumbu husika, kamati ndogo iliyokuwa mkoani Tanga ilikuwa na wabunge ambao ni Mrema, Kafulila, Badwel, Zambi, Mbunge wa Kondoa Kaskazini (CCM), Zabein Mhita na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Kiwanga.
Wengine ni Katibu wa Kamati hiyo, Mswige Dickson Aswile, Mwakilishi wa Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesebu za Serikali (CAG), Denis Mbilinyi na Mary Assey ambaye alikuwa katika msafara wa wabunge hao akimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga (RAS). Kwa mujibu wa toleo la 10 la kitabu cha orodha ya wabunge cha Juni mwaka huu, LAAC ina wajumbe 17.
Mbali na wajumbe waliokwenda Tanga, wengine katika Kamati hiyo ni Makamu Mwenyekiti wa LAAC ambaye pia ni Mbunge wa Kinondoni (CCM), Iddi Azzan, Riziki Lulida (Viti Maalumu, CCM), Subira Mgalu (Viti Maalumu, CCM), Hasnain Mohamed Murji (Mtwara Mjini, CCM), Abdul Mteketa (Kilombero, CCM), Tauhida Nyimbo (Viti Maalumu, CCM), Joseph Selasini (Rombo, Chadema) na Kurthumu Mchuchuli (Viti Maalumu, CUF).
Kwa mujibu wa kitabu hicho, makatibu wengine wa kamati hiyo mbali na Aswile ni Edwin Tongora na Chipanda Chilemeji. Hata hivyo, taarifa ya ziara ya kamati ndogo ya LAAC iliyofanya ziara mkoani Pwani haikuweka bayana majina ya wajumbe waliokuwa katika msafara mkoani humo.
LAAC ni kamati ambayo ilijizolea sifa nyingi kwa jinsi ilivyoanza kazi yake kwa kasi na kuwachukulia hatua watendaji wa halmashauri kadhaa nchini ambao walithibitika kuwa dhaifu katika usimamizi wa rasilimali za maeneo yao ya kazi kiasi kwamba baadhi yao walikatwa asilimia 15 ya mishahara yao kama adhabu mojawapo.
Tuhuma za rushwa
Mbali na tuhuma zilizotolewa na Kafulila kwa wajumbe waliokuwa ziarani Tanga, pia zimetolewa tuhuma mpya kwa baadhi ya wajumbe wa kamati ndogo iliyokuwa mkoani Pwani ambako inadaiwa kuwa kiongozi wa kamati hiyo, Azzan alikuwa akikumbana na upinzani mkali pale alipokuwa akijaribu kuhoji baadhi ya mambo katika halmashauri husika.
Habari zaidi zinadai kwamba hata kamati iliyokwenda Pwani baadhi ya wajumbe wake wanatuhumiwa kuomba rushwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, ambaye baada ya kumpigia simu alitoa taarifa kwa kiongozi wa timu hiyo, Azzan.
Hali hiyo inadaiwa kuitafuna Kamati hiyo kiasi kwamba imeshindwa kukutana tangu kuanza kwa mkutano wa nne wa Bunge la bajeti, licha ya Mwenyekiti Mrema kuitisha vikao mara tatu kwa nyakati tofauti.
Mrema aliliambia Mwananchi kuwa atamweleleza Spika kuhusu hali ya kamati yake ili kupata mwongozo wa nini kinachotakiwa kufanywa. Vikao vilivyokwama ni vile vilivyotishwa Juni 16, Juni 20 na Julai 19, mwaka huu na ajenda saba zilizokuwa zimepangwa kujadiliwa zimeendelea kuwekwa kiporo.
Kikao cha Julai 19, kilikuwa kimepanga pamoja na mambo mengine, kupitia kumbukumbu ya yaliyojiri katika ziara za Tanga na Pwani, makubaliano ya kujadili taarifa za hesabu za baadhi ya halmashauri wakati kamati ikiwa bungeni, makubaliano kuhusu mwaka wa hesabu (2008/09) au 2009/10) zitakazoendelea kujadiliwa katika kipindi kijacho na Taarifa ya Katibu wa Kamati kuhusu barua kutoka kwenye halmashauri kwenda kwa Katibu wa Bunge.
Mrema katika mazungumzo yake na gazeti hili alisema: "Nikiwaita akija Kafulila baadhi yao hawaji, lakini Kafulila asipokuwepo, wengine utawaona wamefika na hapo unakuwa huwezi kuwa na kikao kinachoweza kufanya uamuzi kwa manufaa ya nchi yetu".
Habari zaidi zinadai kwamba, tuhuma za Kafulila bungeni dhidi ya Zambi na Badwel zinawatisha hata baadhi ya wale waliokuwa katika kamati ya mkoani Pwani kwani wanahofu kwamba huenda nao wakaanikwa ndani ya kikao cha kamati hiyo ya LAAC. Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aanasema ili kuinusuru kamati hiyo, ipo haja ya kuvunjwa na kuundwa upya kwani hivi sasa ni kama imesambaratika kwani wajumbe husika hawaaminiani.
"Ni bora ikaundwa upya, kazi hazifanyiki na sasa tuna viporo kwa sababu hesabu za mwaka 2009/2010 bado kabisa hatujazigusa na mwezi Aprili mwakani lazima tuwasilishe taarifa bungeni, sasa tutawasilisha nini kama kazi hazifanyiki?" Alihoji mjumbe huyo.
Kanuni za Bunge
Pamoja na Kanuni ya 114 (3) kusema kwamba kamati zinaweza kukutana kila itakapotakiwa kufanya hivyo na Spika, Naibu Spika au Mwenyekiti wa Kamati husika kwa idhini ya Spika, kanuni hizo haziweki wazi hatua zitakazochukuliwa ikiwa wajumbe wa kamati watashindwa kukutana kama ilivyotokea kwa LAAC.
Ama kanuni za 113 (6) na (7) zinaeleza kuwa ujumbe wa mbunge katika kamati unaweza kukoma ifikapo mwishoni mwa mkutano wa kumi wa uhai wa bunge, ikimaanisha kuwa hakuna mbunge anayeweza kuodoka katika kamati yake ya sasa hadi mkutano wa kumi utakapofikia ukomo.
Huu ni Mkutano wa Nne wa Bunge la 10 na Mkutano wa 10 unatarajiwa kufanyika ifikapo Oktoba 2012, wakati kamati za kudumu za bunge zitakapopangwa upya.
Kwa maana hiyo ni vigumu kwa sasa LAAC kufanyiwa marekebisho kwa mujibu wa kanuni au kuundwa upya, isipokuwa Spika aamue kutumia vifungu vingine vya kanuni vinavyompa mamlaka ya kifanya jambo kadri anavyoona yafaa.
Sunday, July 24, 2011
Ripoti Maalumu:Tuhuma za rushwa zaivuruga Kamati ya Mrema
Posted by Mafia Kisiwani at 10:05 AM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment