Friday, July 15, 2011

Mtei amshika pabaya Wassira

Moses Mashalla, Arusha
MUASISI wa Chadema hapa nchini, Edwin Mtei "amemshika pabaya" Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais (mahusiano na uratibu) ,Stephen Wassira akitaka ajiuzulu kwa kulala bungeni.

Pamoja na kupongeza picha ilivyotoka gazetini, alisema kitendo cha kigogo huyo kuuchapa usingizi bungeni kimedhibitisha jinsi Serikali ya Rais Jakaya Kikwete isivyokuwa makini na kumtaka Wassira ajiuzulu mara moja.

Mtei,alitoa kauli hiyo siku moja kupita baada ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro wakiwamo wasomi kuunga mkono hatua ya gazeti hili kumpiga picha waziri huyo akiwa amelala bungeni huku wakisema kuwa ni sahihi na kubeza kauli ya waziri huyo kuwa kitendo hicho ni uchochezi.

Akizungumza na gazeti hili, Mtei alisema kitendo cha waziri huyo kusinzia bungeni kimemdhalilisha yeye mwenyewe pamoja na Serikali ya Rais Kikwete na kusisitiza kwamba Serikali haiko makini kutatua kero za umma.

"Kitendo cha Wassira kusinzia bungeni kimetuonyesha ni jinsi gani Serikali ya CCM isivyokuwa makini kutatua kero za umma,amejidhalilisha
kwanza yeye mwenyewe, lakini pia wananchi anakotoka na Serikali nzima mimi namshauri aachie ngazi tu"alisema Mtei.

Alisema mara kwa mara chama chao kimekuwa kikiilaumu Serikali kwa kutokuwa makini na kero zinazoligusa taifa hivyo kitendo cha waziri huyo kuuchapa usingizi bungeni kimetoa majibu ya madai yao.

Hatahivyo, alipuuza vikali hoja ya Wassira kuwa kitendo cha gazeti hilo kumpiga picha akiwa amelala kuwa ni uchochezi huku akisema kuwa
kama alikuwa mgonjwa angeenda kupumzika nyumbani kwake na sio kusinzia bungeni.

Mtei,ambaye pia aliwahi kuwa gavana wa Benki Kuu hapa nchini alilipongeza gazeti la Mwananchi kwa kuwafichua wabunge wanaolala bungeni huku akisema kwamba kamwe lisirudi nyuma katika kusimamia maadili ya taaluma ya habari.

"Mwananchi lisirudi nyuma, mnatusaidia sana kuwafichua viongozi wanaolala bungeni bila nyie sisi tusingejua endeleeni na msiogope"alisisitiza Mtei.

Pia alizungumzia kero ya mgao wa umeme uliolikumba taifa na kusema kuwa Serikali ya Rais Kikwete imeshindwa kutatua kero za taifa hali ambayo imesababisha taifa kuendelea kuwa maskini.

Alisema kuwa kero ya mgao wa umeme ni mzigo mkubwa wa Watanzania ambao hauvumiliki huku akionya ya kuwa endapo hali hiyo isipotatuliwa mara moja huenda nchi ikaingia katika matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na vijana kukosa ajira,viwanda kufungwa kwa kushindwa kufanya kazi na uchumi kuporomoka.

SOUCE:MWANANCHI

No comments: