Leon Bahati, Dodoma
MTAZAMO tofauti miongoni mwa wabunge umeendelea kuwa chachu ya kutaka kuvunjwa kwa muungano wa Tanzania.Hali hii imejionyesha wazi wiki hii katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma baada ya wabunge kuvutana kuhusu hatima yake, huku baadhi yao wakitaka uvunjwe na kuundwa upya na wengine kuutetea.
Chanzo cha mvutano huo ni kufutia baadhi ya wabunge kutoka Zanzibar kuubeza na kuonyesha wazi kuwa Tanzania bara inanufaika zaidi kuliko visiwani.
Hoja hii si tu kwamba iliwakoroga wabunge wa bara, bali pia wananchi walioisikia wamekuwa wakihoji sababu za wabunge hao kuubeza muungano kana kwamba hauwasaidii.
Kauli tata kuhusu muungano ambazo kwa ujumla zinadhoofisha uhusiano baina ya pande hizo mbili, ulianza muda mrefu hasa baada ya nchi kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya saisa na unaendelea kukua kadiri muda unavyosonga mbele huku Serikali ikifanya jitihada za kuunusuru.
Katika mvutano ulioibika bungeni wiki hii, wabunge wa Chadema na baadhi wa Chama cha Wananchi (CUF), walioonekana dhahiri kutaka muundo wa sasa wa Muungano huo uvunjwe na kuundwa mwingine wenye serikali tatu; Tanganyika, Zanzibar na Serikali ya Muungano.
Hata hivyo, mfumo huo umekuwa ukipingwa kila mara kwa vile ni sawa na kumwondole madaraka na nguvu Rais wa shirikisho kwa vile hatakuwa na uwezo kuingilia mambo ya ndani ya serikali ya mbili zitakaozoundwa.Hata hivyo, wakati wabunge hao wakitetea hoja hiyo, wengine kutoka Chama tawala CCM, na baadhi ya mawaziri akiwamo Samuel Sitta wa Afrika Mashairiki, walisimama kudete kuutetea.
Hoja za wabunge
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alishutumu tabia ya viongozi waliopo madarakani kuficha ukweli juu ya suala zima la muungano akiweka bayana kuwa sasa ni wakati mwafaka Watanzania wakajadili hatima ya Muungano huo.
Akitumia vitabu vya watu mashuhuri kama vile Rais wa Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe na Profesa Issa Shivji, Lisu
alisema matatizo na kero nyingi zinatokana na baadhi ya mambo kutowekwa wazi.Alitaja baadhi ya mambo aliyosema siri kuwa ni juu ya Mapinduzi ya Zanzibar na lengo hasa lililolazimu uwepo wa muungano huo.
Mambo mengine alisema ni kuingizwa kinyemela kwenye katika ya Tanzania vipengele kuanzia cha 11 hadi 22.Halima Mdee wa Kawe, alisema kero za muungano zimekuwa hazitatuliwi kutokana na waziri mwenye mamlaka ya muungano kupuuzwa na viongozi wenye mamlaka ya juu katika kuamua kusu suala hilo.
Aliwataja viongozi hao ambao alidai hawana muda wa kutulia ili kutafuta ufumbuzi wa kero hizo kutokana na kuwa na kazi nyingi kuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Alilalamika kuwa kutokana na hali hiyo ni kero sita tu zimetatuliwa, huku saba ambazo ni za msingi, zikiendelea kupigwa danadana.Miongoni mwa kero hizo sugu, alizitaja kuwa ni suala la mafuta, ushiriki wa Afrika Mashariki na suala sahihi za waanzilishi wa Muungano huo.
"Suala la kodi mbili ni kiini macho na kwamba wananchi wengi wamekuwa wakiathirika kutokana na tatizo hilo," alieza Mdee ambaye alipendekeza Katiba ijayo kuwa na mwanga wa kutatua kero za muungano.
Mohamed Amour Chomboh (Magomeni) alitamba kuwa yeye ni miongoni mwa watu wachache walioshuhudia Mapinduzi ya Zanzibar yalivyofanyika na anatambua ni muhimu kuenziwa.Alisema anaona kuna umuhimu wa muungano huo kuendelea kudumu lakini, akaasa kuwa kero zake zimekuwa ni tishio kubwa hasa kwa maslahi ya Zanzibar.
Alilalamikia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa ndio moja ya kero ambazo zinaweza kusababisha Wazanzibari waje juu na hata kutaka kuvunja Muungano.Alisema Zanzibar inategemea zaidi bishara kwa ajili ya kuimarisha uchumi wake na kwamba TRA ndiyo imekuwa ikisababisha biashara kudorora visiwani humo.
Waziri atwishwa mzigo
Jaddi Sumail Jaddi (Mkwajuni-CCM) alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Hassan Suluhu ,ambaye ni Mzanzibar alikabidhiwa nafasi hiyo kama mtego wa kumbebesha lawama za kero za Muungano ambazo zinalalamikiwa na Wazanzibar.
"Ndugu yangu Samia ni mchawi aliyepewa mtoto amlee akimnyonga, alamumiwe yeye," alisema Jaddi.
Sitta alisema huo ni upotoshaji na kwamba alipewa kazi hiyo kwa vile Serikali inaamini kwamba ana uwezo wa kuifanya kazi hiyo.
Yalikuwepo malalamiko kwamba Wazanzibar wanaoajiriwa Bara ni wachache, lakini Sitta alipinga akitoa mfano wa wizara yake ina maofisa wakuu wa idara 12 na kati ya hao, wanne ni Wazanzibari.
Sitta awatuliza
Munkali wa wabunge hao ni kama ulizimwa na Sitta ambaye alifanikiwa kubadili kabisa hali ya hewa iliyokuwa inaashirikia kuwa wabunge wengi wanataka Mungano huo uvunjwe.
Akichangia mjadala huo Sitta alisema siku ambayo Watanzania wataamua kuwa na serikali tatu za muungano, itakuwa ndiyo tiketi ya kuuvunja muungano huo.
"Kuunda tena Tanganyika ni kutengeneza mbia mwingine atakayekuwa anashindana na Zanzibar," alisema Sitta.
Alifafanua kuwa hali hiyo itajenga mazingira ya mvutano kwa serikali ya Tanganyika na Zanzibar wa kila mmoja kupigania maslahi yake na Serikali ya Muungano haitakuwa na nguvu kwa sababu uwepo wake utategemea pande hizo mbili.
Alitoa mfano akisema linaweza kujitokeza suala la kuchangia uendeshaji wa Serikali ya Muungano na hapo yanaweza kujitokeza malalamiko kwamba pande zote zigharimie sawa kwa sawa na hapa Zanzibar ndiyo itakayonyanyasika.
Sitta ambaye alikuwa Spika katika Bunge lililopita alionya akisema kama ni mpango wa kuunda serikali tatu ni bora waridhie kabisa muungano usiwepo na serikali zote zijitegemee.
Alitaka ieleweke kwamba wakati inaonekana kuwa Wazanzibar ndio wanaoonekana kulalamika sana wakati huu kwamba wananyimwa maslahi yao lakini ukweli wapo Watanzania Bara ambao nao wanalalamika vivyo hivyo ila nguvu hiyo inapungua kutokana na kuwepo serikali mbili.
Amtetea Nyerere
Kuhusu Baba wa Taifa kuwa dikteta, Sitta alisema kuwa huo ni upuuzi kwa sababu yapo matendo mengi ambayo yanaonyesha hakuwa mlafi wa madaraka na badala yake alipenda haki kwa wananchi wake na bara la Afrika kwa Ujumla.
Alitoa mfano kuwa kama angekuwa dikteta angeweza kuamua kufuta kabisa uwepo wa serikali ya Zanzibar.
"Lakini alikubali iendelee kuwepo serikali ya Zanzibar ndani ya Muungano," alisema Sitta ambaye pia ni mbunge wa Urambo Mashariki.
Katika kuelezea kuwa Karume hakuwa mtu wa kuburuzwa alisema, Tanzania ilipoishiwa akiba ya fedha za kigeni na kwenda kuiomba serikali ya Zanzibar iwapatie kwa sababu wao walikuwa nazo nyingi kutokana na mauzo ya karafuu, alikataa.
Kuhusu suala la picha ya siku ya Muungano kuonekana Mwalimu Nyerere peke yake akichanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar, Sitta alisema ni suala tu la heshima ambalo alipewa kutokana na wadhifa wake wa Rais wa Muungano.
Alifafanua kuwa siku hiyo waliteuliwa watu wawili, mwanauma na Mwanamke, kutoka pande zote kushiriki katika kufanikisha tukio hilo lililoandika historia ya Tanzania.
Hoja nyingine aliyopangua ni ile ya wabunge wengi kueleza kuwa katiba ilibadilishwa ili Rais wa Zanzibar asiwe tene Makamu wa Kwanza wa Rais tofauti na makubaliano ya waasisi wa muungano kwa hofu ya CCM kwamba Rais wa visiwani anaweza kutoka chama cha upinzani.
Sitta alisema ukweli ni kwamba mabadiliko hayo yalitokea baada ya kuona kwamba nafasi hiyo ya pili itaonekana kuwa ni ya Wazanzibari tu, kwa vile serikali ya Zanzibar daima itaongozwa na mzanzibar.
Zanzibar na OIC
Kuhusu suala la kutaka Zanzibar iruhusiwe ijiunge na Jumuia ya Nchi za Kiislamu Duniani (OIC) kwa vile Tanzania imeamua kutofanya hivyo, Sitta alisema tatizo ni kwamba kanuni haziruhusu.
Alisema kwamba OIC ilikataa kufanya hivyo kwa vile sheria zao ni kujenga ushirikiano na serikali ile inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.
Kuhusu kipengele cha kwanza hadi 11 viliundwa kwa makubaliano ya pande zote lakini baadaye kifungu cha 12 hadi 22 vikaingizwa kinyemela, Sitta alisema, sio kweli.
Kwa mujibu wa Sitta vipengele hivyo vilitokana na kuvunjika kwa Jumuia ya Afrika Mashariki 1977 ambapo baadhi ya mambo mengi yaliyokuwa yanasimamiwa na ushirikiano huo yalibaki bila usimamizi.
Alitaja miongoni kuwa ni Shirika la Posta, reli, bandari na ndege ambapo Tanzania Bara ilibidi iyabebe baada ya rais wa Zanzibar kuridhia.
Hata hivyo alisema Tanzania bara ilibeba jukumu hilo kwa gharamna zake bila kuishirikisha Zanzibar hiyo ikawa ni nafuu kwa Wazanzibar kwa sababu faida zake zinaenda pande zote za Muungano.
Kama hiyo haitoshi, Sitta alisema rais wa Zanzibar aliiomba Bara ianzishe pia elimu ya juu kwa sababu isingeweza kufanya hivyo kutokana na uwezo wa kifedha.
Akipinga malalamiko kwamba Zanzibar haina uwakilishi kwenye Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Sitta alisema katika vikao vyote vya majadiliano visiwa hivyo vimekuwa na uwakilishi.
Isitoshe akasema kuwa katika kuthamini Zanzbar, EAC inajiandaa kuwekza katika miradi mitatu visiwani humo ambayo ni ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa Pemba, ujenzi wa Bandari ya Maruhubi na chelezo ya kusafirisha mizigo na magari Zanzibar, Mombasa na Dar es Salaam.
SOURCE:MWANANCHI
Friday, July 15, 2011
MZIMU WA SERIKALI TATU WARUDI BUNGENI
Posted by Mafia Kisiwani at 9:48 AM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment