Wednesday, November 10, 2010

Uspika vita mpya CCM

na Kulwa Karedia




BAADHI ya vigogo na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameanza mikakati mizito kuhakikisha aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, hapitishwi na chama hicho kutetea kiti chake.

Uchaguzi wa Spika wa Bunge utafanyika Novemba 12 mwaka huu baada ya Kamati Kuu (CC) ya CCM, kupeleka majina matatu kwenye mkutano wa wabunge wote wa CCM ambao nao huteua jina moja la kuwania nafasi hiyo na kulipeleka kwa Katibu wa Bunge kwa ajili ya kupigiwa kura na wabunge wote.

Tanzania Daima Jumapili, imedokezwa kuwa Sitta ameanza kuhujumiwa na vigogo hao ambao baadhi yao wanahusishwa na tuhuma za ufisadi, kwa madai kuwa alishindwa kuliongoza Bunge vizuri katika kipindi cha utawala wa Awamu ya Nne.

Sitta anashutumiwa kwa kuruhusu mijadala mikali ambayo ilihatarisha kuanguka kwa serikali iliyokuwa ikiendeshwa na CCM kiasi cha kuwafanya wabunge wa chama hicho kugawanyika.

Mpaka sasa wanachama wasiopungua tisa wameshajitokeza kuwania nafasi hiyo akiwamo aliyekuwa Naibu Spika, Anne Makinda, Andrew Chenge, Job Ndugai, Kate Kamba na Anna Abdallah.

Wakati joto likipanda, duru za kisiasa ndani na nje ya CCM zimedokeza kwamba chama hicho kinakabiliwa na mpasuko mkubwa unaotokana na vita ya makundi, hasa baada ya Edward Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008, kutokana na kashfa ya Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond.

Vita hiyo mpya inalenga kila kundi kujiwekea mazingira ya ushindi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, pamoja na nafasi za wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama (NEC) na Kamati Kuu (CC).

Harakati hizo za makundi zimechagizwa zaidi na matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 31, mwaka huu ambapo CCM ilipoteza takriban majimbo 52 Tanzania Bara na Visiwani.

Duru za kisiasa zimeidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa kundi linalompinga Sitta limekuwa likihaha huku na huko kuhakikisha jina hilo linaishia Kamati Kuu.

Hofu inayojengwa na kundi hilo ni kuwa Sitta si kiongozi wa kumuamini hasa katika kipindi hiki ambacho wapinzani wameongezeka na CCM inapita katika kipindi kigumu kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kundi hilo, linaloongozwa na watu wenye fedha na wanaotuhumiwa kwa kushiriki kwenye vitendo vya kifisadi, linadaiwa kumtumia Katibu Mkuu, Yusuph Makamba, kushawishi wanachama wakongwe na wenye nguvu ili wagombee, kwa lengo la kumuangusha Sitta.

Sitta, ambaye ameshinda ubunge Urambo Mashariki, tayari ameshachukua fomu za kutetea kiti chake huku akijinasibu kuwa kwa Bunge la sasa yeye ndiye mwenye uwezo wa kuliendesha.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Sitta alisema CCM itafanya makosa kama itawachagua viongozi au vibaraka wao wenye masilahi binafsi katika nafasi ya uspika.

“Wenzenu wengine waliniuliza maswali kama haya mnayoniuliza, maneno yangu ni haya, Mungu akitaka kukuangamiza hakupi nuru mbele, anaendelea kukuweka gizani ili akuangamize vizuri.

“CCM tunapaswa kujiuliza kwa nini tulipata tabu katika uchaguzi uliopita, si kuangalia mtu mmoja jamani,” alisema Sitta.

Alisema anajua mikakati mingi mizito juu yake, yenye lengo la kuhakikisha harudi kwenye kiti hicho, lakini akasisitiza, anaamini mwenyekiti wa chama hataruhusu mipango hiyo kukiangamiza chama.

“Ni kweli wapo watu wanaopita huku na huko kunichafua, nawaambia wasubiri vikao vya chama vitaamua, natoa wito kwa wagombea wanaotumiwa wagonje vikao vya juu.

“Yupo kiongozi mmoja wa juu ndani ya chama anasimamia juhudi hizi, anapigia wagombea simu kwenda kuchukua fomu, wanapitia kwake, ukizingatia wengine wanapitia kwa mkuu wa idara hii, inazua maswali mengi,” alisema Sitta.

Naye mgombea mwingine ambaye alikuwa Naibu Spika, Anne Makinda, alipoulizwa kama anawania kiti hicho kutokana na msukumo wa baadhi ya watu, alisema kuwa ametumwa na dhamira yake kufanya hivyo na si kwa sababu ya utashi wa mtu au kundi la watu fulani.

Hata hivyo, duru zaidi za kisiasa zilisema, mkakati huo pia unasukwa Zanzibar na kusimamiwa na mmoja wa mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye mara kwa mara alikuwa akitajwa kwenye malumbano ya ndani na nje ya Bunge.

Habari hizo ziliongeza kwamba, katika mkutano uliofanyika visiwani humo juzi, mmoja wa vigogo wa CCM, aliweka bayana msimamo huo, akisema Sitta ni mtu hatari, hapaswi kurudi.

“Spika wa serikali iliyopita lazima ang'oke, haiwezekani mtu aliyetusumbua arudi tena, katika awamu hii Wazanzibari lazima tuwe na msimamo wa pamoja,” alisema kigogo huyo.

Mkakati huo unasimamiwa na vigogo watatu, akiwamo waziri mmoja mwanamke, ambao wameapa jina la Sitta kutopita katika Kamati Kuu.

Tayari waziri huyo mwanamke (jina tunalo), amekuwa akitamba kwa kuomba ushawishi kuhakikisha wanamshughulikia Sitta.

“Kilichopo ni kuhakikisha wanaingia watu zaidi ya 10, wakiwamo wenye majina makubwa ili Sitta akiangushwa katika CC ionekane si kwa sababu ya chuki binafsi,” kilidokeza chanzo kimoja.

Tayari kuna mpango wa kumshawishi Balozi Gertrude Mongella, kuhakikisha naye anachukua fomu na wakati wowote kama akikubali huenda akachukua.

Vyanzo vyetu hivyo viliongeza kwamba, Anna Abdallah ni miongoni mwa vigogo waliopewa jukumu la kupunguza idadi ya kura za Spika Sitta.

Chanzo kimoja kimedokeza kuwa kundi hilo linalompinga Sitta, linataka mbunge wa Bariadi Magharibi, Anderw Chenge, awe spika ili aweze kuwadhibiti wapinzani pamoja na makada wa CCM ambao walijipambanua kuwa ni wapambanaji wa ufisadi.

“Kundi linalomuunga mkono Chenge, linaamini kuwa Sitta akipata nafasi ya kurejea kwenye kiti hicho hataweza kuwakabili wapinzani, kwa sababu katika Bunge lililopita alionekana kuwapa uhuru zaidi kiasi cha kuitikisa serikali na CCM,” alisema.

Makada hao wanaamini katika wakati wa sasa Chenge ndiye mwenye uwezo wa kuponya majereha yaliyoipata CCM wakati wa utawala wa Awamu ya Nne, ikiwamo kupoteza majimbo yasiyopungua 20.

Chanzo hicho kimeendelea kudokeza kuwa kundi linalomuunga mkono Chenge pia limekuwa likifanya utaratibu wa kuwasiliana na viongozi wa juu wa serikali ya Uingereza ili wamsafishe Chenge na kashfa ya rada iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya sh bilioni 40 badala ya sh bilioni 20.

Kampuni ya BAE System ya Uingereza ndiyo iliyoiuzia Serikali ya Tanzania rada hiyo, ambapo Chenge alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali.

No comments: