na Irene Mark
RAIS Jakaya Kikwete anatarajia kulihutubia Bunge la kwanza, Novemba 17, mwaka huu baada ya kupitishwa kwa jina la Waziri Mkuu na kupatikana spika.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema jina la waziri mkuu litapitishwa siku hiyo asubuhi kisha jioni, rais kulihutubia Bunge kwa mara ya kwanza na kuahirishwa kwa mkutano wa kwanza wa Bunge.
Kwa mujibu wa katibu huyo, mkutano wa kwanza wa Bunge, utaanza Novemba 12 kwa wabunge wote kufanya uchaguzi wa spika ambaye ataapishwa siku hiyo.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete anatarajiwa kutoa mwelekeo wa serikali yake hususan juu ya hali ya uchumi na jinsi atakavyotekeleza ahadi lukuki alizozitoa wakati wa kampeni.
Alisema baada ya spika kupatikana, ataanza kuwaapisha wabunge wengine, shughuli itakayofanyika kwa siku tatu mfululizo hadi Novemba 16 ambapo jioni ya siku hiyo, utafanyika uchaguzi wa Naibu Spika wa Bunge.
“Hivi sasa wabunge wanakwenda Dodoma kwa ajili ya kutambuliwa, huko wanapeleka vyeti walivyopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi… kazi rasmi za Bunge zitaanza Novemba 12 kama alivyoelekeza rais.
“Baada ya kupatikana kwa Naibu Spika, siku inayofuata, yaani Novemba 17 asubuhi, wabunge watalipitisha jina la waziri mkuu lililopendekezwa na rais halafu ataapishwa. Jioni rais atalihutubia Bunge na waziri mkuu atatoa hoja ya kuahirisha Bunge,” alieleza Dk. Kashililah.
Kuhusu uchaguzi wa spika, aliwataka makatibu wa vyama vya siasa, kuwasilisha majina ya wagombea uspika kutoka kwenye vyama vyao siku mbili kabla ya uchaguzi huo na siku moja kabla ya uchaguzi wa kumpata naibu spika.
Alisema, si lazima nafasi ya spika kuwaniwa na wabunge, bali mtu yeyote mwenye sifa ya kuwa mbunge, na kuthibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), anaruhusiwa kugombea nafasi hiyo.
Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hadi jana jioni jumla ya wanachama watano wamejitokeza kuwania nafasi hiyo inayoonyesha upinzani ndani ya chama hicho.
Spika aliyemaliza muda wake, Samuel Sitta, ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki, ameamua kutetea nafasi hiyo huku akikabiliwa na upinzani mkali kati yake na Andrew Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi.
Wengine wanaokimezea mate kiti cha uspika ni aliyekuwa Naibu Spika, Anne Makinda (Mbunge wa Njombe Kusini), Job Ndugai kutoka Kongwa na Anna Abdallah aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, ambaye katika siku za karibuni alitangaza kung’atuka kwenye siasa.
Wednesday, November 10, 2010
Waziri Mkuu kutajwa Novemba 17
Posted by Mafia Kisiwani at 11:12 AM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment