Wednesday, November 10, 2010

Majimbo 50 CCM yafyekwa

• Mnyika, Mdee waweka historia mpya Dar


na Betty Kangonga na Bakari Kimwanga




WAKATI mawaziri wa Serikali ya Rais Kikwete wakizidi kupukutishwa na wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Mapinduzi (CCM) hadi sasa kimeshapoteza majimbo 50 yaliyonyakuliwa na wapinzani.

Kati ya majimbo hayo, 32 yako Tanzania Bara na Tanzania Visiwani kuna majimbo 20 ya CCM yaliyokwenda upinzani.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo ndicho kinaongoza kwa sasa kwa kupata majimbo 24, NCCR Mageuzi majimbo manne, yote ya mkoani Kigoma, TLP na CUF, yakipata mawili kila moja na UDP, moja. Hata hivyo kuna uwezekano wa kupata majimbo zaidi, kwani zoezi la utangazaji wa matokeo bado linaendelea.

Majina ya wabunge wa CHADEMA na majimbo yao kwenye mabano ni Vincent Nyerere (Musoma Mjini), Anis Jewila (Ilemela), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Mustafa Akuunay (Mbulu), Salvatory Naluyaga (Ukerewe), Meshaki Opurukwa (Meatu), Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), Dk. Antony Mbassa (Biharamulo), Silinde David (Mbozi Magharibi), Halima Mdee (Kawe), Godbless Lema (Arusha Mjini), Sylvester Kasulumbali (Maswa Mashariki), John Shibuda (Maswa Magharibi), John Mnyika (Ubungo) na Freeman Mbowe (Hai).

Wengine ni Joseph Selasini (Rombo), Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini), Israel Yohane Natse (Karatu), Martin Ole Kisambu (Arumeru Magharibi), Profesa Kaigi (Bukombe) na Tundu Lissu (Singida Mashariki).

Majimbo yaliyotangazwa jana kuchukuliwa na CHADEMA ni pamoja na majimbo muhimu ya Ubungo na Kawe ya jijini Dar es Salaam.

Jimbo la Ubungo ambalo ushindi wake ulikuwa ukisubiliwa kwa hamu kutokana na ushindani mkali uliokuwepo, limechukuliwa na John Mnyika, wakati lile la Kawe limechukuliwa na Halima Mdee ambaye miaka mitano iliyopita alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu.

Akitangaza matokeo ya Jimbo la Ubungo, Msimamizi wa Uchaguzi, Raphael Ndungulu, alisema Mnyika, ameibuka na ushindi wa kura 66,742, dhidi ya mgombea wa CCM, Hawa Ngh’umbi, aliyepata kura 50,544 huku mgombea wa CUF Mtatiro Julius, akipata kura 12,964.

Kwa upande wake, Mnyika, alisema anawashukuru wana Ubungo kwa kumchagua na kuwaahidi kwamba hatawaangusha katika kuwatumikia.

“Napenda kuwahakikishia Watanzania, sitawaangusha na moto utawaka bungeni, kwa kuibua hoja zenye maslahi kwa taifa letu, nawashukuru sana wana Ubungo, kwani mimi ndiye chaguo lenu sahihi, hasa kwa mabadiliko ya Ubungo na taifa kwa ujumla,” alisema Mnyika.

Baada ya kutangazwa matokeo hayo, kundi kubwa la vijana lililipuka kwa furaha na kufanya maandamano huku watu wengine wakitokwa machozi ya furaha kwa ushindi huo.

Mbali na ushindi wa kiti hicho, CHADEMA pia imepata viti sita vya Kata ya Mbezi, Sinza, Ubungo, Makuburi, Saranga na Kimara.

Kwa upande wa Jimbo la Kawe, Mdee alipata kura 45,365 wakati mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Angela Kizigha, alipata kura 34,412, huku Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia, akiambulia kura 11,970.

“Ukilima shamba lazima utegemee kupata mavuno, hivyo nimepata nilichopanda kilichobaki ni kuhakikisha natetea masilahi ya wananchi hasa suala la mchezo wa upatu (DECI) wengi waliochukuliwa fedha zao ni wa kutoka jimbo hili,” alisema Mdee.

Wakati majimbo ya Ubungo na Kawe yakitangazwa, matokeo ya Jimbo la Segerea, yanaendelea kugubikwa na utata na kusababisha kutotangazwa kwa matokeo hayo.

Hali hiyo ilisababisha wafuasi wa CHADEMA jana kuvamia Ofisi za Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Arnautoglu, wakimshinikiza atangaze matokeo hayo.

Wakati wengine wakifurika kwenye ofisi za msimamizi wa uchaguzi, kundi lingine lilitawanywa kwa mabomu ya machozi, wakishinikiza kutaka matokeo ya jimbo hilo yatangazwe.

Jimbo hilo linawaniwa na Milton Makongoro (CCM) ambaye amepata upinzani mkubwa kutoka kwa mgombea wa CHADEMA, Fred Mpendazoe.

Mapema jana kulikuwa na taarifa za mmoja kati ya wagombea hao kufikishwa polisi kwa tuhuma za kukutwa na shahada za kupigia kura. Licha ya tukio hilo kuripotiwa na vyombo vya habari vya nje, polisi nchini, wamekana kuwapo kwa tukio hilo.

Kwa upande wake, msimamizi wa jimbo hilo, Gabriel Fuime, alisema matokeo hayo yamechelewa kutokana na watendaji kushindwa kufikisha taarifa zao kwa wakati.

Katika hatua nyingine, mawaziri wengine waliopata kuwamo ndani ya serikali ya Rais Kikwete, wamepoteza majimbo yao.

Mawaziri hao ni pamoja na Lucas Siame na Philip Marmo, ambao wameangukia pua na majimbo yao kuchukuliwa na wagombea wa CHADEMA.

Dk. Siame (Mbozi Magharibi), ambaye amepata kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Maafa na Ukimwi), ameangushwa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), David Silinde.

Msimamizi wa Uchaguzi, Levisson Chilewa, alisema Silinde ameshinda kwa kupata kura 20,835 wakati Siyame amepata kura 20,203, huku mgombea wa CUF, Aloyce Kabange aliambulia kura 220.

Kwa upande wa udiwani, CCM inaongoza kwa kupata viti 12 vya udiwani, CHADEMA viwili, huku CUF ikiambulia patupu.

Kuhusu matokeo ya Jimbo la Mbozi Mashariki, msimamizi huyo alimtangaza Godfrey Zambi kuwa mshindi.

Zambi alipata kura 49,095, Mtela Mwampamba (CHADEMA), kura 31,997, Kunyuntila Siwale (CUF), kura 839.

Katika Jimbo la Mbulu, mgombea wa CHADEMA, Akuunaye Mustafa, amefanikiwa kumwangusha Marmo.

Marmo ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), ameambulia kura 27,210 dhidi ya kura 48,428 alizopata Akuunay.

No comments: