Friday, July 1, 2011

Vijiji 165 kupata umeme wa MCA-T

Thursday, 30 June 2011 20:02
0digg

Steven William,Muheza



VIJIJI karibu 165 vilivyopo katika wilaya za Mkoa wa Tanga vitanufaika na nishati ya umeme kufuatia Mradi wa Changamoto Millennium Challenge (MCA-T) unaofadhiliwa na Marekani kuanza zoezi la kuimarisha miundo mbinu ya nishati hiyo.



Hayo yalisemwa juzi na mratibu wa mradi huo Yusuph Mkindi katika warsha ya siku mbili iliyofanyika Tanga na kushirikisha wafanyakazi wa halmashauri za wilaya nne ambako mradi huo utapita.

Alisema mradi huo unatarajia kuanza kutekelezwa mapema mwezi ujao na kwamba kwa sasa wanajiandaa kufanya zoezi la kuwalipa fidia wakazi waliopo pembeni ambako miundo mbinu ya umeme itapita.



Mkindi alisema zoezi la kulipa fidia hiyo litaanza rasmi Julai 20, mwaka huu ambapo baada ya kuwalipa wataanza zoezi hilo.

Akifafanua zaidi alisema tayari mkandarasi atakayehusika na mradi huo amepatikana na tayari nguzo za umeme zimeshaanza kusambazwa katika vituo ambavyo vimepangiwa kupita mradi huo katika wilaya husika.



Mkindi alisema kuna vituo 16 ambavyo vimetengwa kwa ajili ya kufunga mashine maalumu za kupoozea nguvu za umeme katika Jiji la Tanga, Wilaya za Lushoto, Handeni na Muheza ambako mradi huo umepangiwa.



Kwa upande wake Ofisa habari wa mradi huo wa MCA-T, Magreth Musai alisema lengo la mradi huo ni kuwakwamua wanavijiji sehemu husika ili waweze kuondokana na umaskini kwa kutumia nishati katika miradi endelevu.

Alisema pamoja na kuwanufaisha wananchi, lakini lengo kuu zaidi ni kukuza uchumi wa Tanga kupitia sekta ya viwanda.



Naye mtaalamu wa masuala ya jinsia ,Debora Sungusia alisema kuwa pia wanatoa elimu kwa maofisa wa maendeleo ya jamii waende kuelimisha jinsia ya kike waweze kujiendeleza kiuchumi na kupewa elimu ya kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi inayofadhiliwa na Marekani.



No comments: