Friday, July 1, 2011

Zitto azidi kuichoma Serikali

Thursday, 30 June 2011 20:52
0digg

Kizitto Noya, Dodoma
WAKATI Bunge likiendelea kumsubiri Zitto Kabwe kuthibitisha madai yake kwamba Baraza la Mawaziri limeshawishiwa kuifuta Kampuni Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC), mbunge huyo wa Kigoma Kusini jana alionekana kusisitiza kauli hiyo baada ya kutaka itungwe sheria ya kudhibiti ushawishi kwa viongozi.

Mbali na kutaka itungwe sheria hiyo, Zitto pia alihoji "kwa nini Wizara ya Fedha tusiseme imehongwa wakati imeleta bungeni mambo ambayo hayakukubalika katika vikao vya kamati?"

Zitto alisema hayo jana alipokuwa akichangia Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka fedha 2011/12.

"Mheshimiwa mwenyekiti, mimi naomba tutunge sheria ya ‘ku-regulate lobbying’ kuratibu ushawishi), sio vizuri kumchukua Waziri Mkuu akafungue mkutano wa wawekezaji ambako atasaini pia mambo kadhaa,"alisema Zitto.
Alihoji kwa nini watu wasisemi Wizara ya Fedha na Uchumi imehongwa baada ya kalieleza Bunge kuwa imepingana na maamuzi ya kamati kutaka wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi wasipewe msamaha wa kodi kwa miaka kumi.

Kwa mujibu wa Zitto Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge na Kamati ya Mashirika ya Umma yalipinga mpango huo wa Serikali, lakini inashangaza kuona mapendekezo hayo bado yameletwa bungeni na kuthibitishwa.
"Tanzania hatuhitaji kuweka ‘incentives’ katika sekta ya mafuta na gesi kwa kuwa hatuna mshindani.

Tuliiambia Wizara ya Fedha kuwa hatuhitaji kuzipa kampuni za uwekezaji misamaha ya kodi kwa miaka ya kumi katika mafuta na gesi lakini bado haikusikia. Sasa tukisema Wizara ya Fedha imehongwa watakataaje?"alihoji.

Zitto alisema Tanzania ni tajiri katika mafuta na gesi na haina mshindani katika nchi zote za Afrika Mashariki hivyo haihitaji kuwavutia wawekezaji kwa kuwapa miasma ya kodi kwa miaka 10.

"Kilichotakiwa hapa ni sisi (Tanzania) kujenga ‘plant’ mkoani Mtwara mapema tena kabla wenzetu wa Msumbuji hawajajenga. Tukifanya hivi hatuna sababu ya kuwapa muda wa kulipa kodi wawekezaji,"alisema.

Katika mchango wake huo, Zitto pia alitaka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya uchunguzi na kubaini tatizo lililoko katika mirabaha ya madini hata ikaonekana tofauti ya hasara ya Sh 20 bilioni kati ya fedha wawekezaji wanazodai.

"Rais alienda Hait na akaahidi kulifanyia kazi suala hilo, haiwezekani kuwe na ‘descrepancy’ ya Sh20 bilioni. Inawezekana kuna mifuko miwili fedha hizo zinaenda kuwanufaisha baadhi ya watu," alisema


Katika hatua nyingine Mbunge wa Rungwe Mashariki, David Mwakyusa, aliitaka Serikali iunde tume ya kuchunguza chanzo cha migomo na maandamano ya wanafunzi wa elimu ya juu ili kumaliza tatizo hilo linaloathiri taaluma vyuoni.Mwakyusa alitoa wito huo jana alipokuwa akichangia Makadirio ya Matumizi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa.

“Migomo ya elimu ya juu ni hatari kwa taifa na vijana ambao ndio taifa la kesho na Serikali inatakiwa kuchukua jitihada za makusudi kuidhibiti hali hiyo”, alisema.

No comments: