Friday, July 15, 2011

Tanesco waingiza mitambo ya kufulia umeme

Elizabeth Ernest
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limeanza kuingiza mitambo yenye thamani ya Dola 120 milioni za Marekani kwa ajili ya kufulia umeme, katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Meneja Mahusiano kwa Umma katika Tanesco, Badra Masoud, mitambo hiyo itatumia gesi asilia kuzalishia umeme kwa kiwango cha megawati 100.

Alisema kwa sasa shirika lina upungufu wa megawati 250 za umeme yakiwa ni matokeo ya kupungua kwa kina cha maji katika Mabwawa ya Kidatu na Mtera.

Badra ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema tayari shirika limeshaingiza mtambo mmoja na mingine miwili itaingia wakati wowote kuanzia sasa.

Pia alisema kiwango cha mgawo wa umeme kimeongezeka kwa saa 18 badala ya 12 na kwamba hiyo inatokana na sababu za kitaalamu, zilizolilazimisha shirika kuzima mitambo ya uzalishaji.

"Wananchi wamekosa imani na Tanesco hata wanapotuona hii ni kutokana na mgawo wa umeme unaoendelea lakini tuna jitihada tunazozifanya ili kutatua tatizo hili hatujakaa kimya,"alisema.


Pia alisema, Tanesco inalazimika kukupunguza mgawo katika baadhi ya maeneo kutokana na ukame katika mabwawa.

Alisema mitambo hiyo iliyoingia ina uwezo wa kuzalisha megawati 34 na kwamba itakapofungwa pamoja na ile itakayooingizwa baadaye, itazalisha megawati 100.

Alisema inatarajiwa kuwa kazi ya kufunga mitambo hiyo, itakamilika Desemba mwaka huu.

Badra alisema mitambo hiyo itakayofungwa na Kampuni ya Jacob Sen Elektro, itasaidia kuongeza kiwango cha umeme katika gridi ya taifa na kupunguza tatizo la nishati.

Alisema, pamoja na mitambo hiyo, Tanesco pia itakodisha mitambo ya Agreco itakayoingizwa nchini Agosti mwaka huu kwa ajili ya kuzalisha megawati 100 za umme.

"Serikali inashughulikia mafuta kwa ajili ya kuzalisha mitambo ya IPTL ambayo pia itazalisha umeme wa megawati 100 kwa hiyo tatizo lililopo litakuwa limepungua kwa kiasi kikubwa au kumalizika kabisa,"alisema.

Meneja mkandarasi wa Jacob Sen Elektro, French Richard, alisema tayari wamekwishaanza kujenga maeneo ya kufunga mitambo hiyo na kwamba mitambo iliyosalia inategemewa kuletwa nchini Jumamosi.

No comments: