Friday, July 8, 2011

Sumaye: Mafisadi lazima watoswe


ASEMA CCM NI CHAMA CHA WANYONGE
Daniel Mjema, Moshi
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema tofauti ya kipato kati ya matajiri na masikini, rushwa na ufisadi vinatishia mustakabali wa amani nchini na kusisitiza kuwa mafisadi ndani ya CCM lazima watoswe.Sumaye alitoa kauli hiyo jana katika viwanja vya Soko la Pasua, mjini Moshi alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya chama cha TANU kutimiza miaka 57 tangu kuanzishwa kwake.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali CCM na Serikali, akiwamo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Meja Jenerali Mstaafu Said Kalembo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaji Mussa Samizi na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Vicky Swai.

“CCM ni chama cha wanyonge kwa maana yawafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara wanaofanya biashara halali…. Lakini kuna dalili inayoonyesha kuwa CCM sasa kimeanza kutekwa na wachache wenye uwezo wa kifedha,” alisema Sumaye.

Katika hotuba hiyo iliyovuta hisia za wananchi na wanachama wa CCM waliohudhuria mkutano huo, Sumaye alisema japokuwa mambo hayo yanauma, lakini ni lazima WanaCCM waelezane kuhusu mwelekeo wa chama chao.

“Mwelekeo huu ni hatari kwa chama chetu na kwa mustakabali wa taifa letu…,tusijidanganye ni lazima tujue kuwa Watanzania wengi wanaitegemea CCM, hivyo lazima ikae katika msingi unaoeleweka… Hatuwapigi vita wala kuwachukia matajiri ila ila wasikiteke nyara chama,”alisisitiza Sumaye.

Jambo lingine alilosema ni hatari kwa mustakabali wa nchi, ni mgawanyo mbaya wa utajiri akisema katika nchi yoyote duniani, lazima watakuwepo matajiri na masikini, lakini tatizo ni pale kundi dogo linapohodhi utajiri wa nchi husika.

“Tatizo hapa ni kundi la watu wachache wanapotaka kuhodhi utajiri wa nchi… Hali hiyo si salama kwa matajiri na si salama kwa masikini na wala si salama kwa nchi nzima,” alisema sumaye huku akishangiliwa na wana CCM na wananchi wengine.

Aliongeza kusema”wale wasionacho kama ikitokea na dalili hiyo imeanza kujitokeza katika nchi yetu …wale masikini watapigana na wale walionacho bila kujali kama ulichonacho ulikipata kwa halali ama la”.

Sumaye aliwataka Watanzania kutofikia huko na kudokeza TANU ililisimamia vizuri jambo hilo na CCM ni lazima nayo ilisimamie akisema taifa ni lazima lijenge mfumo utaohakikisha utajiri hauwi kwa watu wachache kwani hiyo ni hatari kwa amani.

Kuhusu suala la rushwa ambalo limekuwa likipigiwa keleke nchi nzima, Sumaye alisema tatizo hilo limeanza kuota mizizi nchini na kwamba, kama Watanzania hawatakuwa na ujasiri wa kuikata basi utaiua CCM na nchi.

“Tutaua chama chetu na hata nchi yetu….ni lazima tuwe na ujasiri wa kukata mizizi ya rushwa….tusiposimama kidete huduma za jamii zitakuwa zinapatikana katika kundi la watu wachache wenye uwezo wa kifedha,”alisema Sumaye.

Sumaye alisema Ufisadi ni mbaya zaidi kuliko wizi akisema tatizo hilo lipo nchini na linaonekana kukua kwa kasi na kushika mizizi kwa nguvu.

Hata hivyo alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kile alichosema ni ujasiri wake wa kulikemea suala hilo kwa nguvu zote za kutoa maelekezo kwa CCM kujivua gamba akisema “kama Rais wa nchi amefikia mahali akalisemea basi tatizo ni kubwa”.

“Marehemu mzee Rashid Mfaume Kawawa Mungu amrehemu aliwahi kutuambia kama mnasafiri katika mtumbwi mmoja na mnamuona mwenzenu anaanza kuutoboa mtumbwi basi mtoseni yeye baharini vinginevyo wote mtazama,”alisema.

Sumaye alifafanua kuwa Mtumbwi wa CCM ndio umebeba Watanzania wote hivyo ni azima uwe salama na kwamba CCM haitakubali mtu au kundi la watu kuutoboa mtumbwi huo ili watanzania wote wazame na kusisitiza lazima mtu huyo atoswe.

Kauli hiyo ya Sumaye ilionekana kuunga mkono tamko la Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) lililowataka wanachama wa chama hicho wanaotuhumiwa kwa ufisadi wakiwemo Wabunge, kujiuzulu wenyewe vinginevyo CCM itawawajibisha.

Lakini mbali na tamko hilo, lakini kauli ya Sumaye ambaye anaonekana kuwa na nguvu ndani ya CCM imekuja wakati kuna sakata la ufisadi katika ununuzi wa rada ambapo Mwanasheria mkuu wa serikali wa zamani, Andrew Chenge anatajwa.

Vyombo vya habari jana vilimkariri katibu Mkuu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Dk. Wilbroad Slaa na Waziri kivuli wa sheria na mambo ya katiba, Tundu Lissu wakisisitiza upo ushahidi wa kumtia hatiani Chenge.

Chenge mwenyewe mara zote amekanusha tuhuma hizo na jana alikaririwa akiwataka wenye ushahidi kuuwasilisha Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa(TAKUKURU) huku akisema uchunguzi wa tuhuma hizo ulishafungwa.

No comments: