Friday, July 15, 2011

Sita wafa maji, wawili walipuliwa kwa bomu

Joyce Joliga, Songea
WATU wanane wamekufa katika matukio mawili tofauti yaliyotokea mkoani Ruvuma, wakiwamo sita waliokufa maji katika Ziwa Nyasa na wawili waliolipukiwa na bomu.Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa wakati watu hao sita walifariki , wengine sita walinusurika kifo baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Nyasa wilayani Mbinga, kutokana na ziwa hilo kuchafuka kutokana na upepo mkali.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamuhanda alisema jana kuwa boti hiyo iliondoka katika bandari ndogo ya Mbamba Bay tangu Julai 11 ikiwa na abiria 12, ikielekea Malawi.

Akifafanua zaidi Kamanda Kamuhanda alisema, ikiwa katikati ya ziwa ilizama na kusababisha watu sita kufa papo hapo na wengine sita kuokolewa baada ya kuogelea kwa umbali mrefu kwa kutumia madumu ya mafuta waliyokuwa nayo katika boti hiyo.Kwa mujibu wa Kamanda Kamuhanda, waliokufa ni Mussa Moses, Daniel Wilson, Kimanda Charahani, Vincent Kambona, Kassim Matembo pamoja na mwingine mmoja ambaye jina lake hadi sasa halijatambulika.

Aliwataja waliookolewa kuwa ni pamoja na Titus Mwakasegye (32), Anna Kalima (35), John Kamanga (36), John Komba (36), Davis Mapunda (33) na Michael Rombola (37), ambao wote wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Mbamba Bay na hali zao zinaendelea vizuri.

Katika tukio hilo, kamanda alisema boti hiyo, mali ya Frank Sumuni, raia wa Tanzania, ilikumbwa na madhara hayo ambapo baada ya muda mrefu kupita bila mawasiliano, wafanyakazi wa bandari walitoa taarifa polisi na ndipo juhudi za kuanza kuwatafuta zilianza na kufanikiwakuwaokoa watu hao sita.

Baada ya uokoaji huo, Kamanda Kamuhanda alisema watu hao walikimbizwa katika kituo cha afya cha Mbamba Bay kupatiwa matibabu na kuongeza kwamba, Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Kufuatia tukio hilo, kamnada huyo aliwashauri wamiliki wa vyombo vya usafiri majini kuacha kubeba mzigo mkubwa kuliko uwezo wao ikiwa ni pamoja na kuweka vifaa vya uokoaji katika boti zao ili pindi kunapotokea matatizo watu wapate vyombo vya kujiokolea.

Hii ni mara ya pili kwa wiki hii kutokea kwa ajali katika Ziwa Nyasa ambapo juzi raia watatu wa Somalia walikufa maji katika ziwa hilo na kufanya idadi ya watu waliokufa maji kwa wiki hii kufikia tisa na wengine 84 kunusurika kutokana na vyombo vyao vya usafiri kuzama wakiwa safarini kwenda Malawi.

Katika hatua nyingine, wakazi wa Wilaya ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma wamepatwa na hofu baada ya wananchi wawili kufariki dunia baada ya kulipuliwa na bomu na vichwa vyao kupasuliwa vipande vipande na viungo vyao kutupwa ovyo baada ya bomu waliloliokota kichakani kwa lengo la kuchomea matofali kulipuka ghafla na kusababisha vifo.

Tukio hilo lilitokea jana katika Kijiji cha Mpitimbi B ambako watu hao ambao wanadaiwa ni mafundi wa kufyatua matofali walipokuwa wakiendelea na shuguli zao katika moja ya vichaka vya kijiji hicho.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kamanda Kamuhanda aliwataja watu waliokufa kuwa ni Alfred Luambano (23), mkazi wa kijiji hicho pamoja na rafiki yake ambaye anajulikana kwa jina la Bonge au Chinga (25), mkazi wa Tunduru ambaye alifika kijijini hapo kwa lengo la kufanya kibarua cha ufyatuaji na uchomaji wa matofali.

Kamanda huyo alisema, "Siku ya tukio Luambano (marehemu), alikwenda kichakani kujisaidia ambapo aliokota kitu kinachodhaniwa kuwa bomu na wakawa wakichezea yeye na mwenzake na ndipo ghafla kilipolipuka.
Akifafanua, alisema bomu hilo lilipasuka na kumlipua kichwani , kusambaratisha miguu na mikono ambako vipande vingine viliruka na kumpasua kichwa huku Bonge naye akifariki papo hapo.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya wananchi kusikia mlipuko huo walianza kukimbia na baadaye walifanikiwa kukuta miili ya marehemu hao ikiwa imeharibiwa vibaya na kitu hicho ambacho kinasadikiwa kuachwa na wapiganaji wa waasi wa Msumbiji wa Renamo wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini mwao.Aliwatahadharisha watu kuacha kuchezea vitu wasivyovifahamu na badala yake watoe taarifa kwa vyombo husika, ikiwamo polisi pindi wakatakapobaini uwapo wake.

Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wametoa maoni yao ambapo wameiomba Serikali kutuma timu ya wataalam wa mabomu toka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) au Polisi kufanya uchunguzi katika eneo hilo ili kuweza kuchunguza kama bado kuna mabaki ya mabomu ili yaweze kuangamizwa ili kupunguza hofu kwa wananchi ambao maeneo wanayoishi yalikuwa yakihifadhiwa mabomu hayo.

Kwa upande wake, Wilbert Mahundi alisema amesikitishwa na tukio hilo na aliiomba Serikali isaidie kupeleka mbwa wa kunusa mabomu katika maeneo ya Mpitimbi na Muhukuru ili wasaidie kuyatafuta ili yasiendelee kuwaathiri wananchi na kuwasababishia kuishi kwa woga.

No comments: