Friday, July 8, 2011

Hivi Wassira amekuwa mufilisi wa hoja?


KATIKA toleo la jana la gazeti hili, tulichapisha habari zilizomnukuu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia masuala ya mahusiano na uratibu, Stephen Wassira akilishambulia vikali gazeti hili kwa kuchapisha picha yake gazetini wiki mbili zilizopita akiwa amechapa usingizi bungeni. Alilituhumu kwa kile alichokiita kuandika habari za uchochezi na kwamba lina asili ya nje, hivyo pengine lingependa nchi ikumbwe na vurugu kama ilivyo katika baadhi ya nchi.

Waziri Wassira ambaye alikuwa akifanya majumuisho ya matumizi ya Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu aliongeza: …”tunamwambia umechelewa, hapa hayawezekani”. Wakati anapigwa picha hiyo akiwa anauchapa usingizi, waziri huyo alikuwa anakaimu nafasi ya Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni.

Pamoja na kukiri kuwa alikuwa ameuchapa usingizi wakati Bunge lilikuwa linaendelea, alikiita kitendo cha gazeti hili kuchapisha picha iliyomuonyesha akiwa usingizini kwamba kilikuwa cha uchochezi. Alisema siku hiyo alikuja bungeni akiwa mgonjwa na dawa aliyopewa katika Zahanati ya Bunge ndiyo iliyomuweka katika hali hiyo ya kusinzia.

Lakini waziri huyo alikwenda mbali zaidi na kunukuu vichwa vya habari ambazo gazeti hili lilikuwa limechapisha huko nyuma, akisema zilikuwa za uchochezi. Moja ya habari hizo ilihusu sakata la posho za vikao kwa watumishi wa umma iliyosema kwamba Chadema ilikuwa imeibwaga Serikali. Habari nyingine ni ile iliyomnukuu Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akisema bungeni kwamba Serikali iliyo madarakani ilikuwa inaogopa kufanya maamuzi.

Tumeorodhesha mlolongo wa tuhuma zilizotolewa na waziri huyo dhidi ya gazeti hili siyo kwa kutaka kuonewa huruma, bali kuwapa fursa wasomaji wetu na wananchi kwa jumla ya kuamua kama kweli gazeti hili linastahili lawama na laana zinazoelekezwa kwake na Waziri Wassira. Rekodi yetu katika muongo mmoja wa kuwapo gazeti hili imeonyesha kuwa, tumekuwa tayari kukosolewa na mara zote tumeomba radhi pale tunapofanya makosa.

Lakini tunapata wasiwasi pale waziri wa serikali anapoweza kupata ujasiri wa kutoa shutuma na tuhuma za uongo dhidi ya gazeti ambalo hata viongozi wa juu wa chama chake cha CCM wanakiri kwamba linaandika ukweli. Kwamba sisi ni wachochezi na gazeti hili lina asili ya nje, hivyo pengine lingependa nchi itumbukie katika vurugu kama ilivyo katika baadhi ya nchi ni tuhuma nzito zinazoweza tu kutolewa na mtu asiyewatakia wenzake mema.

Pamoja na kwamba dhima kubwa ya gazeti hili ni kuwafahamisha na kuwahamasisha wananchi, ukweli ni kwamba gazeti pia linafanya biashara na lishindana kibiashara katika soko ili lipate faida. Ili tuweze kufanikiwa kufanya biashara tunahitaji mazingira mazuri yenye amani, mshikamano na utulivu. Tuhuma za Waziri Wassira kwamba gazeti linataka nchi ikumbwe na vurugu hakika ni kichekesho cha karne.

Pengine tuchukue fursa hii kuwafahamisha wananchi kwamba, tuhuma hizi za waziri huyo ni mwendelezo wa mchezo mchafu wa baadhi ya washindani wetu katika sekta ya umma wenye kusimamia dhana yenye matege kwamba, kwa kuwa wamiliki wa gazeti hili ni wawekezaji kutoka nje, basi waandishi wake hawana uzalendo kwa sababu ajenda wanazotekeleza zinaamuliwa na watu wa nje.

Lakini lazima tuseme tukiwa tunatembea vifua mbele kwamba, waandishi wa habari na wahariri wa Mwananchi na gazeti dada la The Citizen, wanaongozwa na Sera ya Uhariri inayozingatia weledi na inayowapa uhuru kamili wa kuendesha magazeti hayo pasipo kuingiliwa na mtu yeyote. Wasomaji wetu pengine watashangaa kujua kwamba, kati ya wafanyakazi 132 wanaofanya kazi katika magazeti hayo, ni wafanyakazi watatu tu tena wasio na nafasi za kufanya maamuzi ya uhariri ndio wanatoka nje ya nchi.

Tungependa kuwahakikishia wasomaji wetu na wananchi kwa jumla kwamba, hatutarudi nyuma katika kusimamia ukweli na tutafanya hivyo bila woga wala upendeleo. Kwa upande wa wabunge wanaochapa usingizi bungeni, tunawapa tahadhari kuwa tutawachongea kwa wapigakura wao ili siku ikifika wafanye maamuzi magumu.

No comments: