Friday, July 8, 2011

'Serikali haitaingia gharama kutafiti mafuta,gesi'


Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema Serikali ya Tanzania haitaingia gharama zozote wakati meli ya Poisedon, itakapokuwa inafanya uchunguzi wa mafuta na gesi katika pwani ya Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Pinda alitoa kauli hiyo jana baada ya kutembelea eneo la viwanda vya kujenga meli ili kuona hatua mbalimbali za ujenzi wa meli na kuikagua meli ya uchimbaji mafuta.

Meli hiyo ya Poisedon inajengwa katika Bandari ya Geoje, Kusini Mashariki mwa Seoul, Korea Kusini.

Waziri Mkuu anatarajiwa kuizindua meli hiyo leo saa 4 asubuhi katika Bandari ya Geoje.

Alisema wanachofanya sasa wataalamu kutoka Kampuni ya Petrobas ya Brazil ni kutafiti na kubainisha maeneo mawili ambako meli hiyo itachimba endapo matokeo yatakuwa mazuri.


"Tunaishukuru Serikali ya Brazil kwa kuamua kuisadia Serikali ya Tanzania kufanya utafiti huo muhimu," alisema Waziri Mkuu Pinda.

Alisema hatua hiyo ni dalili njema kuwa uwekezaji unawezekana kufanyika Tanzania na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania itafanya kila iwezalo, kuweka ulinzi wakati wataalamu hao wakiwa kazini ili kuzuia hatari ya kupambana na maharamia.

Mapema, akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu kuhusu ujenzi wa meli hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Petrobas Tanzania, Samuel Miranda, alisema wanatarajia kwamba meli hiyo itafanya kazi katika ukanda wa pwani kwa muda wa miezi 20 katika maeneo ya kati ya Mafia na Mtwara.

Kuhusu uendelezaji wa miundombinu, Miranda alisema hadi sasa wameshawekeza kiasi cha dola za Marekani milioni 11 na ifikapo Desemba mwaka huu watatoa Dola za Marekani milioni 14 ili kuendeleza Bandari ya Mtwara.

Kuhusu utoaji ajira kwa Watanzania, alisema wameanza kutoa mafunzo kwa vijana 50 wa kike na wa kiume wa kutoka Mtwara ambao wakifaulu, watafanya kazi katika meli hiyo.

"Meli hii itakuwa Mtwara na tunatarajia kuanza kazi mwanzoni mwa Septemba. Tumeanza na vijana 50 kuanzia Julai mosi, watapewa mafunzo maalumU ya miezi mitatu ya umeme, umakenika na masuala ya uchimbaji mafuta na si kitu kingine," alifafanua.

"Mafunzo haya yanaendeshwa kwa ubia baina ya TPDC, Veta, Petrobas na Taasisi ya Cenal ya Brazili ambayo inafanana na Veta ya hapa Tanzania, nia yetu ni kupata wakufunzi ambao wataendelea kufundisha vijana wengi zaidi katika fani hii,"alisema.

Mbali na hatua hiyo, Miranda alisema wana mkataba na wahandisi wanne wa Kitanzania ambao tayari wamepelekwa Brazil kwa mafunzo ya muda mfupi na kisha watapelekwa Uingereza ili kujifunza zaidi masuala ya uchimbaji mafuta.

Meneja Mradi wa Kampuni ya Ocean Rig ya Uingereza inayosimamia ujenzi wa meli hiyo, David Gray, alimweleza Waziri Mkuu kwamba kwamba meli hiyo yenye urefu wa mita 242 na upana wa mita 52, imegharimu Dola za Marekani milioni 800.
SOURCE:Mwananchi

No comments: