Friday, February 4, 2011

Siri ya Bitchuka kutoka Mlimani Park kwenda Safari Sound

Juma Kasesa
AHALAN wasahlan mpenzi msomaji wa Jamvi la Kulonga ikiwa ni Ijumaa nyingine tunapokutana Jamvini katika kujadili na kuchambua hili na lile yaliyojiri na yanayotarajiwa kutokea katika tasnia ya sanaa na burudani.

Katika Jamvi letu la leo ningependa kumzungumzia nguli mwingine wa muziki wa dansi ambaye ni mtunzi na mwimbaji wa bendi ya Mlimani Park Orchestra zamani ikijulikana DDC Mlimani Park Sikinde ‘Ngoma ya Ukae’ naye si mwingine ni Hassan Rehani Bitchuka.

Kubwa ambalo Jamvi hili limepanga kukudadavulia kuhusu Bitchuka ni sababu ipi ilimfanya yeye na kundi la wanamuziki wenzake kuchukua uamuzi wa kuitosa DDC Mlimani Sikinde Ngoma ya Ukae na kwenda kuiasisi bendi ya Orchestra Safari Sound ‘Wanandekule’.

Huyu ni mwanamuziki ambaye alizaliwa katika Kijiji Kagunga kilichopo pembezoni mwa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma na kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya muziki wa dansi Tanzania hakujatokea mwanamuziki aliyevunja rekodi yake ya kuimba sauti kali licha ya uwepo wa kina wa hayati Suleimani Mbwembwe, Nico Zengekala na wengineo.

Mchango wake ni mkubwa katika medani ya muziki wa dansi kutokana na kutunga nyimbo nyingi zenye kuelimisha na kuburudisha jamii, akiwa ameng’ara katika kila bendi ambayo amewahi kupitia.

Jamvi la Kulonga linapenda kukufahamisha kuwa nguli huyu wa muziki wa dansi alisoma katika Shule ya Msingi Kipampa Ujiji, mkoani Kigoma na kuishia darasa la sita kutokana na kujikita zaidi katika uhuni wa utotoni.

Uwezo wa sauti yake kali ya kuimba na yenye kuleta hisia kwa msikilizaji ni kipaji alichojaaliwa na Mungu kikiongezewa na mafunzo ya madrasa ambako alikuwa msomaji mzuri wa Kurani na kughani kaswida hali ambayo ndiyo chachu ya mafanikio ya kuwa na sauti kali hadi leo.

Bitchuka ambaye katika familia yao yeye ndiye mwanamuziki pekee alianza shughuli za muziki mwaka 1972 katika bendi ya Nationality iliyokuwa ikifanya maonyesho yake mkoani Arusha kabla ya bendi ya Jumuiya ya Wazazi Tanzanaia JUWATA Jazz kuja jijini humo na kumuona akiwa na bendi na kuvutiwa naye.

Jamvi hili linakujuza kuwa nguli huyu alijiunga na Juwata mwaka 1973 baada ya kufanyiwa majaribio ‘Ikiwa kama Hunitaki’ na kuimba sauti kali iliyowasisimua wakongwe aliowakuta katika bendi hiyo Joseph Lusungu, Abel Baltazar, Kiza Husein, Ahmed Omary, Mabruk Khalfan, Saidi Mabera, Juma Kitambi na Muhidin Maalim Gurumo.

Baada ya kufuzu majaribio ya kuimba nyimbo yake ya kwanza kutunga ilikuwa ni ‘Msondo wa NUTA’ ambako pia aliweza kutunga na kuimba nyimbo kadhaa ambazo ni ‘Mpenzi Zarina’ ambalo ni jina la mkewe, ‘Dada Rehema’, ‘Dada Asha’ akishirikiana na wakongwe hao.

Kutokana na maudhi aliyokuwa akiyapata kutoka ndani ya bendi hiyo mwaka 1980 aliamua kujitoa na kwenda kuiasisi DDC Mlimani Park ambako alishirikiana na Abel Baltazar, Joseph Mulenga, Michael Enock ‘King Michael’ na wengineo ambako wimbo wake wa kwanza kutunga ulikuwa ni ‘Duniani Kuna Mambo’, ‘Wafanyakazi’ na ‘Mume wangu Jerry’.

Jamvi la Kulonga linakujuza kuwa nyimbo hizo zilimng’arisha Bitchuka na kupata mafanikio katika medani ya muziki huo ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambako hadi leo nyimbo zake zinaendelea kupigwa kabla ya kutunga wimbo ‘Nawashukuru Wazazi Wangu’ ambao ulimuongezea umaarufu zaidi.

Baada ya kukudadavulia kwa kifupi historia fupi ya nguli huyo turudi katika hoja ya Jamvi letu la leo ambayo nataka kukudadavulia kwanini Bitchuka licha kupata mafanikio akiwa na bendi hiyo aliamua kujitoa 1990 akiwa na wenzake na kwenda kuasisi Orchestra Safari Sound.

Aliamua kujitoa Mlimani Park akiwa na Abel Baltazar, Muhidin Maalim Gurumo, Charles Ngosha, Kassim Rashid ‘Kizunga’, ‘Ally Makunguru’ baada ya kiongozi mmoja wa bendi hiyo aliyekuwa akisimamia suala la nidhamu marehemu Mpoto kuwatusi kuwa kama wameshindwa kuimba na kutunga atawafukuza kazi, kauli ambayo iliwaudhi wanamuziki hao wakiongozwa na Bitchuka.

Jamvi la Kulonga linakujuza wakati huo Bitchuka alikuwa akilipwa mshahara wa shilingi 90,000 lakini kibaya zaidi Mpoto alitishia kushusha mishahara yao kwakile ilichoelezwa ni kubana matumizi ya bendi, hali ambayo ilimfanya yeye na wenzake kufanya uamuzi wa kwenda kuasisi Safari Sound na wimbo wake wa kwanza kutunga ulikuwa ni ‘Chatu Mkali’ akafuatia na ‘Shukrani kwa Mjomba’, ‘Pole Kaka Mudi’ na ‘Wajifanya Wajua’.

Nyimbo hizo zilimpandisha chati zaidi kiasi cha DDC Mlimani Park kuamua kumshawishi kurejea kundini mwaka 1992 ambako alirejea na kutunga na kuimba nyingi zenye mafunzo na kuburudisha kwa jamii kabla ya viongozi wa JUWATA kumchukua tena mwaka 1994 hadi mwaka 2003 alipoamua kurudi Mlimani Park ambako yupo hadi sasa akiwa na kina Shabani Dede, Abdalah Hemba, Joseph Bernad na wengineo.

Huyu ndiye Hassan Bitchuka ambaye ni shabiki wa kutupwa wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Wekundu wa Msimbazi (Simba) ambaye Jamvi la Kulonga lilitaka kukujuza nini hasa kilimfanya kujitoa Sikinde na wenzake na kwenda kuiasisi Orchestra Safari Sound.

Kwa leo nalikunja Jamvi hadi Ijumaa ijayo nikikutakia wikendi njema tukutane Jamvini kama ilivyo ada yetu.


Tuwasiliane kwa barua pepe:

jkasesa@hotmail.com, simu 0715-629298

No comments: