Friday, February 4, 2011

DAWASCO yashambuliwa kwa ufisadi Ubungo

na Ambrose Jimmy




WAKAZI wa jimbo la Ubungo na wadau mbalimbali wa maji nchini wamesema ufisadi katika Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) na serikali kupuuza malalamiko ya wananchi ndivyo vinavyokwamisha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Wakazi hao walitoa hitimisho hilo baada ya kujadili kwa kina tatizo la maji katika jimbo la Ubungo kupitia kongamano lililoitishwa na mbunge wa jimbo hilo, John Mnyika, hivi karibuni.

Kwa mujibu wa wajumbe wengi waliohudhuria kongamano hilo, vioski vya kuuza maji huchangia kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa maji kwa madai kuwa ni biashara ya vigogo wa mamlaka hiyo hasa katika maeneo ya Mbezi, Kimara, Ubungo, Msigani, Saranga, Goba na Manzese.

Wajumbe wa kongamano hilo walisisitiza kwamba vigogo hao wa DAWASCO hukata maji kwa muda wa wiki tatu ili wayauze wakisingizia uchakavu wa miundo mbinu. Pia ilielezwa katika kongamano hilo kwamba magari mengi ya kuuzia maji ni ya vigogo wa mamlaka hiyo au watu walio karibu nao.

“Ufisadi hata kwenye maji ya kunywa?! Ule upendo wa Watanzania wa zamani umeenda wapi?!” alisema mama mmoja huku akiungwa mkono kwa kushangiliwa na wajumbe wengine.

Hata hivyo, hakufika mwakilishi yeyote kutoka DAWASCO licha ya mamlaka hiyo kupewa wito na mbunge huyo takriban wiki tatu kabla.

No comments: