Friday, February 4, 2011

Mengi amenivunjia heshima - Manji

na Happiness Katabazi
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Yusuf Manji (35), jana aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa kashfa zilizotolewa na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi kuwa yeye ni Fisadi Papa zimemvunjia heshima na kupoteza uaminifu wake mbele ya wabunge.

Aidha Hakimu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, anayesikiliza kesi hiyo inayovuta hisia za wengi nchini, Aloyce Katemana, alikubali kupokea vielelezo vya hati ya barua ya mwaliko wa Kamati ya Bunge zisizo halisi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Manji alitoa nyaraka nane zisizo halisi (Original) ambazo ni mialiko ya shughuli za kiserikali ya ndani na nje ya nchi zilizodai kumtaka awe mgeni rasmi na kutoa hotuba mbalimbali za masuala ya kiuchumi.

Pia alitoa magazeti ya This Day na Kulikoni pamoja na DVD, ambavyo vyote vilipokelewa na mahakama kufanya jumla ya vielelezo vilivyopokelewa kufikia tisa.

Manji ambaye jana ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupanda kizimbani hapo, alitoa maelezo hayo wakati akitoa ushahidi wake juu ya kesi hiyo.

Mfanyabiashara alikuwa akitoa ushahidi wake huku akiongozwa na jopo la mawakili maarufu wa kujitegemea nchini: Mabere Marando, Dk. Ringo Tenga, Richard Rweyongeza, Sam Mapande na Beatus Malima.

Manji ambaye anadai alipwe fidia ya sh moja kwa madai ya kukashfiwa na Mengi, aliwasili mahakamani na msafara wa magari mbalimbali likiwemo gari aina ya fuso lilobeba lundo la magazeti ambayo yanadaiwa kuchapisha habari iliyomnukuu Mengi akimkashifu ambayo yaliwasilishwa mahakamani hapo kama kielelezo.

Katika ushahidi wake, Manji alidai Aprili 23-27 mwaka 2009, Mengi kwa kutumia kituo cha televisheni cha ITV, alitoa madai kuwa Manji na wafanyabiashara wengine kuwa ni mafisadi papa, wanahamisha rasilimali za taifa kupeleka nje ya nchi na kwamba wameshiriki kikamilifu katika ufisadi wa ununuzi wa magari ya JWTZ, rada, mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma, mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSPF na NSSF, Dowans na Richmond.

Kwa mujibu wa Manji, Mengi alidai zabuni hizo walizipata kwa rushwa na fedha walizonazo zimetokana na ufisadi.

Mkanda wa kipindi hicho maalum, ulionyeshwa mahakamani hapo kama kielelezo cha ushahidi.

“Mheshimiwa hakimu kupitia matamshi hayo ya mdaiwa (Mengi) kwenye kipindi hicho maalum, kwa kweli, kimenivunjia heshima ndani ya familia yangu, wafanyakazi wangu zaidi ya 4,000, wafanyabiashara wenzangu wa ndani na nje ya nchi na jamii iliniona kama mtu mchafu na wabunge wamepoteza imani na mimi kwa ajili ya matamshi hayo.

“Na kuthibitisha kuwa wabunge hawana imani na mimi hasa wabunge waliokuwa wabunge wa Bunge lilopita….Kamati ya Uchumi ya Bunge, ilinialika kwenye moja ya kikao chao nikatoe hotuba lakini cha ajabu nilivyofika kwenye kikao hicho, kuna baadhi ya wabunge wa kamati hiyo walinikataza kutoa hotuba yangu kwa sababu ni mtu mchafu kwenye jamii na Mengi alikwishanitaja hadharani kuwa mimi ni Fisadi Papa, nililazimika kuondoka kwenye mkutano huo na kurejea nyumbani kwa aibu,” alisema Manji.

Aliendelea, “Kashfa zilizoelekezwa na mdaiwa kwangu, si za kweli kabisa kwani sijawahi kujihusisha na biashara za rada, Dowans, Richmond, ununuzi wa magari ya jeshi, kuhamisha fedha nchini kuzipeleka nje ya nchi na wala sijawahi kushtakiwa kwa kutoa rushwa ili nipate tenda za serikali na hadi nina umri huu sijawahi kutoa fedha zangu mfukoni kujenga nyumba hata moja hapa nchini wala nje ya nchi…hapa jijini naishi kwenye nyumba ya familia pale Upanga na Marekani kuna nyumba ya familia aliyoiacha marehemu baba yangu Meibou Manji,” alidai Manji.

Wakili Marando alipomhoji Manji anatafsri vipi neno Fisadi Papa aliloitwa na Mengi; Manji alijibu kuwa analitafsiri kwamba yeye ni mtu anayekabiliwa na skendo na kwamba papa ni aina ya samaki mkubwa aishie baharini na kukana kwamba yeye siyo samaki aina ya papa bali ni binadamu.

Hakimu Katemana aliahirisha usikilizaji wa kesi hiyo hadi leo asubuhi ambapo Manji ataendelea kutoa ushahidi wake na baadaye kuhojiwa na mawakili wa Mengi.

Mapema mwaka juzi, Manji alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa alitumia televisheni yake kumkashfu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na mmoja wa watu wanaopora rasilimali za taifa.

No comments: