Friday, February 4, 2011

Kagasheki agawa Katiba jimboni kwake

na Asha Bani, Bukoba
MBUNGE wa Bukoba mjini Balozi Khamis Kagasheki (CCM), amewataka wananchi kuisoma na kuijua Katiba ya zamani ili utakapofika wakati wa mabadiliko wajue wanachotakiwa kufanya.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba jana baada ya kukabidhi nakala 50 za Katiba kwa Meya wa mji huu, mbunge huyo alisema hiyo ni moja ya ahadi zake kwa wananchi wakati wa kampeni.

Balozi Kagasheki aliahidi kugawa nakala 100 za Katiba na kwamba ameanza kutimiza ahadi hiyo ili wapigakura wa Bukoba mjini waisome na kuifahamu vema Katiba hiyo kabla ya kuifanyia mabadiliko.

“Ukweli ni kwamba watu wengi hawaitambui hata hii Katiba iliyopo ndiyo maana nimewaleteeni muisome kabla ya kudai mabadiliko ili mchakato wa kukusanya maoni utakapoanza mjue pa kuanzia wapi.

“Mabadiliko ya Katiba kwa sasa hayaepukiki… iwe kwa upya au kufanyiwa marekebisho lakini ni lazima kuwepo na mabadiliko katika Katiba ili kukidhi haja za wananchi wengi,” alisisitiza mbunge huyo ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani.

Naye Meya wa jiji hilo Dk. Anatory Amani alisema kwa kuanza atagawa nakala za Katiba hiyo kwa madiwani wote bila kujali itikadi za vyama na zilizosalia zitapelekwa kwa wenyeviti wa serikali za mtaa.

No comments: