Friday, February 4, 2011

Chiligati apata wakati mgumu Maswa

na Samwel Mwanga, Maswa
HALI si shwari ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu, baada ya viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho wilayani humo kutakiwa kuachia ngazi kutokana na kuendeleza migogoro ya mara kwa mara na kukidhoofisha.

Hayo yamejitokeza juzi katika kikao cha Kamati ya Siasa ya wilaya hiyo kilichohudhuriwa pia na viongozi wa ngazi za juu wa Mkoa wa Shinyanga chini ya Katibu Mwenezi wa CCM Taifa, Kapteni John Chiligati, kilichofanyika katika ukumbi ofisi za chama hicho, mjini Maswa.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao, zilisema kuwa Chiligati ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Shinyanga, alitaka kufahamu kilichosababisha wakakosa viti vya ubunge katika majimbo ya Maswa Mashariki na Maswa Magharibi katika uchaguzi mkuu uliopita.

Ndipo aliposimama Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Maswa, Jeremiah Shigalla na kueleza kwamba kulikuwa na usaliti uliofanywa na baadhi ya watendaji wa chama hicho na wanachama kwa kukiunga mkono Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hususan Katibu wa UWT wilayani humo, Nuru Mselemo na hivyo kupendekeza atimuliwe.

Pia waliendelea kumtupia lawama Mselemo kuwa ndiye anaendeleza migogoro ndani ya chama hicho ambaye anatuhumiwa kuchakachua jina la Pili Lameck, katika nafasi ya udiwani wa viti maalum ambaye alishindwa kupata nafasi hiyo licha ya kuongoza kwa kupata kura nyingi katika mkutano mkuu wa UWT wilayani humo.

Wakati tuhuma hizo zikielekezwa kwa Katibu huyo wa UWT baadhi ya wajumbe walipinga maelezo hayo akiwemo Katibu wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Bakari Mbonde, ambaye alieleza wazi kuwa migogoro ndani ya chama hicho wilayani humo, inasababishwa na Mwenyekiti wa CCM, Peter Bunyongoli, pamoja na Katibu Mwenezi, Jeremiah Shigala, hivyo kupendekeza waondolewe.

“Baada ya kumtuhumu kwa muda mrefu Mselemu, wajumbe wengine tulikataa kwani tunajua chanzo cha wananchi na wanachama kukichukia chama chetu ni hawa viongozi wawili wa wilaya ambao ni Mwenyekiti, Bunyongoli na Katibu Mwenezi, Shigala,” alisema mzee Bonde.

Walisema viongozi hao wamekigeuza chama kama kikundi cha watu binafsi, jambo ambalo limezua mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hata kushindwa kufanya kazi na makatibu wa CCM wanaoletwa wilayani humo.

Hata hivyo Chiligati alipata wakati mgumu kujibu sababu hizo, lakini aliahidi kwamba angeyachukua mapendekezo hayo na kuyafikisha katika ngazi ya taifa.

Katika hatua nyingine, Chiligati alishindwa kuhutubia mkutano wa hadhara uliondaliwa na chama hicho katika viwanja wa MADECO kutokana na wananchi kutohudhuria mkutano huo.

Chiligati ambaye alipaswa kuhutubia mkutano huo majira ya saa 10:00 jioni kulingana na matangazo yaliyokuwa yakitolewa kupitia vipaza sauti kwenye gari lililozunguka mitaa yote ya mji wa Maswa, hakuna watu waliojitokeza kuhudhuria.

Ilipofika majira ya saa 11.56 jioni ambapo mwandishi wa habari hizi alikuwepo katika viwanja hivyo, kulikuwa na watu wanne tu wakiwa eneo la mkutano, huku wakilalamika kutokuwa na taarifa ya mkutano huo..

Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja alipotafutwa kuzungumzia kitendo cha Chiligati kutofika eneo la mkutano alisema kuwa walipata taarifa ya misiba mitatu, hivyo watu hawakuweza kuhudhuria, ndiyo maana waliahirisha.

No comments: