Friday, February 4, 2011

Simba yaipumulia Yanga

na Mwandishi wetu
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba jana waliiadhibu African Lyon kwa mabao 3-0 katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, jana.

Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 30 ndani ya michezo 13 hivyo kuipumulia Yanga ambayo iko kileleni kwa pointi 31 na mchezo mmoja mbele.

Simba waliouanza mchezo huo kwa kasi ya aina yake, walifanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya tano lililofungwa na Amri Kiemba kutokana na kona ya Haruna Shamte.

Kabla ya bao hilo, kipa wa African Lyon Noel Lucas aliumia katika harakati za kuokoa hatari langoni mwake, hali ambayo ilifanya mchezo huo kusimama kwa dakika 15.

Simba waliendelea kufanya mashambulizi langoni mwa Lyon, ambako dakika ya 18 Mussa Mgosi alipiga shuti karibu na lango la Lyon lakini mpira ulipaa.

Lyon ilijibu mapigo dakika ya 29, baada ya shuti la Mohamed Samata kupaa juu ya lango la Simba.

Katika dakika ya 39, Rashid Gumbo alipiga shuti kali langoni mwa Lyon, lakini kipa Lucas alipangua na kuwa kona.

Hadi mwamuzi wa mchezo huo, Oden Mbaga, anapuliza filimbi ya mapumziko, Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili, Simba walirejea uwanjani kwa nguvu na kufanikiwa kufunga bao la pili dakika ya 46 na mfungaji akiwa Mbwana Samata aliyeambaa na mpira kutoka katikati ya uwanja na kufumua shuti kali lililojaa wavuni.

Baada ya bao hilo, Simba waliendelea kulisakama lango la Lyon ambapo wapinzani wao kila walipojaribu kusaka namna ya kuliona lango la wana Msimbazi mabeki wa timu hiyo walikuwa makini.

Samata alifunga bao la tatu katika dakika ya 82 baada ya kazi nzuri ya Haruna Shamte.

Katika dakika ya 83, mshambuliaji wa Simba Ahmed Shiboli alipiga shuti kali karibu na lango la Lyon baada ya pasi safi ya Mohamed Banka, lakini likapaa juu ya lango.

Dakika ya 85, Mohamed Banka alikosa bao la wazi baada ya kazi nzuri ya Juma Jabu aliyeambaa na mpira kutoka upande wa kaskazini mwa uwanja wa Uhuru. Hivyo hadi mwisho wa mchezo Simba iliibuka kidedea kwa mabao 3-0.

Simba iliwakilishwa na Ally Mustafa, Haruna Shamte, Juma Jabu, Meshack Abel, Kelvin Abel, Jerry Santo, Rashid Gumbo/Aziz Gilla, Patrick Ochan, Mussa Mgosi/Ahmed Shiboli, Mbwana Samata na Amri Kiemba/Mohamed Banka.

African Lyon iliwakilishwa na Noel Lucas, Rajab Zahir/Stephano Nkomola, Hamis Shengo/Haji Dudu, Zubery Ubwa, Bakari Omar, Hamis Yusuf, Hamis Thabit/Samuel Ngassa, Mohamed Samata, Adam Kingwande, Idrissa Rashid na Sunday Bakari.


Mwisho

No comments: