Monday, January 24, 2011

CCM sasa balaa

• Makundi ya chuki, fitina yaibuka upya

na Waandishi wetu




HALI ya mambo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) si shwari na huenda makada wake wakajiengua au kufukuzwa ndani ya chama hicho, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.

Hatua hiyo inatokana na kuibuka upya kwa makundi yanayohasimiana ambayo sasa yanadaiwa kufikia hatua mbaya zaidi kuliko ilivyowahi kutokea huko nyuma.

Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa makundi hayo hivi sasa yanashutumiana kwa kuendesha kampeni za chini kwa chini kuhakikisha baadhi ya watu wanapoteza madaraka yako ndani ya chama na serikalini.

Miongoni mwa watu wanaoonekana kuwa katika wakati mgumu ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ambao wameonekana kukosoa hadharani uamuzi wa wizara nyingine.

Sitta na Mwakyembe walipinga hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kutangaza kuwa serikali itailipa Kampuni ya Dowans sh bilioni 94 baada ya kushinda kesi waliyoifungua dhidi ya Shirika la Umeme (TANESCO).

Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ulimtaka Rais Jakaya Kikwete achukue maamuzi magumu ya kuwashughulikia makada wa CCM wanaokiyumbisha chama na serikali kiasi cha kuifanya ikose imani kwa wananchi.

Hata hivyo kikao cha Kamati Kuu ya CCM (CC) kilichoketi juzi kiliweka bayana kuwa hatima ya Sitta na Mwakyembe ipo serikalini na Rais Jakaya Kikwete ndiye atakayejua mustakabali wa viongozi hao waliojizolea umaarufu kwa kupinga ufisadi.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, jana alijitosa kutuliza upepo mbaya ulioanza kuvuma ndani ya chama hicho, kwa kuwaonya wabunge wake kuacha malumbano na serikali.

Ingawa hakuwataja makada wanaolumbana hadharani, lakini mazingira yanaonyesha anawalenga Sitta na Mwakyembe, ambao wameweka wazi msimamo wao juu ya kulipwa fidia kwa Kampuni ya Dowans.

Kauli hiyo ya Pinda, inachukuliwa ni kuwafunga kufuli Sitta, Mwakyembe na makada wengine wa chama hicho walio mstari wa mbele kupinga malipo hayo.

Onyo hilo alilitoa jana kwenye ufunguzi wa semina ya wabunge wa CCM, iliyofanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam, ambapo alisema malumbano yanayoendelea kujitokeza miongoni mwa wabunge wa CCM si ishara nzuri kwa wananchi dhidi ya serikali yao.

Pinda alisema kuwa umefika wakati kwa wabunge hao kutoa maoni yao ya wazi bila jazba, hasa wakati wa mijadala ya kitaifa ili kujiepusha na kauli zinazoweza kulivuruga taifa.

“Chama chetu na serikali haiwezi kuwa imara kama wabunge hamtakuwa makini na kauli mnazozitoa kwa umma,” alisema Pinda.

Pinda alisema Bunge la tisa lilitawaliwa zaidi na wapinzani kwa sababu wabunge wa CCM hawakuitumia nafasi hiyo.

Aliongeza kuwa wapinzani walionekana kwa wananchi kuwa ndio wenye uchungu na masilahi ya taifa kuliko wa CCM, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa lilikiangusha chama tawala.

“Tumieni vizuri kipindi cha maswali ya papo kwa hapo, kwa Waziri Mkuu, lakini Bunge lililopita wapinzani walifanikiwa kutumia nafasi hiyo na wananchi wakapima uwezo wao…kumbukeni kuhudhuria vikao vya wabunge wote ili kujua msimamo wa pamoja kuhusu utendaji wa serikali,” alisema.

Pinda alisema kuwa wabunge na mawaziri wanapaswa kuhudhuria vikao vya Bunge na kuchangia hoja kwa kuzingatia kanuni za Bunge.

Alibainisha kuwa kipimo sahihi na uwezo wa mbunge ni uchangiaji wa mijadala ya kitaifa na wananchi hupima uwezo huo na kwa chama kilichompa fursa ya kuchaguliwa na wananchi katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Pinda alisema kukosa umoja miongoni mwao ni hatua ya kukifanya chama pamoja na serikali kuonekana havifanyi kazi ipasavyo kama ilivyokusudiwa na wananchi.

Alisema vitendo vya kuchangia mijadala kwa jazba bila kujali misingi ya umoja na mshikamano ni hatari kwa chama.

Pinda, alisema ni lazima wabunge wote wa CCM wawe kitu kimoja na kutambua kuwa chama hicho ndicho kinachoongoza dola.

Alisema madhumuni ya semina hiyo ni kuwafanya wabunge hao wa CCM kutambua wajibu wao hasa wanapokuwa ndani na nje ya Bunge.

Aliongeza kuwa leo Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuhudhuria semina hiyo na kusikiliza mijadala ya wabunge pamoja na mada ya wajibu wa wabunge wa CCM katika mfumo wa vyama vingi, ambayo itawasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa.

Awali akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua semina hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Mkuchika, alisema wabunge wa CCM hawana sababu ya kuwa wanyonge kwa sababu chama chao ndicho kinachoshikilia dola.

Alisema umoja ni muhimu kuimarishwa ndani ya chama na kuwataka kujipanga sawasawa katika Bunge, ili kulifanya liwe rahisi kwa uchangiaji wao wa mijadala itakayowasilishwa au kuibuka.

“Umoja ndani ya chama ni muhimu tuuimarishe na tunatakiwa kujipanga hadi ndani ya Bunge na kuchangia mijadala itakayowasilishwa ili kulinda na kutetea masilahi ya wananchi wote wa Tanzania,” alisema Mkuchika.

Alisema mbunge ni haki yake kusema lakini ni muhimu kukumbuka kuna mahali pengine hapaswi kuropoka na kuwataka kutambua umuhimu wa kuendelea kuilinda na kuihami CCM.

Semina hiyo ya siku tatu ambayo itafikia tamati kesho, imehudhuriwa na wabunge wote 260 wa Chama Cha Mpinduzi (CCM).

Mkoani Dodoma, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, ametakiwa kujitafakari upya na ikiwezekana aachie ngazi ili awapishe wengine waongoze.

Kauli hiyo imetolewa na mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, kutoka mkoani Mara, Anthony Mtaka, wakati wa kikao cha viongozi vijana wa chama hicho.

Alisema umefika wakati kwa Makamba na viongozi wenzake wa sekretarieti ya chama hicho kutafakari wanavyomsaidia Rais Jakaya Kikwete.

“Nawataka makada wa CCM akiwamo Makamba waeleze wamemsaidiaje rais katika utendaji wao wa kazi za chama na wajikosoe na kama haitoshi wajitoe,” alisema.

Mtaka alisema viongozi hao wakijikosoa na kubaini upungufu wao wanaweza kumshukuru Rais Kikwete kwa kuwapa nyadhifa hizo na kumwambia wanajitoa kwa sababu ya kushindwa kuwajibika ipasavyo.

Alisema kwa kufanya hivyo watakuwa wamemsaidia sana rais katika kurahisha utendaji wake wa kazi, kwani ndani ya chama kuna Wana CCM wengi wanaoweza kushika nyadhifa hizo.

Naye Mwenyekiti wa wenyeviti wote (UVCCM) taifa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa umoja huo mkoani Mbeya, Fadhili Ngairo, amesema ndani ya CCM kuna maadui wakubwa watatu.

Alisema adui wa kwanza yumo ndani ya chama hicho na ambao wameingia kwa kadi na masilahi yao binafsi na si kwa moyo, ambao wanafanya kazi ya kukihujumu chama na wamejipanga kugombea urais mwaka 2015.

Alisema maadui wa pili wako nje ya chama, ambao ni wanaharakati na wapinzani, wao wamekuwa wakifanya kazi ya kuchochea na kuendeleza maandamano kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi.

Alibainisha kuwa maadui wa tatu wako nje ya nchi, ambao amewaita kuwa ni mabeberu wanaofanya kazi ya kuingia na kuvuruga nchi.

Alisema mabeberu hawa wanawatumia Wana CCM ambao ni viongozi ndani ya chama kuvuruga nchi kwa njia ya fedha na kutoa misaada mbalimbali ambayo inawanufaisha wao na wajanja wachache.

No comments: