Monday, January 24, 2011

CCM, udini na kisa cha mfalme na nyuki

Prudence Karugendo




RIWAYA ni habari ya kufikirika iliyo katika tungo za kubuni, lakini mara nyingi riwaya hueleza visa vilivyo sawa na matukio ya kweli katika jamii za wanadamu. Kisa kimojawapo katika riwaya ni cha mfalme na nyuki.

Mfalme mmoja aliyependa kutukuzwa sana na watu wake bila yeye kuutumia utukufu wake kuwafanyia watu wake mambo yaliyolingana na utukufu waliokuwa wanampatia.

Ilifikia wakati akajiangamiza mwenyewe kwa ulevi wake uliosababishwa na tabia yake ya kupenda utukufu kupita kiasi na kutaka abaki yeye tu aliyetukuka milele yote.

Kilitokea kipindi himaya ya mfalme huyo ikakumbwa na matatizo yatokanayo na nguvu za asili, ukame na njaa, watu wakaanza kufa kwa njaa, utukufu wake ukaanza kupungua na kuelekea kupotea kabisa.

Lakini badala ya mfalme yule kufanya jitihada za kuwatafutia watu wake chakula yeye akawa anahangaika kuwatafuta wachawi waliosababisha hali ile kutokea, imani yake ilikuwa kwamba ile ni hali iliyosababishwa na wabaya wake ili atolewe kwenye kiti cha enzi.

Kwahiyo jitihada zikaanza, siyo za kuwatafutia watu wake chakula, bali za kuidhibiti hali ile ambayo kwake ilikuwa kama uasi wa makusudi, iliyoanza kujitokeza ikichochewa na hatari ya watu kufa kwa njaa.

Akiwa anajitahidi kuurudisha juu utukufu wake ulioanza kuporomoka kwa kasi. Kwake madaraka na utukufu vilikuwa muhimu kuliko uhai wa watu aliowatawala.

Ndipo mfalme akapata ushauri kutoka kwa wapambe wake na kuukubali, akashauriwa itafutwe mizinga ya nyuki kwa wingi kadiri ilivyowezekana ili ikazungushwe katika himaya nzima.

Alikubaliana na wapambe wake kuwa wakati ukifika mizinga ile ikafunguliwe na nyuki waanze kuwashambulia watu, hususan wabaya wa mfalme, waliokuwa wakiaminika kwamba ndio waliokuwa wanachochea uasi dhidi ya utukufu wake.

Mawazo ya mfalme yule mlevi wa utukufu yalikuwa kwamba kwa nguvu za utukufu wake angeweza kuwaamrisha nyuki kwa kuwaambia acha nao wakatii amri.

Matokeo yake nyuki walipofunguliwa wakaanza mara moja kuwashambulia kwa hasira wapambe wa mfalme na kuwaangamiza wote, baada ya hapo nyuki wakabisha hodi Ikulu kwa mfalme na kumuangamiza naye.

Hawakumgusa mtu mwingine yeyote kwenye himaya ile. Kwa ujinga na ulevi wa madaraka aliokuwa nao mfalme wao, watu wa himaya ile wakawa wamepata ukombozi.

Hiyo ni riwaya, lakini hata hivyo kisa kizima tunaweza kukifananisha na yanayotokea nchini mwetu kwa sasa. Chama tawala, CCM, baada ya kubanwa na upinzani kila upande.

Upinzani ambao kwa muda mrefu kilikuwa hakikuuzoea, kwa kuwa ni chama ambacho hakikutokana na ushindani wa kisiasa, sasa kimeanza kufanya viroja!

Mfano tuliyaona yaliyotokea kwenye kampeni za uchaguzi ulioisha. Baada ya CCM kupelekwa mchakamchaka kwa kasi ambayo chama hicho hakikuizoea wala kuitarajia, mara tukasikia linatoka tamko la ajabu ambalo ni la kwanza tangu tupate uhuru.

Tamko hilo ni lile la vyombo vya ulinzi na usalama kuingilia mchakato wa kisiasa. Vyombo hivyo vikatoa vitisho kwa kadri vilivyoweza bila kuweka bayana kiini cha vitisho hivyo, huku CCM ikiwa nyuma ikitetea kila kitu.

Ni mwendawazimu peke yake anayeweza kuamini kuwa zile ni juhudi binafsi za vyombo vile bila maelekezo kutoka kwingine.

Uchaguzi ukafanyika katika mazingira ya uchakachuaji wa kutisha, mshindi akatangazwa kwa mabavu kuwa ni CCM. Baada ya hapo CCM ikatulia ikiamini kwamba kazi imekwisha, ikiwa imesahau kwamba mwisho wa harakati moja ni mwanzo wa harakati inayofuata.

Chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, kwa uerevu wa historia walio nao makada wake kwamba Roma haikujengwa kwa siku moja, kikaendelea kuwasha moto kikiwa kimeiteka nchi nzima kiasi ambacho tunaweza kusema kwa kimombo kwamba “CHADEMA is now reigning though not ruling”, (CHADEMA inaongoza hata kama haitawali).

Hilo limeichanganya CCM na hivyo chama hicho kuamua kubuni njia mpya za kukabiliana na upinzani wa CHADEMA.

Ikumbukwe kwamba CCM ni chama kilicho na mbinu kongwe za kuukandamiza upinzani, iwe ndani ya chama chenyewe au nje yake. Kama nilivyosema hiki ni chama ambacho hakikuzoea upinzani.

Niseme hakiujui upinzani kwa vile hakikutokana na ushindani wa kisiasa. Hakizijui siasa za ushindani. Ni sawa na mtoto aliyelelewa kwa deko.

Ndiyo maana chama hicho kimeona mbinu inayokifaa kwa sasa ni ile mbinu chafu ambayo kimekuwa kikiitumia muda wote kuwanyoosha wanachama wake kiliowaona kuwa wanakisumbua, tena usumbufu wenyewe ukiwa ni wa kukitaka chama kuzingatia maadili yake.

Mbinu ambayo imekuwa ikitumiwa na CCM ni ya kuwapachika sifa mbaya waadilifu hao, si mwenzetu huyo, na baabaye kuwavua uraia! Na kwa vile wengi wa makada wanaokifanya chama hicho kikatoka kwenye misingi yake ya maadili ni wale walio wazito katika kujenga hoja zinazoeleweka na kushawishi, kinachowawia chepesi ni fitina za fulani na fulani wavuliwe uraia.

Ndipo tukashuhudia makada kadhaa wa chama hicho wakivuliwa uraia katika mazingira ya ajabu ajabu, lakini lengo kuu likiwa ni la kuwanyamazisha waadilifu hao wachache.

Lakini kwa vile mbinu hiyo ya kuwavua uraia wale wanaotokea kuukumbatia uadilifu haiwezi kutumika kwa chama kizima cha siasa kinachotanguliza uadilifu kama mwongozo wake kisiasa, kama vile kusema makada wote, wanachama na wapenzi wa CHADEMA, kwa mfano, wavuliwe uraia, ndipo zikatengenezwa mbinu mbadala za ukabila na udini.

Mfano tuliona NCCR- Mageuzi mwaka 1995 kikidaiwa kwamba ni chama cha kikabila, cha Wachaga, ingawa ukweli ni kwamba chama hicho muasisi wake ni Mjaluo kutoka mkoa wa Mara.

Baadaye kikafuata Chama cha CUF, tukaelezwa ni chama cha kidini, cha Kiislamu na cha kikabila, cha Wapemba, wakati ukweli ni kwamba muasisi wa chama kile ni Mkristo na Mnyamwezi wa Tabora.

Cha ajabu sasa hivi chama hicho kilichodaiwa ni cha kidini kimefunga ndoa rasmi na chama tawala kule Visiwani na ndoa tunayoweza kuiita ya mkeka huku Bara, ili kuendesha serikali pamoja bila CCM kutueleza ule udini wa mwenzake huyo umeishia wapi!

Hizo zote ni propaganda chafu za kisiasa ambazo pasipo kuziendea kwa umakini zinaweza kumfanya mtu asahau hata jinsia yake. Mfano zinaweza kuanzishwa propaganda kwamba wanawake wamezidi kudai hiki na kile.

Kila wakati wanadai, kumbe katika madai hayo yamo pia yanayowagusa wanaume, lakini kwa vile propaganda zimewalenga wanawake, inaweza ikatokea hata wanaume wanaoguswa na madai hayo wakajiona nao ni wanawake!

Sasa hivi Chama Cha Mapinduzi kimeanzisha propaganda maalumu kwa ajili ya kukabiliana na nguvu za CHADEMA. Naweza kusema kwamba propaganda hizi ni za kijinga kwa sababu mbali na kuwa chafu pia ni hatari hata kwa CCM yenyewe.

Ni kwamba eti Chama cha Demokrasia na Maendeleo kina ajenda ya udini! Sielewi ni udini gani unaosemwa ndani ya CHADEMA, sijui ni Uislamu au Ukristo. Watoa hoja hawafafanui vizuri.

Nikiangalia naona chama hicho kimesheheni watu wa dini zote, na kwa vile CCM wanaelewa kuwa wanachokisema ni uongo inawawia vigumu kututamkia kuwa udini unaosemwa ni huu. Hiyo inabaki ni mikakati ya “Divide and rule”.

Lakini hata hivyo propaganda hizi ni chafu na hatari, sawa na ushauri wa kuleta nyuki ili wawaangamize wabaya wa mfalme, zinalenga kuifanya CHADEMA ionekane ina udini, sana sana Ukristo, ingawa Ukristo pekee ni vigumu kuuita udini kutokana na kugawanyika katika madhehebu mbalimbali mengi.

CCM hawajatamka ni udini gani isipokuwa tunasoma tu sura zao, ingawa baadaye wanaweza wakageuka kwa vile wana kauli zinazokwenda na upepo kwa maana ya kauli zao kutokuwa na mizizi ya ukweli.

Hebu tuangalie orodha hii ya wabunge wa CHADEMA halafu tuutafakari udini wa chama hicho: Sabrina Mlasi, Zitto Kabwe, Said Arfi, Maulida Kommu, Abubakary Akonaay, Mariam Msabaha, Chiku Abwao, Raya Suleiman, Mwanamrisho Abama, na Muhonga Said Ruhanywa.

Hao ni baadhi ya wabunge wa CHADEMA kutoka katika madhehebu ya Kiislamu, waliobaki ndio wanaotoka katika madhehebu mengine zaidi ya 100. Hivyo udini uko wapi na ni upi?

Tofauti na ilivyo katika CCM kwa mfano, ambako Mwenyekiti wa chama ni Mwislamu, tena akafanya chini juu kuhakikisha Mkristo aliyekuwa Katibu Mkuu anaondoka kwenye nafasi hiyo na yeye kumteua Mwislamu mwenzake kushika nafasi hiyo. CHADEMA Mwenyekiti ni Mlutheri na Katibu Mkuu ni Mkatoliki.

Hawa ni watu wa madhehebu mawili tofauti, kama ni kusali kila mmoja anakwenda kwenye nyumba ya ibada iliyo tofauti na ya mwenzake, kinyume na Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa CCM wanaosali kwenye nyumba moja ya ibada, msikitini.

Itakuwa ni ujinga kuuangalia udini katika CHADEMA, chama ambacho tabaka lake la juu linaonyesha mchanganyiko wa madhehebu na kuacha kuutazama udini katika chama ambacho tabaka lake la juu linajihakikisha ni la madhehebu ya aina moja tu.

Lakini hata hivyo hilo la udini katika CHADEMA limeibuliwa baada ya kukiona chama hicho kimeanza kunguruma nchi nzima. Mwanzoni tuliambiwa kuwa ni chama cha kikabila, Wachagga, kwa vile muasisi wake anatoka katika kabila hilo.

Lakini CCM hakijawahi kuitwa chama cha Wazanaki kutokana na Baba wa Taifa, muasisi wake, kutoka katika kabila hilo na ukweli ni kwamba bado mpaka sasa wapo makada wengi wa chama hicho wanaotoka katika kabila hilo dogo.

Tukirudi nyuma, wakati Rais Kikwete alipopendekezwa kwa mara ya kwanza na chama chake kuwa mgombea urais, viongozi wa dini mbalimbali, kwa kujua au kutokujua walichokuwa wakikifanya, waliitisha kongamano la kumuunga mkono katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam.

Lengo lilikuwa kuwakatisha tamaa wagombea urais wengine kwa madai ya kwamba Kikwete lilikuwa ni chaguo la Mungu. Je, hawa mafundi wa kuangalia udini walikuwa wapi wakati huo?

Ilikuwaje wasione udini ulivyokipamba Chama Cha Mapinduzi na kukiwezesha kupata kilichoitwa ushindi wa kimbunga?

Maaskofu walioona kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu mwaka 1995 sasa hivi wanaona vingine, maana hata Mwenyezi Mungu aliumba malaika wengine wakageuka mashetani.

Mauaji ya Arusha, maaskofu wamelaani, wasingekosa kufanya hivyo kwa vile eti walishatamka kwamba Kikwete ni chaguo la Mungu.

Inawezekana hapo ndipo CCM inapouona udini! Lakini katika mauaji hayo ya kinyama mtu wa kwanza kupigwa risasi alikuwa ni Mwislamu. Kwa hiyo CCM watueleze, maaskofu wanaingia hata misikitini siku hizi? Watueleze huo udini umekaaje ambapo maaskofu wamemkataa meya bandia ambaye ni Mkatoliki wakidai hawatamtambua kama hakuchaguliwa kihalali?

Kada mmoja wa CCM amenikabili akionyesha mimi nisivyofahamu kitu, anataka anishawishi nikubali kuwa mauaji ya Arusha ni matakatifu hivyo nisiyafananishe na yale ya Sharperville wala Soweto, Afrika Kusini, wakati aina ya mauaji ni ileile moja.

Hoja yake ni kwamba kule Afrika Kusini walikuwa ni Wazungu wanawaua weusi, lakini mweusi kumuua mweusi mwenzake eti haina neno!

Nimalizie kwa maoni yangu kwamba, CCM walichopaswa kukifanya ni kukabiliana na changamoto za upinzani wala siyo kukabiliana na upinzani wenyewe kama wanavyofanya sasa.

Vinginevyo kwa hili la udini ni lazima waelewe kwamba wanatengeneza mizinga ya nyuki ambayo si ajabu wakawaangamiza wao na huo kuwa ukombozi wa nchi yetu.


prudencekarugendo@yahoo.com

No comments: