Monday, January 24, 2011

Slaa airushia UVCCM kombora

• Asema yupo tayari kupimwa akili nzuri

na Mwandishi wetu




KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa, amesema yupo tayari kupimwa akili nzuri alizonazo za kupambana na wanaotafuna rasilimali za taifa.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili juzi, Dk. Slaa alisema kuwa yeyote mwenye kutetea rasilimali za taifa zisitafunwe na walafi wachache waliopo ndani ya Chama Cha Mapinduzi hawezi kuwa na matatizo ya akili.

Kauli hiyo aliitoa baada ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kuitaka serikali imkamate kiongozi huyo na kumpeleka katika hospitali kumpima akili.

Katibu Mkuu wa UVCCM (taifa), Martin Shigela, alisema wameamua kutoa kauli hiyo baada ya kujiridhisha kuwa kiongozi huyo wa upinzani hakutakiwa kukataa matokeo ya urais kwa kudai kura zake zimechakachuliwa (kuibwa).

Aliongeza kuwa Dk. Slaa ni miongoni mwa vinara waliochangia kuhamasisha vijana wafanye maandamo yaliyopigwa marufuku na Jeshi la Polisi mkoani Arusha, ambako vijana watatu walifariki dunia na zaidi ya 20 kujeruhiwa.

Umoja huo ulisema Dk. Slaa amekuwa akitoa kauli mbalimbali za kichochezi ili kuwafanya wananchi wasiiamini na kuipenda serikali ya CCM chini ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

Akijibu mashambulizi hayo ya UVCCM, Dk. Slaa amesema yuko tayari kupimwa akili zake nzuri alizonazo kutokana na kuwa mstari wa mbele kuibua hoja nzito dhidi ya serikali.

“Unakwenda kunipima akili kwa kitu gani? Mimi naona nipimwe kwa akili nzuri, maana siku zote nimekuwa nikisimama kidete kutetea rasilimali za nchi, likiwamo suala la Dowans kutolipwa.

Sasa kati ya mimi, Shigela na vijana wenzake wa CCM, nani akapimwe akili zisizofaa?” alihoji Dk. Slaa.

Alisema umaarufu wa mtu na umakini wake unatokana na ujengaji wa hoja na anavyozitetea pamoja uungwaji mkono wa jamii, hivyo haoni sababu kwa watu wa aina hiyo wapimwe akili.

Aidha, mkoani Mwanza, Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, (CHADEMA), amemtaka Rais Jakaya Kikwete, asome alama za nyakati, ili asije kuitumbukiza nchi katika migogoro na machafuko ya umwagaji wa damu kama ilivyotokea nchini Zimbabwe, Kenya na Ivory Coast.

Alimtaka Rais Kikwete kuwaongoza Watanzania kwa misingi mizuri na kufuata matakwa ya Katiba ya nchi, vinginevyo atasababisha kutoweka kwa amani na upendo ulioachwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo juzi jimboni humo wakati akiwahutubia mamia ya watu katika mikutano miwili tofauti ya hadhara ya kuwashukuru wananchi kwa kumpigia kura na kumwezesha kuwa mbunge.

Highness alisema dalili zinavyoonekana hivi sasa zinaashiria serikali kushindwa kuwaongoza vema Watanzania, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi. “Namtumia salamu Rais Kikwete ahakikishe analiongoza taifa letu kwa kufuata Katiba ya nchi, asije akalizamisha kwenye machafuko kama yaliyotokea Kenya, Zimbabwe...hatutaki kuona wananchi wetu wanapigwa mabomu na kuuawa na polisi,” alisema.

Highness alitumia fursa hiyo kulaani mauaji yaliyotekelezwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha, Januari 5, mwaka huu wakati wakiwazuia wanachama na viongozi wa CHADEMA kufanya maandamano ya amani.

Alisema ni heri serikali ikajikita zaidi katika uboreshaji wa maendeleo ya wananchi, ikiwa ni pamoja na kutatua kero na matatizo mengi yanayolikabili taifa.

Aliongeza kuwa ni vema Rais Kikwete akalionya Jeshi la Polisi liache kufanya kazi kwa misingi ya kisiasa kama inavyoonekana sasa.

Highness aliwahakikishia wananchi wa Jimbo la Ilemela kuwa ahadi zote alizoahidi atazitekeleza, ikiwa ni pamoja na kujenga kituo cha polisi Kata ya Bugogwa-Igombe, kuboresha sekta ya elimu, barabara, maji na afya.

Katika mikutano aliyoifanya Highness, wananchi walimtaka mbunge wao huyo kuhakikisha anaporudi bungeni asimame kidete kupinga dhamira ya serikali ya kutaka kuilipa Kampuni ya Dowans sh bilioni 94.

Wananchi hao wamemtaka mbunge huyo asimamie suala hilo ili fedha hizo zielekezwe kupeleka maendeleo kwa wananchi na zisaidie kupunguza umaskini.

No comments: