Monday, January 24, 2011

Mengi awatahadharisha viongozi wa dini

• Walemavu nao walilia Katiba mpya

na Mwandishi wetu
MWENYEKITI Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, amewataka viongozi wa dini nchini kuacha kuhubiri kwa kutoa maneno ambayo yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Mengi alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika hafla ya chakula cha mchana na watu wenye ulemavu.

“Ninawaomba viongozi wa dini zote nchini kutohubiri kwa kutoa maneno ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kuwa chanzo cha kuhatarisha amani na utulivu wa nchi,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema pindi kunapotokea uvunjifu wa amani kundi la walemavu huwa la kwanza kuathirika.

Alisema amani na utulivu uliopo nchini unatakiwa kuwa endelevu ili nchi iendelee kusifiwa ndani na nje.

Aliongeza kwamba walemavu wanaweza kupata fursa sawa na kundi lingine la jamii endapo suala la amani na utulivu litazidi kushamiri nchini.

“Kwa niaba ya kundi hili na wengine wote nchini, ninatoa rai ya kuwataka kudumishwa kwa amani na utulivu nchini,” alisema Mengi.

Awali, Mwakilishi wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Lupi Naswanya, alisema wanahitaji Katiba mpya kwa maslahi ya taifa na jamii hiyo kwa ujumla.

Lupi alisema serikali haina budi kuwashirikisha katika mchakato wa kuandaa Katiba mpya kama moja ya jamii ya Watanzania.

“Tunahitaji kushirikishwa katika mchakato wa kuandaa Katiba mpya, Katiba iliyopo inahitaji mabadiliko makubwa kutokana na kutotupa fursa sawa katika jamii,” alisema.

Aliongeza kwamba endapo Katiba itakuwa nzuri, jamii yote itaboreka, hivyo bado kunahitajika maboresho katika Katiba ya sasa,” alisema.

Mengi amekuwa na utaratibu wa kila mwaka wa kuandaa tafrija kwa ajili ya jamii ya watu wenye ulemavu na kupata nao chakula cha mchana na kubadilishana nao mawazo.

No comments: