Monday, January 24, 2011

Si muda mrefu Azam itazizima Simba, Yanga

Ojuku Abraham



TANZANIA bado iko katika ugonjwa sugu wa kuzipenda timu kongwe za Simba na Yanga. Popote walipo mashabiki wa soka, lazima watagawanyika kwa misingi ya timu hizo mbili.

Moja kati ya vitu vya kusikitisha ni kwamba wakongwe hao walioasisiwa miaka mingi iliyopita, bado wanaendesha timu zao kizamani mno.

Lakini katika miaka michache iliyopita, imeanzishwa timu ambayo mwanzo wake, watu waliona kama nguvu ya soda, Azam FC.

Azam ilianzishwa na kuanza kucheza madaraja ya chini, kila mmoja akiamini ingekuwa na mwisho muda siyo mrefu kama klabu nyingi zilizowahi kuanzishwa kwa mbwembwe.

Lakini hatimaye msimu ya 2008/9 ulishuhudia Azam ikifanikiwa kuingia Ligi Kuu na kudumu hadi sasa. Msimu uliopita ilifanikiwa kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu na hadi hivi sasa ligi hiyo ikiwa katika mzunguko wake wa pili, timu hiyo inashika nafasi kama hiyo.

Katika kuhakikisha timu hiyo inafanya mambo vizuri zaidi, imejenga uwanja wake wa kisasa ulioko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, huko Mbagala.

Kwa kuangalia mikakati inayoelezwa na viongozi wa klabu hii inayomilikiwa na familia ya mfanyabiashara mkubwa, Said Salim Bakhressa, ni wazi kuwa muda siyo mrefu ujao, klabu hii itakuwa juu ya Simba na Yanga timu zilizodumu kwa miaka mingi.

Na itakuwa juu kwa maana zote, kwani licha ya kuwa na uwezo wa kifedha wa kuweza kushindana na klabu hizo katika usajili wa wachezaji nyota, hata michakato yao juu ya makocha wa kuifundisha timu hiyo inaonyesha wazi dhamira waliyonayo.

Katika kipindi cha hivi karibuni, timu hiyo imewahi kunolewa na makocha watatu wa kigeni: Wabrazil Neider dos Santos, Itamar Amorin na sasa chini ya Mwingereza, Stewart Hall.

Moja ya kitu kitakachosaidia sana kupanda kwa haraka kwa umaarufu wa klabu hii, ni kuendelea kwa mipango mibovu, migogoro na soka la magazetini la klabu zingine, hasa Simba na Yanga.

Ukiangalia kwa mfano, katika uwanja wao ambao pia watautumia katika Ligi Kuu utakapokamilika, wanayo shule ya watoto wenye vipaji ya kwao kwa ajili ya wachezaji wao vijana.

Na timu hii imekuwa ya kudumu kwa kipindi kirefu sasa ambayo hadi sasa imeweza kuwapandisha hadi kikosi cha kwanza wachezaji wake kadhaa wakiwemo Sino Augustino, Himid Mao, Mau Ali, Tumba Swed, Ali Mkuba na Samih Nuhu.

Kitu kimoja ambacho klabu hiyo inakosa kwa sasa ni kupata nafasi kubwa katika vyombo vya habari ambavyo vyote navyo bado vimeendelea na utaratibu na fikra mgando za miaka yote kuzikumbatia Simba na Yanga.

Kama ingekuwa inaandikwa mara kwa mara, klabu hiyo ndiyo yenye wachezaji wazuri na mahiri kuliko wanaokuzwa na magazeti katika Simba na Yanga.

Na bila shaka, itakuwa ndiyo klabu inayolipa mishahara mizuri zaidi kwa wachezaji wake, tena kwa uhakika kabisa, tofauti na mishahara inayolipwa kwa fedha binafsi za watu katika Simba na Yanga.

Binafsi ninafurahishwa sana na uendeshaji wa timu hii, kuanzia benchi lake la ufundi lililojitosheleza, uongozi wake na hata wachezaji.

Na mashabiki watakaoipenda timu hii, watakuwa ni hawa hawa kutoka ndani ya Simba na Yanga, lakini waliochoshwa na madudu ya uongozi wa timu hizo zisizokuwa na dira.

Badala ya kupanga mikakati ya kuziingiza katika nyakati mpya, viongozi wake hadi leo wanagombea uhalali wa kuzungumza!

Pamoja na kuwa na uzoefu wa miaka mingi katika fitina za soka, upo uhakika wa wazi kuwa miaka si mingi ijayo, kama siyo mwakani, Azam itaanza kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa.

Ikifika huko, ni wazi kuwa zitakuwa ni fikra za klabu hiyo kuanza kuona ni kwa jinsi gani inaweza kuwa yenye mafanikio katika Afrika kama ilivyo TP Mazembe au zile timu kutoka Afrika Magharibi na Kaskazini.

Nichukue nafasi hii kuwapa moyo Azam FC, waendelee na mipango yao ya kuwa klabu ya mfano wa kuigwa katika Tanzania, licha ya kuwa haina mtaji wa mashabiki.

Itakapofanikiwa katika mipango hiyo mingine, kazi ndogo iliyobaki ili kuwapata mashabiki, ni kutandaza kandanda la kuvutia na watu wa kweli wa mpira watakuwa pamoja nao kama zamani ilivyokuwa kwa Pan African, Pamba ya Mwanza na Ushirika ya Moshi.

No comments: