Monday, January 24, 2011

Yanga wabariki Mwalusako kubwaga manyanga

• Papic, Mpangala nao kuiacha timu Shamba la Bibi leo

na Juma Kasesa
BAADA ya Kamati ya Utendaji ya Yanga jana kubariki kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako, mzimu huo utarajiwa leo kuliandama benchi la ufundi.

Habari za uhakika zilizopatikana jana jijini Dar es Salaam, zilieleza kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Mserbia Kostadin Papic na Meneja Emmanuel Mpangala nao wamedhamiria kufuata nyayo za katibu huyo.

Inadaiwa kuwa Papic na Mpangala wamekerwa na hujuma dhidi Mwalusako zilizomfanya abwage manyanga, hivyo nao wanatarajiwa kuwasilisha barua zao leo kwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyod Nchunga, baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kilichoketi jana kubariki kuachia ngazi kwa Katibu Mkuu huyo ambaye hajatimiza hata mwaka tangu akabidhiwe mikoba hiyo mwaka jana.

Mwalusako alilithibitishia gazeti hili kuhusu kuwasilisha kwake barua ya kujiuzulu, huku akigoma kufafanua sababu za kufanya hivyo na kuahidi kuzungumza na vyombo vya habari leo.

Lakini habari za uhakika kutoka kwa mmoja wa watu wa karibu na Mwalusako zilisema, uamuzi huo wa kujiuzulu umetokana na kushinikizwa na mmoja wa wadhamini wa klabu hiyo, kutokana na kitendo chake cha kumkana mwenyekiti wake Nchunga, kuwa hakushirikishwa katika barua iliyoandikwa kwenda kwa mmoja ya wadhamini wa klabu hiyo, Francis Kifukwe.

Imeelezwa, kitendo cha Mwalusako kukana kufahamu barua ya mwenyekiti wake ikimuagiza Kifukwe kutafuta wakurugenzi 10 wenye uwezo wa kutoa shilingi milioni 50 kila mmoja ili kuunda kampuni itakayokuwa ikitengeneza bidhaa za Yanga, kimemkera mdhamini huyo na kuona kuwa katibu huyo hafai kuendelea kuingoza klabu hiyo.

Barua hiyo ya Nchunga kwa Kifukwe ni kati ya sababu zilizosababisha mwishoni mwa wiki iliyopita, viongozi wa matawi ya Yanga kuitisha mkutano wa dharura kumjadili mwenyekiti huyo kwa kitendo hicho, ambacho walikiita ni ukiukwaji wa katiba uliofanywa kwa makusudi, ikiwemo suala la uteuzi wa kiholela wa Mbunge wa Temeke, Abass Mtemvu, kuwa mmoja ya wadhamini wa klabu hiyo.

Katika mkutano huo wa viongozi wa matawi, Mwalusako na mjumbe wa Kamati ya Utendaji Mohamed Binda walihudhuria kwa niaba ya uongozi ambapo alikana kulifahamu suala hilo na kwamba hakushiriki kubariki uanzishwaji wa kusaka wakurugenzi hao, hivyo kumtupia msala mwenyekiti wake, jambo lililomkera mdhamini.

Aidha chanzo hicho kimefafanua, sababu nyingine ya kujiuzulu kwa Mwalusako, ni kufahamu njama za muda mrefu za kundi moja la wanachama, kupania kumng’oa yeye na meneja wa timu hiyo Emmanuel Mpangala kutokana na kutofautiana na baadhi ya viongozi wake.

Imeelezwa, Mwalusako amesoma alama za nyakati kwani hali ya amani imeanza kutoweka ndani ya klabu hiyo, kutokana na kundi hilo la wanachama kumfanyia fujo, Mpangala mara baada ya mechi baina ya Yanga na AFC ya Arusha, mchezo uliopigwa jijini Dar es Salaam na kulazimika meneja huyo kuondoka uwanjani saa 2:00 usiku chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Chanzo hicho kilibainisha kuwa katibu huyo amechukua uamuzi huo mzito, baada ya kuona akielemewa na mzigo wa utendaji wa majukumu ya Yanga kutokana na ukata wa fedha uliotanda klabuni hapo, hivyo kulazimika kufanya kazi ya ziada kuhakikisha timu hiyo inasonga mbele katika Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

“Hivi ninavyozungumza, Yanga haina fedha za kuwagharamia waamuzi na timu ya Dedebit ya Ethiopia kwa ajili ya mechi ya Kombe la Shirikisho na huyo aliyeshinikiza ajiuzulu, amesema atatoa fedha hizo mara baada ya Mwalusako, Mpangala na Papic kuondoka, hivyo ndiyo ujue Yanga inaelekea kubaya, kwani mtu mwenye pesa akiwa hakutaki atafanya kila hila uondoke,” kilisema chanzo hicho.

Imeelezwa kuwa Kocha Papic ambaye ameishatafutiwa msaidizi wake Fred Felex Minziro ‘Majeshi’ anatarajiwa kuicha Yanga leo katika dimba la Uhuru wakati Yanga itakaposhuka dimbani kuumana na polisi Dodoma, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

No comments: