Monday, January 24, 2011

Simba wautafuta mpira kwa tochi Dar

na Makuburi Ally




MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, jana walianza mzunguko wa pili Ligi Kuu bara vibaya baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-2 mbele ya ‘Watengeneza Koni’ Azam Fc kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Simba waliuanza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kufunga bao lao la kwanza katika dakika ya tisa, mfungaji akiwa Nico Nyagawa baada ya kazi nzuri ya Mussa Mgosi.

Baada ya bao hilo, Azam nao walibadilika na kuanza kulisakama lango la Simba na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 14 kupitia kwa John Bocco baada ya kuvunja mtego wa kuotea.

Azam waliendelea kulisakama lango la Simba na kufanikiwa kufunga bao la pili katika dakika ya 24 lililowekwa wavuni na Mrisho Ngassa aliyemlamba chenga kipa Juma Kaseja na kudumu hadi mapumziko. Kipindi cha pili, Simba walirejea uwanjani wakiwa na nguvu mpya baada ya kutolewa Nyagawa na nafasi yake kuchukuliwa na Ali Ahmed Shiboli ambaye alipiga mashuti mengi langoni mwa Azam, lakini umahiri wa kipa Vladimir Niyonkuru, uliokoa jahazi.

Azam walifunga bao la tatu dakika ya 54 kupitia kwa Bocco aliyemzidi ujanja beki Juma Nyosso na kipa Kaseja na kuukwamisha mpira wavuni.

Baada ya bao hilo Azam waliendelea kulisakama lango la Simba, kwa kugonga zaidi ya pasi 20 ambazo ziliwafanya Simba ‘wausake mpira kwa tochi’, lakini kucheza huko hakukuisaidia Azam kuongeza bao.

Simba ilipata bao la pili la Simba likifungwa na Hilary Echesa dakika ya 87 akitumia vema pasi ya Mohammed Banka; bao lililowaongezea nguvu kutaka kusawazisha, lakini hadi mwamuzi Ibrahim Kidiwa Mdudu anamaliza mpira, Azam 3 Simba 2 hivyo kulipa kisasi cha kichapo cha 2-1 mzunguko wa kwanza.

Kocha Simba, Patrick Phiri, alisema kipigo hicho kimesababishwa na mawasiliano mabaya kati ya mabeki na kipa Kaseja huku Stewart Hall akisema ingawa wameshinda wapinzani wao ni wazuri.

Simba iliwakilishwa na Juma Kaseja, Haruna Shamte, Amir Maftah/Juma Jabu, Meshack Abel, Juma Nyoso, Jerry Santo, Rashid Gumbo/Mohamed Banka, Hillary Echesa, Patrick Ochan, Mussa Mgosi na Nico Nyagawa/Ally Ahmed Shiboli.

Azam iliwakilishwa na Vladimir Niyonkuru, Ibarahim Shikanda, Mutesa Patrick, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Obrahim Mwaipopo, Jamal Mnyate/Himid Mao, Salum Abubakar, John Bocco/Ssenyonjo Peter, Ramadhani Chombo na Mrisho Ngassa.

No comments: