Friday, January 14, 2011

Historia potofu ya Vita ya Majimaji

Evaristy Masuha




NI takriban miaka mitatu sasa tangu nilipotoa mfululizo wa makala yenye kuelezea ukweli wa historia ya Vita ya Majimaji.

Historia ambayo ilibeba sehemu kubwa ya ukamilifu wa taifa la Tanganyika lililopata uhuru wake mwaka 1961.

Ukweli wa kihistoria niliojaribu kuuelezea katika tukio hilo linalostahili heshima kama kielelezo cha ushujaa kwa Watanzania liliwagusa wengi, lakini kubwa zaidi ni kualikwa na kushilikishwa kwenye kamati iliyokuwa ikiandaa kumbukumbu ya maonyesho ya miaka 100 tangu vita hiyo iishe.

Sherehe zilizokuwa zifanyike huko Kilwa ambako ndiko chimbuko la vita hiyo kama nilivyojitahidi kuiandika katika usahihi wake.

Nilipokuwa katika mfululizo huo nilijaribu kuangalia baadhi ya kasoro za kihistoria ambazo aidha zilibadilishwa makusudi ili kuwapa ufahamu tofauti vizazi vipya vya Tanzania ambavyo vitashiriki historia hiyo kwa njia ya masimulizi au kwa kusoma.

Pengine makosa hayo yalitokea katika mazingira ya kawaida ya ukomo wa akili ya binadamu kadiri Mungu alivyomuwezesha, au yalikuwa ni makusudi ya viongozi wetu waliohusika kuweka kumbukumbu hiyo wakakusudia kuweka kumbukumbu isiyo sahihi kwa sababu zao binafsi.

Waswahili husema: “Safari moja huanzisha nyingine,” baada ya kuianza historia hiyo, Mengi yenye kufichua ukweli wa historia hiyo yamejitokeza na kunipa udadisi ambao nimeona ni vema nikawashirikisha wasomaji wangu katika hili.

Tathmini ilinionyesha uhitaji mkubwa sana wa kuelewa mengi yaliyofichika katika historia nyingi zinazomzunguka Mtanzania na hasa hii vita ya majimaji.

Katika mfululizo huu ambao ama kwa hakika utafichua mengi nitafurahi kama nitapokea changamoto mbalimbali za kukosoa, kurekebishana na hata taarifa zaidi nitakazokuwa sijaziambatanisha katika haya ninayoyajadili.

Pamoja na changamoto hizo, katika makala hii nakusudia kujibu maswali yafuatayo ambayo kwa hakika majibu yake ndiyo yatakayotufikisha katika ukweli wa vita hii.

Vita ya Majimaji ilianza Julai 15, 1905. Wapiganaji wa majimaji waliamini uwezo wa dawa kubadili risasi kuwa maji. Mwezi mmoja baadaye yaani Agosti 24, kiongozi wake, Kinjekitile Ngwale, alinyongwa. Je, muda huo ulitosha kumhukumu kwamba ni muongo na kwamba dawa zake hazikuwa na uwezo wa kubadili risasi kuwa maji?

Wapiganaji wa Kimatumbi waliokuwa katika mazoezi yaliyokuwa yakijulikana kama Lininda, waliingia vitani bila kibali cha kiongozi wao Kinjekitile. Je, yaweza kuwa sababu ya kushindwa?

Hoja nyingine ambayo pia nitaenda nayo hatua kwa hatua ni juu ya moja ya masharti ya kutumia dawa ya Kinjekitile ambapo mpiganaji alitakiwa asishiriki tendo la ndoa wakati wa vita. Pia asichukue chochote kutoka kwa adui aliyeshindwa.

Je, hayo masharti yalifuatwa? Na kama hayakufuatwa je, yaweza kuwa sababu ya kushindwa?

Katika utafiti wangu huu ambao naamini utaibua hoja nyingi zenye kutufikisha katika ukweli nitajaribu kuyaangalia maisha binafsi ya Kinjekitile katika Kijiji chake cha Ngalambe.

Katika hilo nitajaribu kuangalia uhalisia wa umaarufu aliokuwa amejitwalia katika ukanda huo wa kusini. Hasa uwezo wake binafsi wa kuishi na mifugo ambayo kwa mazingira ya kawaida siyo rahisi binadamu kuweza kuishi nayo. Hasa uwezo wake wa kufuga wanyama kama simba, chui, nyoka na wanyama wengine wa mwituni.

Ili kuiweka historia katika usahihi wake nitavitumia vitabu mbalimbali na hasa vile vilivyoandika historia ya awali kabisa. Kwa hapa sitaweza kukwepa kuvitumia vitabu vya Wazungu na hasa Wajerumani wenyewe kwani vitabu vingi vya historia ya awali ni vile vilivyotungwa na Wajerumani wenyewe ambao hawasiti kukiri ajabu ya Kinjekitile kuishi na wanyama hao kama Mmasai wa leo hii anavyoishi na ngombe lakini waandishi hawa wakiwa na tafsiri yao ambayo pia nitaiangalia.

Masuala kama hayo yanaweza kuambatana na fikra zingine zenye kuweza kuiweka historia katika usahihi wake pale tunapoweza kujiuliza ni kiasi gani na ni kwa vipi mwambao wa kusini mwa Tanzania hadi pwani ya Afrika Mashariki na kwingineko walihusika.

Makabila ya Wazaramo, Wangindo, Mbunga, Wapogoro, Wamatumbi, Wangoni, Wamwera na makabila yote yanayozunguka mwambao wa bahari wote waliweza kuamini fikra za mtu mmoja tu na kuingia vitani wakiamini uwezekano wa risasi kugeuza maji.

Wazee wa Kimatumbi leo hii wanaamini kungekuwa na ushindi wa wapiganaji wa Vita ya Majimaji kabla ya upepo kubadilika baada ya kukiuka baadhi ya taratibu muhimu ambazo ziliwafikisha kuanza kupoteza ushindi ulioanza kushangiliwa mapema.

Kwa kuuangalia ushindi huo nitatoa sababu za msingi ambazo ndizo pengine zilizowaweka waandishi wa historia hii ambayo ina kipindi cha miaka zaidi ya 100 kuibadili ili tuweze kuipokea kimakosa kabisa. Makosa hayo yakapokewa hivyo na kuenezwa hadi leo hii.

Lakini la mwisho kabisa tutahitaji kuchunguza vyombo mbalimbali vyenye kuthibitisha kama kweli uchawi upo au la. Naomba tuwe pamoja Alhamisi ijayo.

No comments: