Friday, January 14, 2011

Wakili: Dowans itadhohofisha nchi

• Ataja mashahidi walioiponza TANESCO ICC

na Happiness Katabazi
MMOJA wa mawakili mahiri wa kujitegemea nchini, Kennedy Fungamtama, ameiomba serikali na umma upuuze ushauri wa aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, wa kutaka serikali kukataa kuilipa fidia ya sh bilioni 94 Kampuni ya kuzalisha umeme ya Dowans, kwani ushauri huo unaweza kulidhohofisha taifa kwa kuliingiza katika matatizo makubwa.

Fungamtama aliyasema hayo juzi katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muda mfupi baada ya gazeti hili kupata taarifa kuwa wakili huyo ni miongoni mwa wanasheria walioisoma hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Kusuluhisha Migogoro ya Uwekezaji (ICC).

Mwanasheria huyo ambaye alimuelezea Sitta kuwa mtu anayejaribu kucheza na akili za Watanzania, kwa sababu ya kutojua kwao undani wa hukumu ya ICC, alisema endapo serikali itakaidi kulipa fidia hiyo ni wazi taifa linaweza kukabiliwa na madhara makubwa mawili.

Alisema moja ya madhara hayo ni kwa wafadhili kuiweka nchi kwenye orodha ya kunyimwa misaada, kwa sababu ya kutoheshimu sheria na mikataba ya kimataifa ambayo imeridhia.

Wakili huyo alisema madhara mengini ni pamoja na wawekezaji kuingiwa na hofu ya kuja kuwekeza hapa nchini na kuongeza kuwa hilo likitokea taifa ndilo litakalopata hasara na si Waziri Sitta binafsi.

Fungamtama alisema amefikia uamuzi wa kuzungumzia jambo hilo baada ya kuisoma na kujiridhisha kwamba hukumu hiyo yenye kurasa 150 ya kesi namba 15947/VRO kati ya Kampuni ya Dowans na TANESCO ilipokewa na ICC Novemba 20, mwaka 2008 na ikatolewa hukumu Novemba 15 mwaka jana.

Alisema mkataba kati ya TANESCO na Dowans ulisainiwa Juni 23, mwaka 2006 na mkataba huo unajulikana kama ‘Power Off - Take Aggreement (POA)” chini ya kifungu cha 14 (e) cha POA, na kufafanua kwamba pande zote mbili katika mkataba huo zilikubaliana kwamba uamuzi wa Mahakama ya ICC ndio utakuwa wa mwisho na utazibana pande zote mbili na hautaweza kukatiwa rufaa.

Fungamtama alisema kifungu cha 14 (f) cha POA, kinasomeka: “The parties waive any right to challenge or contest the validity or enforceability of this arbitration agreement or any arbitration proceeding or award brought in conformity with this section.”

Kwa tafsiri nyepesi, Fungamtama alisema kifungu hicho kinasema, TANESCO na Dowans katika mkataba wao walikubaliana kwa maandishi kuweka kando haki za kupinga au kuhoji mwenendo na tuzo zitakazotolewa na baraza la usuluhishi.

Alisema Waziri Sitta amenukuliwa na vyombo vya habari akitaka serikali itumie kifungu cha 16 cha Sheria ya Tanzania ya Usuluhishi Sura ya 15 kama ilivyofanyiwa marekebisho ya mwaka 2002, kwamba serikali inaweza kutumia kifungu hicho kutengua hukumu ya mahakama ile ya kimataifa.

“Ni kweli Mahakama Kuu ya Tanzania imepewa mamlaka ya kutengua maamuzi yanayotolewa na mahakama za kimataifa endapo tu itadhihirika kuwapo kwa mambo mawili yafuatayo:
Moja; msuluhishi wakati akiendesha kesi alikuwa akiegemea na kupendelea upande mmoja (arbitrator has miss - conducted himself. Pili: Mazingira ya kufikia uamuzi ule yalitawaliwa na rushwa au shauri lilifikishwa mahakamani bila kufuata taratibu za kisheria (an arbitration or award has been improperly procured).

“Hayo ndiyo mambo mawili peke yake yanayoweza kusababisha Mahakama Kuu ya hapa nchini kutengua hukumu zilizokwisha kutolewa na mahakama za kimataifa za usuluhishi na si kwa jambo jingine lolote.

“Sasa kama Sitta ana ushahidi, vigezo hivyo viwili vya kisheria katika lililokuwa shauri baina ya Dowans na TANESCO kwamba wasuluhishi wale ambao ni majaji waliipendelea Dawans, au walikura rushwa, ingekuwa ni vyema haraka apeleke ushahidi huo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili aweze kuwatuma wanasheria wake wakafungue kesi Mahakama Kuu ili iweze kutengua hukumu hiyo kupitia huo ushahidi wake kama anao na si kama anavyofanya hivi sasa kupayukapayuka kwenye vyombo vya habari,” alisema wakili huyo.

Aidha, alisema kwa mujibu wa kifungu cha 3 cha jedwali la 3 katika Sheria ya Usuluhishi ya Tanzania, Sura ya 15 ya mwaka 2002 kinasomeka hivi:
“Each contract state undertakes to ensure the execution by its authorities and in accordance with the provisions of its national laws of arbitrarily awards made in its own territory under the preceding articles”.

“Kwa tafsiri rahisi, kifungu hicho utaona tayari nchi imejifunga mikono na utekelezaji wa hukumu zinazotolewa na mahakama za kimataifa kwa sababu ni nchi yetu yenyewe imeridhia sheria na mikataba ya kimataifa.”

Alisema kwa hiyo maelezo ya Waziri Sitta ya kutaka Dowans isilipwe, ni kutaka kuishawishi serikali na umma kukaidi kutekeleza maamuzi halali chini ya sheria na mikataba ambayo serikali iliiridhia kuitii na kuitekeleza.

Aidha, alisema jambo jingine lililojitokeza wakati kesi hiyo ikiendelea baina ya Dowans na TANESCO ni TANESCO walitaka kujua wamiliki wa Dowans ni kina nani na Mahakama ya ICC iliona hoja hiyo ya TANESCO ya kutaka kumjua mmiliki haina umuhimu wowote katika mgogoro uliokuwa mbele yao na ikatupilia mbali, kwa sababu iliona hoja hiyo haina maana yoyote mbele yao.

“Kwa hiyo kwa kitendo cha Waziri Sitta kulianzisha suala hilo la kutaka kujua wamiliki wa Dowans wakati hoja hiyo tayari ilikwishatolewa uamuzi na ICC, kisheria hawezi kulianzisha tena jambo hilo la kutaka kujua wamiliki kwa njia anayoitumia ya vyombo vya habari.

“Kwa hiyo maelezo yote yanayoendelea kutolewa kuhusu hukumu hiyo ni kutaka kujinasua katika lawama wakati yeye na baadhi ya maswahiba zake enzi zile akiwa Spika wa Bunge ndio waliokuwa chanzo cha TANESCO kuvunja mkataba na Dowans, hivyo mwisho wa siku shirika hilo la umeme kujikuta likiburuzwa katika korti ya ICC.

“Na ifike mahala wananchi na vyombo vya habari na serikali itoke usingizini na ijiulize maswali yafuatayo kwamba Sitta hakuwepo kwenye usikilizwaji wa shauri hilo? Sitta hakuwa akijua kwamba TANESCO imefunguliwa kesi na Dowans katika Mahakama ya ICC?

“Kwa kuwa Sitta alikuwa mstari wa mbele kuzipiga vita Dowans na Richmond, ni wazi alikuwa akifahamu kwamba TANESCO imeburuzwa mahakamani na kama kweli Sitta ni mzalendo wa kweli na hana chuki binafsi katika hili ni kwanini hayo madai anayoyasema asingeiomba serikali imuweke kama shahidi wa upande wa TANESCO ili akatoe ushahidi anaousema kila kukicha kwenye vyombo vya habari?

“Amesubiri tayari shirika letu la umeme ambalo ndilo lilikuwa mdaiwa katika shauri hili limeshindwa kufurukuta kwenye kesi hiyo na tumetakiwa tulipe kiasi hicho kikubwa cha fidia ndiyo kila kukicha anazungumza kwenye vyombo vya habari kuhusu hukumu hiyo, tena ukitazama maoni anayoyatoa utafikiri si mtu aliyesomea sheria kabisa….naomba sana hasa serikali ipuuze ushauri wa Sitta kwani ni wazi kabisa anataka kuliingiza taifa kwenye matatizo mengine makubwa.

“Watanzania na huyo Waziri Sitta ambao hawajaisoma hukumu ile naomba niwaeleze wazi mimi nimeisoma hukumu hiyo kwa zaidi ya mara saba, kama taifa kupitia hukumu hiyo tumeshikwa pabaya, hivyo hatuwezi kukata rufaa, isipokuwa tu kama tutathibitisha sababu zile mbili nilizozitaja,” alisema wakili Fungamtama.

Aidha, Fungamtama aliviasa baadhi ya vikundi mbalimbali vya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kuacha kuzungumzia hukumu hiyo ambayo hata wengine hawajawahi kuisoma wala kuiona, kwani tayari kuna baadhi ya waandishi wa habari wamekuwa wakiandika makala kwamba wakati kesi hiyo ikiendeshwa TANESCO haijawahi kuleta shahidi hata mmoja kutoa ushahidi.

Jambo ambalo Fungamtama alisema si kweli na linalenga kuhadaa umma, kwani majibu na nakala ya hukumu hiyo ambayo anayo inaonyesha TANESCO ilipeleka mashahidi watano na walitoa ushahidi wao.

Wakili huyo aliwataja mashahidi hao kuwa ni Subira Wandiba, ambaye ni Mwanasheria wa TANESCO, ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Zabuni iliyotoa tenda kwa Dowans, Balozi Fulgence Kazaura, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Dk. Idrisa Rashid, Mhasibu Mkuu wa shirika hilo, Jamhuri Ngeline na Boniface Njombe.

No comments: