Wednesday, January 12, 2011

DOWANS kuvunja Baraza la Mawaziri

• LHCR wamuunga mkono Sitta, Wafungua kesi kuipinga Dowans.

na Nasra Abdallah na Betty Kangonga




SAKATA la malipo ya fidia kwa Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans Tanzania Ltd limechukua sura mpya baada ya kuwapo mpasuko mkubwa ndani ya serikali unaotishia kumeguka au kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri la Rais Jakaya Kikwete, Tanzania Daima Jumatano limebaini.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa siku kadhaa sasa, umebaini kuwa tangu serikali ilipoamriwa kuilipa Dowans sh bilioni 185, kumekuwa na mzozo mkali wa wazi na wa chinichini miongoni mwa mawaziri, baadhi wakiapa kwamba wako tayari kujiuzulu kuliko kuona fedha hizo zikilipwa.

Kundi la mawaziri wanaopinga kulipwa kwa fedha hizo, linaongozwa na Spika wa zamani wa Bunge, Samuel Sitta, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC).

Kwa upande wa pili, kundi la mawaziri walioridhia malipo ya fedha hizo linawajumuisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ambao kwa nyakati tofauti wamepata kunukuliwa wakisema taifa halina njia ya kukwepa faini hiyo.

Taarifa kutoka serikalini zinaeleza kuwa kundi la mawaziri wanaokubaliana na maamuzi ya ICC limekumbwa na mgawanyiko mkubwa miongoni mwao kuhusu hatua anazopaswa kuchukuliwa Sitta.

Baadhi ya watu walio ndani ya serikali waliozungumza na Tanzania Daima Jumatano wanasema wako wale wanaotaka kuona Waziri Sitta akipuuzwa huku wengine wakimtaka Rais Jakaya Kikwete amfukuze kazi kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kukiuka kwake misingi ya uwajibikaji wa pamoja.

Habari nyingine ambazo gazeti hili halijazithibitisha zinaeleza kuwa wako baadhi ya mawaziri ambao wamefikia hatua ya kutafakari uamuzi wa kuendelea kubakia ndani ya Baraza la Mawaziri iwapo suala hilo litashughulikiwa isivyo.

Tangu Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC Court), ilipotoa hukumu yake Novemba 15 dhidi ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kutaka ilipe fidia ya sh bilioni 94, Sitta amekuwa waziri wa kwanza kupinga hadharani hukumu hiyo akiitaka serikali isilipe.

Kundi la mawaziri linalounga mkono msimamo wa Sitta, linadaiwa kufanya vikao vya faradha katika siku za hivi karibuni kupanga mkakati wa kupinga ulipaji wa fedha hizo na msimamo wao wanatarajia kuuweka hadharani katika kikao cha Baraza la Mawaziri, kinachotarajiwa kufanyika wakati wowote mwezi huu, chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete.

Duru zaidi za siasa zinasema kuwa nje ya Baraza la Mawaziri suala la malipo ya Dowans, linatarajiwa kulitikisa tena Bunge, kupitia hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), na mjadala huo unaweza kusababisha baadhi ya mawaziri kuachia ngazi.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, Sitta alisema anashangazwa na hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kutangaza msimamo wa serikali kuilipa Dowans bila suala hilo kujadiliwa na kupitishwa na Baraza la Mawaziri.

“Nimekuwa wa kwanza kupinga serikali kulipa fedha hizi na anaendelea kusisitiza hatuna sababu ya kuzilipa, bado tuna nafasi kisheria ya kupinga, lakini kibaya zaidi nashangaa kusikia Waziri wa Nishati na Madini, ameutangazia umma kwamba serikali inajiandaa kuilipa Dowans. Uamuzi huo umepitia Baraza gani la Mawaziri,” alihoji Sitta.

Alisema fedha hizo ni nyingi kuilipa Dowans ambayo alisema ina mkono wa mafisadi watatu, wanaotaka kuzitumia fedha hizo kwa maslahi yao kisiasa.

Wiki iliyopita, Ngeleja alikaririwa akisema, Serikali imekubali kuilipa Dowans dola za Marekani za Kimarekani milioni 65, sawa na sh bilioni 94.

Alisema sh 185 bilioni zilizokuwa zikitajwa kwenye vyombo vya habari ndizo ambazo kampuni ya Dowans iliiomba ICC ilipwe fidia kwa TANESCO kwa kukatiza mkataba walioingia wa kufua umeme, lakini mahakama iliafiki ilipe dola 65 milioni za Marekani.

Alisema fedha hizo zitalipwa baada ya pande husika kusajili uamuzi huo katika Mahakama Kuu.

“Serikali tumekwishaamua kuwa tutailipa Dowans dola za Marekani 65 milioni, kama ilivyoamuliwa na ICC ambazo ni sawa na sh 94 bilioni, kuchelewa kuwalipa kutatufanya tulipe riba ya asilimia 7.5,” alinukuliwa akisema.

Katika mkutano huo, Ngeleja pia aliwataja wamiliki wa Dowans Tanzania Ltd na hisa wanazomiliki katika mabano kuwa ni Dowans Holding S.A ya Costa Rica (81) na Portek.

Huku akirejea barua ya Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brella), aliwataja wakurugenzi na nchi wanazotoka kuwa ni Andrew James Tice (Canada) na Gopalakrishnan Balachandaran (India).

Wengine ni Hon Sung Woo (Singapore), Guy Picard (Canada), Sulaiman Al Adawi (Oman) na Stanley Munai (Kenya).

Wakati Ngeleja akitamka kwamba serikali inajiandaa na kulipa fidia hiyo haraka, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, ameibua utata mwingine baada ya kuutangazia umma kwamba wizara yake haina fedha na haina mpango wa kutenga fedha katika bajeti ijayo kwa ajili ya kuilipa Dowans.

Mkullo alisema TANESCO kupitia wizara yake ya Nishati na Madini, inatakiwa ijipange kusaka fedha za kuilipa Dowans na kamwe fedha hizo hazitatoka Hazina.

Kiini cha sakata hilo kilianza mwaka 2006, wakati TANESCO ilipoingia mkataba wa mauziano ya umeme wa TANESCO na kampuni ya Richmond Development LLC.

Miezi sita baadaye mkataba huo ulihamishiwa kwa kampuni ya Dowans Holdings ya nchini Costa Rica na baadaye kwa Dowans Tanzania Ltd.

Wakati wa utekelezaji wa mkataba huo, ilizuka hoja kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo wabunge kwamba mkataba baina ya TANESCO na Richmond haukuwa halali kisheria hivyo usingeweza kurithiwa na Dowans.

Suala hilo lilizua mjadala mkubwa hali ambayo TANESCO kwa kuwatumia mawakili wa kampuni ya Rex Attorneys ya jijini Dar es Salaam walivunja mkataba huo.

Baada ya kuvunjwa kwa mkataba huo, ndipo kampuni hiyo ikalipeleka suala hilo ICC kama walivyokubaliana na TANESCO kwenye mkataba.

Uamuzi huo wa ICC ulizua mjadala katika siku za hivi karibuni baada ya viongozi wa serikali kutofautiana kuhusu kuilipa kampuni hiyo au kutoilipa.

Katika hatua nyingine, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHCR), kinatarajia kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa serikali kukubali kuilipa Dowans.

LHCR, pia inapinga kusajiliwa kwa tuzo hiyo Mahakama Kuu kwa sababu mikataba ya awali ilipatikana kwa rushwa na kukiuka maslahi ya umma.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Fransis Kiwanga, alisema walitarajia kufungua kesi hiyo jana na itasimamiwa na Kampuni ya Uwakili ya The South Law Chembers Advocates.

Sambamba na hilo pia kituo hicho kimeitaka TANESCO kutokubali kuilipa Dowans hata senti moja kwa kuwa haikuridhia kurithishwa na kuhamishwa kwa mkataba wa Richmond kwenda Dowans.

Aidha ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuacha mara moja kuwabebesha Watanzania mzigo wa kulipia gharama zinazotokana na uzembe, ubadhirifu na ufisadi wake yenyewe huku ikiingilia uhuru na utendaji wa Tenesco kwa kuitaka iilipe Dowans.

“Kwa taifa maskini kama letu lenye matatizo mengi kama ukosefu wa umeme, mfumko wa bei na mengineyo, kutumia hela nyingi hivyo kulipa kampuni ambayo iligundulika kwa uchunguzi sahihi kuwa ni hewa, inatia shaka kwenye umakini wa serikali,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema katika suala la Dowans kuna mambo ya kujiuliza ikiwemo kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilithibitisha kama Richmond ni kampuni hewa, inawezekanaje kuwa na mkataba wa kurithisha mali zake kwa Dowans kwani uhalali wa kisheria wa milki ya Dowans kwa mali ya Richmond, haupo na kuhoji kwa nini serikali haikutaifisha mali za Ricmond tangu awali.

Maswali mengini ni ikiwa Dowans haikurithi kwa uhalali mali ya Richmond, inawezaje Dowans kuwa na madai halali dhidi ya serikali
kuhusiana na mali iliyopatikana kwa uhalifu.

Halikadhalika serikali kuharakisha kuilipa Dowans kuhusiana na mali iliyopatikana kwa uhalifu, je nini hasa maslahi ya Wizara ya Nishati na Madini na kuhoji wizara hiyo inamuwakilisha nani katika suala la Dowans.

Hata hivyo wanaharakati hao walionyesha wasiwasi wao kwa serikali inaposema kuwa inalazimika kuilipa Dowans huku wakihoji kama imefuata taratibu za kisheria na kama shauri hili lilipowasilishwa katika mahakama ya ICC, wananchi walijulishwa kuhusu shauri hilo.

Kwa mujibu wa Kiwanga sababu za kuliendesha shauri hilo kwa siri na kutohudhuria mahakamani kwa mawakili wa serikali, zinatia dosari mwenendo mzima wa suala hili ukizingatia kuwa limegubikwa na ufisadi tangu awali.

Alitoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kupinga hukumu hiyo ya kimataifa na nyingine kama hizo pamoja na maamuzi yoyote ya serikali yasiyokuwa na maslahi kwao zisitekelezwe.

Naye Mkurugenzi wa Tamwa, Annelia Nkya, alivitaka vyombo vya habari kuendelea kupigia kelele sakata hili hadi kuona fedha hizo hazilipwi kwa Dowans.

No comments: