Monday, January 24, 2011

Wafanyakazi Mbeya wamkataa RC

na Gordon Kalulunga, Mbeya
WAFANYAKAZI wa sekta za taasisi na mashirika mbalimbali ya umma na binafsi mkoani hapa wamemkataa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, kupokea maandamano yao ya amani ya kupinga ongezeko la gharama za nishati ya umeme yanayotarajia kufanyika Januari 29, mwaka huu, Tanzania Daima limebaini.

Maazimio hayo yalifikiwa katika kikao cha pamoja cha Shirikisho la Wafanyakazi (TUCTA) kilichofanyika wiki iliyopita mjini hapa.

Kikao hicho kilichojumuisha wajumbe 83 wa matawi ya vyama 11 vya wafanyakazi vilivyounda shirikisho hilo, walikubaliana kumteua Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA), maarufu kwa jina la Sugu kuwa mgeni rasmi wa maandamano hayo kwa kile walichodai kuwa mkuu huyo wa mkoa (RC) hana uwezo wa kufikisha kilio chao kwa wahusika.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa TUCTA Mkoa wa Mbeya, Thomas Kasombwe, alisema wajumbe hao amethibitisha kuwepo kwa maandalizi ya maandamano hayo na waliridhia kufanya maandamano ili kupinga hatua ya Shirika la Umeme (TANESCO) kupandisha gharama za umeme, hali itakayoongeza ugumu wa maisha kwa wafanyakazi kutokana na kipato kidogo wanachokipata.

‘’Kupanda kwa gharama za nishati hiyo ni kuongeza kilio kwa Watanzania walio wengi, kwani watashindwa kumudu gharama za maisha katika familia zao hasa kuwapeleka watoto shule,” alisema Kasombwe.

Kasombwe alisema tayari shirikisho hilo limewaagiza viongozi wa matawi ya wanachama katika maeneo yote kuhamasisha wafanyakazi kujitokeza siku hiyo ili kupinga ongezeko hilo.

No comments: