Sunday, January 2, 2011

Werema anajitia upofu wa Samwel ili iweje?

Abdul Juma
IPO hadithi ya kuchekesha kidogo inayowahusu marafiki wawili Sauli na Samwel. Vijana hawa walikuwa na mitazamo tofauti kiimani na matamanio ya mali.

Sauli alikuwa kijana wa imani aliyependa kusali wakati wote. Na kutokana na imani yake Mwenyezi Mungu alikuwa akimpatia kila alichokiomba.

Lakini hali ilikuwa ni tofauti kwa rafiki yake Samwel ambaye alikuwa kijana mwenye tamaa ya vitu na imani haba kwa Mungu, hivyo maombi yake yalikuwa hayana manufaa.

Siku moja Samwel alimwendea Sauli na kumwambia waombe kwa Mungu ili awapatie kile wanachokitaka. Na kutokana na Samwel kumwamini rafiki yake huyo kuwa ana bahati ya kusikilizwa na mungu na kupatiwa kila ambacho, alimshauri aongoze sala yao.

"Sauli ndugu yangu, wewe una bahati maana chochote uombacho mungu anakusikiliza, sasa leo mimi niko tayari tusali pamoja na utakachokiomba nami ni hicho hicho" alisema Samwel.

Sauli baada kusikia kauli hiyo ya rafiki yake, alimkubalia kuwa wataomba pamoja. Lakini hakujua kumbe mwenziye alikuwa na tamaa ya mali.

Kwa upande wake Sauli alikuwa amekerwa na maovu mengi aliyokuwa akishuhudia watu wakitenda, na kutokana na imani yake kwa mungu aliona ni bora aombe awe kipofu.

Ndipo akarudia kumuuliza rafiki yake Samwel kwa mara nyingine kabla ya kuomba ili kujihakikishia kama kweli yuko tayari kwa chochote kitakachoombwa. Mwenzie akijibu 'niko tayari'.

Hapo Sauli akamwomba Samwel afumbe macho waombe na sala yake ikiwa hii, "Ee mwenyezi mungu, tazama tumechoka kushuhudia maovu haya ya dunia.

Kuanzia sasa mimi na rafiki yangu Samwel tunaomba utupe upofu, tuachane na kuona dhambi hizi za dunia hii" alihitimisha Sauli na kuanzia wakati huo wakawa hawaoni tena.

Lakini katika hali ya kushangaza Samwel alipojaribu kufumbua macho yake bila mafanikio, alianza kumshutumu rafiki yake akimtaka aombe tena ili apate kuona kwa vile hakuwa akitaka upofu.

Kama wewe si mwelewa wa kutambua dhamira za viongozi wetu wa serikali, hadithi hii ya Sauli na Samwel haiwezi kukusaidia. Lakini kwa wale wanaoelewa utapeli wa kisiasa watanielewa.

Tunamshukuru Mungu kwa kuona mwaka mpya wa 2011. Huu hakika ni mwaka mpya kweli, maana tumetoka kwenye vinyongo na visasi vya uchaguzi mkuu, wananchi wanalia na chakachua iliyofanyika.

Haki na kura zao wanaona kama ziliporwa na sasa wamejielekeza kukata mzizi wa fitina, wanataka katiba mpya. Hii ndiyo inaonekana kuwa suluhu ya kuwabana wachakachuaji wa kila kitu.

Kwa majonzi makubwa watawala hawataki kabisa kusikia wimbo huo wa katiba mpya na kila anayejitokeza kuuimba wimbo huo hasemi kama mtawala anatoa maoni yake. Utajiuliza yeye anasimamia nini?

Viongozi wetu wana hulka na tamaa za Samwel, hawaamini kwenye ukweli kama Sauli. Wako radhi kwa wakati huu kujitia upofu wakiamini kuwa Katiba iliyopo haina tatizo na bila haya wanasema eti iweke viraka tu.

Hatuwalaumu kwa hilo bali tunawaombea watoke madarakani wakae upande wa upinzani ndipo wataona umhimu wa katiba mpya, kwa sasa hawawezi, watajitia upofu bila kutaka kwa vile ubovu huo ndiyo unawasaidia kuendeleza ufisadi wao.

Mwanzoni kabisa baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuibua hoja hii ya katiba mpya, Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani ndiye alikuwa wa kwanza kujipofusha na kusema wazi haoni umhimu huo kwa sasa.

Kama kawaida yao kugongana wakati wa kuisemea serikali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye kimamlaka ndiye mkuu wa baraza la mawaziri, alipingana na Kombani akisema madai ya katiba hayakwepeki kwa sasa.

Kisha akatoa ahadi ya kumshauri Rais aunde kamati itakayoratibu mchakato huo, ili kuhakikisha wananchi wanapata katiba mpya inayotokana na wao wenyewe badala ya ile ya mwaka 1977 inayoonekana kubeba mtazamo wa uliopitwa na wakati.

Sasa mitaani kila mmoja anazungumzia hoja hiyo, maoni yameanza kutolewa jinsi gani wananchi washirikishwe. Lakini mapema wiki hii, mwanasheria Mkuu wa serikali naye akajitia upofu kamaKombani.

Mwanasheria Mkuu, Jaji Fredrick Werema alisema kuwa hakuna haja ya Katiba mpya kwa sasa na badala yake hii iliyopo inaweza kufanyiwa marekebisho na kuwekwa viraka kwa kurekebisha vipengele vyenye kasoro.

Kauli yake tunaweza kuiita ya serikali kwa vile yeye ndiye mshauri mkuu wa serikali kisheria, lakini pia kama raia ana haki ya kutoa kauli yoyote kama maoni yake imradi asivunje katiba.

Ila ukweli lazima usemwe kuwa Jaji Werema kajiaibisha yeye mwenyewe, kaiabisha taaluma yake na serikali anayoishauri. Huyu hana tofauti na Samwel aliyekwenda kumshawishi Sauli waombe akijua kuwa watapata mali kumbe hakujua hitaji la rafiki yake.

Hitaji la Watanzania kwa sasa si kutetea wala kuwaonea huruma mafisadi na ving'ang'anizi wa madaraka. Watu wanataka katiba mpya inayoweka mipata ya kuwabana manyang'au wanaokwapuamali za umma, wanaopeana nyadhifa kwa kuangaliana usoni badala ya ufanisi.

Hoja inajengwa kwa kujenga hoja, kama huna hoja si lazima usema. Heri kunyamaza watu watakuelewa kuliko kusema ukawachefua na kujitia aibu. Kama mwanasheria mkuu ndiye huyu asiyeona matatizo ya nchi, bora tuanze kulia mapema. Tafakari na uchukue hatua.

No comments: