Sunday, January 2, 2011

Kujiajiri ni chimbuko la mafanikio

Betty Kangonga




KILA mwanadamu mwenye utashi thabiti huwa na kiu ya kufanya maendeleo kwenye sekta mbalimbali ili aweze kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya teknolojia, uchumi na utamaduni

Maendeleo ya familia na taifa, hayawezi kupatikana iwapo wananchi hawatashiriki kwenye shughuli za kujiongezea kipato ambazo ni halali.

Kwa muda mrefu watu wamekuwa na dhana kuwa kuajiriwa iwe serikali au kwenye sekta rasmi ndiyo msingi wa maendeleo lakini wanadharau kujiajiri ambako ndiko kwenye ajira nyingi zaidi.

Kuajiriwa na utegemezi ndivyo vinayowafanya walio na elimu kushindwa kuitumia ipasavyo pindi wanapokosa kazi za kuajiriwa huku wale wasio na elimu nao kujiona wanyonge, wasio na mwelekeo kwenye maisha yao.

Ni ukweli usiopingika kuwa iwapo watu wataelekeza nguvu zao katika kujiajiri taifa litapiga hatua kwenye maendeleo sambamba na kupunguza umaskini unaozidi kushamiri kadri siku zinavyokwenda.

Utegemezi nao kwa muda mrefu umekuwa ukichukua nafasi kwenye familia ambapo wanawake walionekana kuwa ni watu wa kufanya shughuli za nyumbani huku wakisubiri kuletea huduma na wanaume.

Dhana hiyo ndiyo ilijenga mazoeza kuwa kuna kazi zinazopaswa kufanywa na wanaume na mwingine za wanawake kwa kigezo kuwa ni ngumu na maalum kwa kundi fulan

Katika siku za hivi karibuni utegemezi huo unaonekana kuanza kuota mbawa hasa baada ya wanawake wengi kujiingiza katika shughuli mbalimbali za kujipatia kipato ikiwemo biashara, kilimo, uvuvi na nyinginezo.

Mabadiliko ya kiteknolojia, kukua kwa elimu na mwingiliano wa watu umechangia kwa kiasi kikubwa kuwakutanisha wanawake na kujiwekea mikakati ya maendeleo hasa kwa kujishughulisha na ujasiliamali.

Shani Kondo ni miongoni mwa wanawake waliokata minyororo ya utegemezi na ile ya kudhani kazi za kuajiriwa ndiyo zenye maana na masilahi zaidi kuliko za kujiajiri.

Mwanamke huyo aliamua kuachana na dhana hiyo kwa kuanza kuuza nguo kuu kuu maarufu kama mitumba kwa lengo la kujikomboa kiuchumi.

Anasema alifanya kazi ya kuajiriwa kwa kipindi kirefu bila kupata mafanikio aliyoyatarajia hivyo kuamua kubadili mwelekeo na kujiajiri kwa kuamua kuanza kufanya biashara ya mitumba kwa lengo la kutaffuta maisha bora zaidi

"Si kwamba kazi ya kuajiriwa ni ni mbaya lakini niliamua kugeuka mjasiriamali nia ikiwa ni kufikia lengo la kuwa na uwezo wa kifedha kitu ambacho nilikifanya kwa ujasiri."

Anasema aliamua kuingia katika biashara licha ya kutokuwa na elimu ya biashara jambo ambalo lilimpa wakati mgumu wakati akianza kuuza mitumba.

Anabainisha kuwa alipata wazo la kufanya biashara hiyo baada ya kuona idadi kubwa ya watu wakipenda kununua nguo hizo ama kutokana na bei yake kuwa ya kuridhisha au kwa sababu ya uimara wake.

"Binafsi nilikuwa mteja mzuri wa mitumba na pia niliona idadi kubwa ya watu nao wakizitumia, hivyo niliona ndiyo fursa yangu ya kujiongezea kipato iwapo nitajikita kwenye biashara hiyo" anasema

Shani anasema kama ilivyo kwa mtoto anapohitaji kuanza kutembea ni lazima atafute msaada ndivyo ilivyokuwa kwake ambapo alipata msaada kutoka kwa mtu aliyekuwa akimuuzia nguo hizo ambaye hawezi kumsahau.

Anasema kuwa aliweza kupata msaada na ushauri hata wakati mwingine alikuwa akifuata mitumba hiyo mkoani Mbeya akiongozana na mwalimu wake huyo aliyekuwa akimfunza biashara hiyo.

Anabainisha kuwa baada ya kufanya safari kwa zaidi ya mara mbili aliweza kupata uzoefu na mwaka 2008 ndipo alipoanza rasmi kuifanya pasi kutegemea msaada wa mwalimu wake huyo.

Anasema alipata mtaji wa kuuza mitumba kutoka kwa mchumba wake ambaye ndiye mshauri katika uendelezaji wa biashara hiyo ambayo hivi sasa ajivunia.

Shani kitaaluma ana stashahada ya utawala wa masuala ya hoteli, aliyoitumikia kwa miaka zaidi ya mitano na baadaye kujiingiza kwenye biashara hiyo.

"Nilifanya kazi sehemu mbalimbali na nilipoacha kazi mara ya mwisho nilikuwa hoteli ya Serena iliyoko huko visiwani Zanzibar."

Anasema kwamba pamoja na mambo mengi aliacha kazi ya kuajiriwa kutokana na maradhi ya tumbo yaliyokuwa yakimkabili kipindi hicho ambayo alishayapatia tiba baada ya kufanyiwa upasuaji.

Shani anafafanua kuwa ajira binafsi aliyonayo sasa ina nafasi kubwa ya kumfikisha katika mafanikio zaidi, kuliko angeendelea na kushikilia ile ya kuajiriwa.

"Tatizo letu ni kutokuwa na ujasiri na kuthubutu kufanya jambo jingine na lile tulilolizoea, mimi nilijaribu na hivi sasa najivunia mafanikio niliyonayo" anasema.

Anasema kuwa kutokana na biashara hiyo naweza kulipia kodi ya nyumba, na anamudu kutimiza majukumu mengine pasi na kusubiri mwisho wa mwezi au mshahara kama alivyokuwa ameajiriwa.

"Kwenye kuajiriwa unajituma na kufanya kazi, lakini kipato kipo vile vile hadi itakapofika mwisho wa mwezi, huku kwenye kujiajiri kadri unavyozidisha jitihada ndivyo unavyoongeza fedha."

Anasema kwenye kujiajiri juhudi zaidi ndicho kinachotakiwa na yoyote anayefanya uvivu huharibu maisha, mtaji aliowekeza sehemu husika ttofauti na kwenye ajira ambapo mtu anaweza kuwa mvivu asitambulike kwa hara kutokana na wingi wa wafanyakazi wa sehemu husika.

Anakiri kwamba bado hajafikia lengo alilokusudia kwa sababu ya kutokuwa na mtaji wa kutosha ambao ungemuwezesha kununua mitumba kwa wingi na kuiuza ambapo angepata faida kubwa.

"Mtaji bado ni tatizo kwa wanawake wanaohitaji kujikomboa hivyo ninaziomba asasi na taasisi zinazojihusisha na utoaji mikopo kuweka masharti mepesi ili kila mmoja aweze kupata na itoe elimu juu ya matumizi ya mikopo hiyo" anasema.

Anasema kiu aliyonayo ni kufika wakati akipata mtaji mkubwa ili aweze kufuata mzigo ikiwezekana nje ya nchi na kuongeza upana wa soko.

Shani anasema wanawake duniani kote hivi sasa wameona thamani ya kujishughulisha na kuacha utegemezi jambo ambalo ni muhimu zaidi kwa maisha yao na litawasaidia kutimiza malengo waliyojiwekea.

Anaeleza kwamba katika shughuli yoyote lazima kuna matatizo yanayokabili hivyo biashara yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kununua mzigo na ndani kukuta nyingi zikiwa zimeharibika.

"Kwa kweli hakuna biashara zisizo na changamoto maana nimekuwa nikipita kipindi kigumu kuna wakati ambapo kuna wakati naagiza mzigo na ninapokuja kufungua nakosa kabisa kupata nguo za maana lakini yote namshukuru Mungu na maisha yanaendelea" anasema.

Anasema wakati mwingine inatokea mteja ananunua nguo lakini akabaini kuwa nguo hiyo imetoboka hivyo inabidi umbadilishie na inakuwa hasara.

Anasema jamii bado inapenda kuvaa nguo za mitumba ingawa bado wapo wanawake wanaopenda nguo za asili lakini wengi huzivaa kipindi cha sherehe za harusi, kumuaga binti na zile za kumfunda

"Si kwamba wanawake wanapenda kuvaa nguo za asili pekee bali wapo wanaoona nguo za mitumba ni nzuri na zinaenda na wakati" anafafanua Shani.

No comments: