Sunday, January 2, 2011

Katiba mali ya wananchi si watawala

Christopher Nyenyembe




WANANCHI wanataka katiba mpya, hawataki katiba yenye viraka viraka vilivyobandikwa na watawala wachache tangu Tanganyika ilipopata Uhuru wake mwaka 1961, pale Watanganyika walipojiondoa kwenye mikono ya wakoloni wa Kiingereza.

Umuhimu wa katiba mpya ni wa kimahitaji na umefika wakati ambao suala hilo linapaswa kuwa la kitaifa zaidi kuliko jinsi mgawanyiko wa kiitikadi na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanavyokuwa bubu kulizungumzia suala hili au kutaka kulipa zaidi nguvu ya kichama kuliko utaifa.

Pengine kuna mambo kadhaa ya kujifunza na haitakuwa rahisi kama tunahitaji kujifunza kutokana na machafuko ambayo wenzetu wa nchi jirani yamejitokeza tu kwa sababu ya tofauti za watawala lakini kinyume chake wananchi wa kawaida ndio wanaokuja kuumia.

Nadhani umefika wakati ambao vyombo vya habari, wanaharakati wa haki za binadamu,viongozi wa madhehebu ya dini, wanasiasa, nchi marafiki na wahisani ambao wanaitakia mema Tanzaniawakubali,washawishi na waone kuwa umefika wakati muafaka wa kuwa na katiba mpya itakayoweza kukidhi matarajio ya watanzania wote.

Niliwahi kuandika na hatupaswi kuchoka kuandika kuhusu suala hili la katiba kuwa iwe isiwe, kikombe hiki cha katiba mpya serikali isijidanganye ijue kuwa kikombe hiki hakiepukiki, katiba ni ya wananchi na sio ya watawala wachache wanaodhani kuwa kwa kupuuza kwao jambo hili wanaweza kuwa salama.

Usalama wa viongozi na dhamana kubwa waliyopewa na wananchi wa kuliongoza na kulisimamia taifa hili lisiweze kwenda mrama ni pamoja na uwezo wao wa kufungua akili na masikio yao, kujua na kutambua kwa haraka kuwa sasa wakati umefika mchakato wa kuwa na katiba mpya haupaswi kupuuzwa hata kidogo.

Nashukuru rais Kikwete, amesoma alama za nyakati kuwa taifa linahitaji katiba mpya na juzi wakati akitoa salama za mwaka mpya alisema ameamua kuunda tume ya watalaamu ambao watasaidia kukusanya maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya na baadae watayapeleka kwenye vyombo husika kwa utekelezaji zaidi.

Pamoja na dalili ndogo za wazi zinazojionyesha kuwa wapo baadhi ya viongozi ambao kwa uwezo wao mkubwa wa kujua na kupambanua mambo wangeweza kumwambia wazi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa umefika muda wa kuruhusu rasmi mjadala wa kitaifa kuhusu katiba lakini wanamuogopa.

Pengine kwa mawazo yao wanamuogopa, Rais kwa vile ndiye aliyewateua kushika madaraka hayo waliyonayo au wanamuogopa rais kwa kujua inawezekana wakamuudhi katika kuutoa ushauri huo na kama hatakubaliana nao wanaweza kujikaanga na kuhatarisha vyeo walivyopewa kwa muda mfupi uliopita.

Lakini inawezekana pia katika hilo hata Rais mwenyewe hajui kama kuna watu muhimu kwake ambao wanamuogopa na hawapo tayari kumpa ushauri mzito kama huu wa katiba kwa ajili ya manufaa ya taifa hili na pengine kuwa na kinga madhubuti ya kujiepusha na machafuko ya kisiasa kadri miaka inavyozidi kusogea.

Tukiachia mawazo ya washauri wachache wanaopaswa kumjuza rais juu ya jambo hilo, wapo viongozi wa dini, wanaharakati na nchi marafiki wanaosikia kwa karibu matamanio haya ya wananchi ya kuhitaji katiba madhubuti ya nchi na kuondokana na ile ya urithi kutoka kwa wakoloni ambayo tunaweza kusema kuwa imepitwa na wakati, haifai (Ime-Expire).

Watanzania wanajijua fika kuwa walikuwa koloni la mwingireza na bado ni wanachama wa jumuiya ya madola hilo haliepukiki labda kwa namna nyingine ya kuikana historia ya utumwa na kutawaliwa na taifa hilo ambalo hakuna anayeona umuhimu wa kuwa na sura ya utumwa mamboleo na kujikana kwa akili zetu kutaka kitu ambacho ni chetu.

Zipo njia nyingi za kuishawishi serikali iliyopo madarakani kuona umuhimu huo na ni wazi na dhahiri ya kweli kuwa kuwepo kwa katiba mpya kutaruhusu na kurejesha undugu na upendo mkubwa walionao Watanzania katika kujijenga nchi yao kwa kuwa kitakachoweza kuwaongoza sasa ni mawazo na maamuzi yao waliyoweza kuridhia kwa moyo mkunjufu bila shaka kuwa wanaonewa.

Katiba mpya ndio itakayokuwa msingi wa zama hizi mpya za kufufua maadili ya kitaifa yaliyopotea,kupoteza sura ya uzalendo na kutaka kujenga ukuta imara katika jamii nzima bila shaka wala hofu kuwa Tanzania yenye kuhitaji demokrasia halisi inawezekana na bila katiba mpya lazima watawala waliopo wataiongoza nchi hii kwa hofu na mashaka.

Mbali ya kuwataja washauri kadhaa ambao pengine kwa hulka zao wanaogopa kumweleza ukweli Rais kuhusu hilo lazima tukiri wazi kuwa hata rais mwenyewe kwa nafsi yake,uelewa na ujasiri mkubwa alionao wa kuliongoza taifa hili kwa masikio yake amesikia kuwa sasa Watanzania wanahitaji mchakato wa haraka wa kuwa na katiba mpya.

Hatuwezi kusema eti rais hasikii haya yanayopiganiwa sasa, anajua kabisa kila kinachosemwa na Watanzania zaidi ya milioni 5 waliompa haki ya kuliongoza Taifa hili aliposhinda kwenye uchaguzi mkuu mwaka jana, ni ushahidi tosha na anajua kuwa nchi hii ina watu wanaokadiriwa kufikia zaidi ya milioni 40 ambao kwa wingi huo kuna swali la kujiuliza.

Kwa namna hali ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita huku, taa na kurunzi za wanasiasa zikielekezwa mwaka 2015 na kwa namna hiyo hiyo ya idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza katika uchaguzi huo ipo haja rais akafanya maamuzi sahihi ya kuitengeneza vizuri katiba mpya ili kuwapa kile roho inapenda Watanzania wengi.

Sio siri naweza kusema usalama na amani ya Wazanzibari iliyofanywa na Rais mstaafu,Amani Karume imeweza kumrejeshea heshima kubwa kuliko jambo lolote kwa kipindi cha miaka 10 aliyoiongoza Zanzibari hivyo kwa rais wetu wa Tanzania,Jakaya Kikwete anapaswa kuliona hili la katiba mpya kuwa ndio silaha pekee iliyobaki ya kumletea heshima kubwa mara atakapomaliza kipindi chake hiki cha mwisho.

Afadhali aachane na ahadi zote alizozitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu mwaka jana kwa kuwa yapo mambo yasiyoweza kutekelezaka na machache yatatekelezeka lakini hili la katiba mpya ni mzigo ambao serikali ya awamu ya nne ya Rais Kikwete haiwezi kulikwepa.

Na kwa kutambua hivyo kuwa katiba ndio msahafu mkubwa katika maisha ya hapa duniani ,inayowaongoza watu kuishi kwa haki,uhuru na amani hapo inapaswa kujulikana wazi kuwa katiba ni mali ya umma na sio mali ya watawala wachache,wao watapita lakini umma hauwezi kupita.

Kwa kuitakia nia njema nchi hii na watu wake,maadam kwa pamoja tumeridhia uwepo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa lazima sasa tukubali pia kuiridhia katiba ya umoja wa kitaifa,hicho ndio kilio cha wengi kwa kuwa dalili za mwanzo za watu kutofautiana zimeanza kujionyesha kwa sababu ya itikadi ya vyama vyao,tusifike huko,Katiba mpya haikwepeki.

No comments: