Sunday, January 2, 2011

Kikwete kujinasa kwa katiba mpya?

Ansbert Ngurumo
KAULI ya Rais Jakaya Kikwete kukubali kuundwa kwa katiba mpya ni ya kiungwana; na uthibitisho kwamba CHADEMA waliposusa hotuba yake Bungeni, aliguswa. Na sasa amejua hawezi kushindana na nguvu ya umma.

Lakini kauli yake inapaswa kutazamwa kwa uangalifu mkubwa; kwani imeonyesha sura halisi ya serikali anayoiongoza. Na imempa mtihani mkubwa na kumuweka katika mtego ambapo akikaa vibaya utamnasa yeye mwenyewe.

Yeye ndiye aliyemteua Celina Kombani kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Hata kabla hajakaa ofisini kusoma mafaili, Kombani alionyesha udhaifu mkubwa na upeo mdogo katika suala nyeti kamahili. Akabeza hoja ya mabadiliko ya katiba.

Kauli ya Rais Kikwete ina maana moja kwa Kombani. Ana uwezo mdogo sana kwa kazi aliyopewa. Ni waziri asiye na upeo wa kuongoza Wizara ya Katiba na Sheria. Kauli ya rais wake, imemshushua yeye.

Maana yake ni kwamba waziri haaminiki hata kwa rais mwenyewe aliyemteua. Angekuwa muungwana, Celina Kombani angejiuzulu.

Na kama akikataa kujiuzulu, Rais Kikwete mwenyewe anapaswa kumwondoa katika wizara hiyo. Kama wote watashindwa kuchukua hatua, basi, rais na waziri wake watakuwa wameonyesha udhaifu mkubwa kwa mara nyingine.

Lakini Rais Kikwete ana mtego wa pili. Ndiye alimteua Jaji Frederick Werema kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Katika hali isiyotarajiwa, Jaji Werema amejikuta akifanya kazi ya siasa badala ya kazi ya sheria. Naye akabeza hoja ya katiba mpya; akasema kinachohitajika ni viraka katika katiba ya zamani.

Huyu ndiye mshauri mkuu wa rais katika masuala makubwa ya kikatiba na kisheria. Kauli ya rais kukubali katiba mpya ina maana kwamba Jaji Werema alikurupuka. Ama hakusoma alama za nyakati na mahitaji ya taifa; au hakujua hata mchezo wenyewe wa siasa aliotaka kuucheza kulinda uhafidhina wa chama tawala na serikali iliyo madarakani.

Kwa kiongozi, mwanasheria ambaye amefikia hadhi ya kuitwa jaji na akapewa dhamana kubwa kama aliyonayo; Jaji Werema amekatisha tamaa wananchi waliokuwa na imani naye, hasa wale waliokwishachoka kuona ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali ikishindwa kutumika kulinda maslahi ya nchi, inalinda ya wachache wenye vyeo na nguvu, kama ilivyotokea huko nyuma.

Je, naye anajiona shujaa baada ya kushushuliwa na rais? Kwa nini naye asifanye kile tunachomshauri KombaniĆ¢€“ kujiuzulu? Na kama hataki, rais anaona tatizo gani kumpa kazi nyingine inayolingana na uwezo na upeo wake?

Lakini kuna mtego mwingine ambao unaweza kumnasa rais katika hoja hii. Amesema kwamba atateua mwanasheria aliyebobea kusimamia na kuongoza tume ya kuangalia upya (kurekebisha) katiba.

Watanzania wenye akili timamu wanaamini kwamba mwanasheria huyo atakuwa na viwango vilivyo juu ya hivi alivyoonyesha Jaji Werema; na wala hatakuwa Werema.

Maana sote ni mashahidi kwamba inawezekana ana uwezo katika masuala kadhaa ya kisheria, lakini katika hili, Jaji Werema hajabobea. Rais asifanye kosa kumpa kazi hiyo. Ataichakachua!

Kama kweli Rais Kikwete ametoa kauli yake kwa nia njema na kama anaamini kwamba historia ya Tanzania inapaswa kuandikwa upya baada ya miaka 50 ya uhuru, na kama anataka kukumbukwa kwa urithi mwema wa katiba mpya; aunde tume inayoongozwa na watu ambao hawajipendekezi kwa serikali. Iwe chini ya watu huru, wasioogopa kupendekeza yasiyopendwa na wakubwa; wasiotafutwa kuonekana na "kurushiwa makombo."

Maana wanasiasa wetu, hasa hawa wa viwango wa Kikwete, hawaaminiki katika mambo nyeti kama haya. Wana kawaida ya kutanguliza maslahi ya vyama vyao, watu wao na serikali wanayoiongoza. Wana tabia ya kuishi ndani ya kapu na kuogopa mawazo mapya, na maamuzi magumu.

Na tume za marais si jambo la kujivinia sana hapa kwetu. Zimeundwa nyingi huko nyuma. Ripoti zake na mapendekezo yake, vimepuuzwa.

Rais Ali Hassan Mwinyi aliunda Tume ya Nyalali kuhoji wananchi kama wanataka mfumo wa vyama vingi au kimoja. Ikahoji wana CCM. Wakakataa mfumo wa vyama vingi. Hata wasio wana CCM waliokuwapo wakati ule, si wote walikuwa tayari kwa vyama vingi.

Wakati serikali inajiandaa kutekeleza hujuma yake ya kukataa vyama vingi kwa kutii mapendekezo ya wananchi, Baba wa Taifa akaingilia kati, akailazimisha ikubaliane na wachache. Kwa kuwa serikali ililazimishwa, ndiyo maana hadi leo inaendelea kufanya hujuma mchana na usiku dhidi ya wanaoipinga na kuikosoa.

Leo, katika mazingira ambayo Baba wa Taifa hayupo kumshinikiza Kikwete, nani anaamini kwamba matakwa ya wakati ndiyo yatakayozingatiwa?

Mazingira kama hayo yalitokea mara mbili wakati Rais Benjamin Mkapa alipounda Tume ya Warioba kuchunguza mianya ya rushwa, na Tume ya Jaji Kisanga kuhoji wananchi juu ya suala hili la katiba kwa mfumo wa White Paper.

Ni nani miongoni mwetu anayeweza kusema pasipo shaka kwamba serikali ya Mkapa ilifanikiwa kupiga vita rushwa? Ni mara ngapi tumemsikia Jaji Warioba akinung'unika pembeni na waziwazi kuhusu kupuuzwa kwa mapendekezo yake?

Hata baada ya Jaji Kisanga kuwasilisha maoni ya tume yake na kupendekeza mfumo wa serikali tatu kama hitaji la wakati, Rais Mkapa alimshambulia na kumshuhua hadharani. Kisa alitoa mapendekezo ambayo serikali haikuyataka.

Katika jeuri hii ya ulevi wa madaraka na kushindwa kusoma alama za nyakati, ni kwa nini tusitilie shaka hata nia ya sasa ya rais kuunda tume ya marekebisho ya katiba?

Na kinachoanza kutia shaka ni kauli ya rais mwenyewe. Amesema: "Baada ya makubaliano kufikiwa, taifa letu litapata katiba mpya, itaamuliwa lini ianze kutumika, pasiwepo kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana wala kushinikizana. Washiriki waongozwe na hoja badala ya jazba."

Kwa msomaji wa kawaida, kwa juu juu, rais ametamka maneno mazuri tu. Ni kauli ya kawaida. Lakini kwa mtu anayejua kusoma na kutafsiri msingi na nia ya kauli, ataona kuna kitu kimefinyangwa kwenye kauli hii.

Kwanza, hakuna haja ya kuhofia kutukanana. Kwa nini watu waungwana watukanane wakati wanashirikiana vema kwa nia ile ile? Na kwa kawaida, watu (hata wasio waungwana kabisa) huwa hawaamki na kutukanana tu. Yapo mazingira yanayochokoza watu hao kutukana. Haya ndiyo rais anapaswa kuhakikisha kwamba hayatakuwapo.

Lakini hoja nzito kama hii haiwezi kujengwa bila msuguano wa hisia, na hoja kinzani. Maana makubaliano hayafikiwi kirahisi hivi hivi, hasa katika jamii iliyogubikwa na uhafidhina wa watawala.

Kama serikali au chombo chochote kitathubutu kufanya ghiliba za kutumia tume hii kuhujumu mchakato wa katiba mpya, kushutumiana, kudharauliana, kubezana, kuzomeana na kushinikizana kutajitokeza.

Lakini hata katika mazingira ya kawaida ya ushindani wa kisiasa, linapojadiliwa jambo zito kama hili, hoja haziwezi kujengwa kama vile watu wako katika nyumba ya ibada. Msuguano utakaojitokeza ni zao la lazima la mchakato wenyewe.

Kwa hiyo, rais anafanya makosa kutisha watu wasijadiliane, wasitofautiane, na wasitumie staili mbalimbali za kujadiliana kupata watakacho.

Maana kama serikali yake yenyewe haina kauli moja (rejea ya Kombani, Werema na Rais Kikwete) itakuwaje mchakato unaohusisha wadau wengi zaidi, kutoka mazingira tofauti, uanze na kuhitimishwa bila mikwaruzo? Kama mikwaruzo haitakuwapo, itapatikana wapi furaha ya "makubaliano" anayozungumzia?

Lakini Rais Kikwete atakuwa muungwana kweli kama atatazama na kusoma kwa umakini rasimu zilizo tayari na ambazo zimekuwa zinapigiwa debe kwa miaka kadhaa sasa. Zimeandaliwa na wanaharakati na wanasheria waliobobea, wanaotazama zaidi maslahi ya taifa kuliko chama, wasioomba upendeleo au kazi serikalini.

Asiwe wa kwanza kubeza wengine. Wawaulize CUF na CHADEMA. Watamuonyesha pa kuanzia. Maana hata mjadala huu hajaukubali kwa dhati, bali ameshinikizwa na nguvu ya hoja na matakwa ya wakati. Na CHADEMA waliposusia hotuba yake Bungeni, hiki ndicho walikuwa wanatafuta. Sasa kama amekubaliana nao, asiwabeze, awaunge mkono, mchakato uanze.

No comments: