Sunday, January 2, 2011

Hili la Katiba litazamwe kwa makini

JUZI Rais Jakaya Kikwete, katika hotuba yake ya kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011 alizungumza mambo mengi lakini kubwa zaidi ni serikali kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya Tanzania ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikipigiwa kelele haiendani na wakati.

Wadau mbalimbali kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakipaza sauti zao kutaka Katiba ifumuliwe na kuundwa nyingine huku wakiweka bayana baadhi ya vipengele ambavyo vinaonekana kutokukidhi matakwa ya hivi sasa.

Rais Kikwete, alisema ameamua kuunda Tume Maalum ya Katiba, ambayo itaongozwa na mwanasheria aliyebobea, itakayokuwa na wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii hapa nchini kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, jukumu la msingi la tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato utakaowashirikisha wananchi wote bila kubagua, vyama vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanataaluma na makundi mbalimbali ya watu wa nchi yetu kote nchini, katika kutoa maoni yao juu ya wayatakayo kuhusu Katiba ya nchi.

Tunapenda kuchukua fursa hii, kumpongeza Rais Kikwete, kwa kuona haja ya uwepo wa Katiba mpya licha ya baadhi ya watendaji wa serikali yake akiwemo Mwanasheria Mkuu, Fredrick Werema, kuweka bayana kuwa hakuna haja ya kuwa na Katiba mpya bali iliyopo ifanyiwe marekebisho

Pamoja na kumpongeza Rais Kikwete, kwa hatua hiyo lakini tayari baadhi ya wadau wameshajitokeza kupinga utaratibu alioutangaza Rais Kikwete wa kushughulikia mchakato huo kwa madai kuwa timu ya waratibu wa zoezi hilo watokane na baraza la Katiba ambalo halitakuwa likiegemea upande wowote.

Hoja za wadau hao ni kuwa uteuzi huo wa rais unaweza ukawa na ushawishi kwa wajumbe kuchukua maoni fulani kulingana na matakwa ya aliyewateua (Rais) na hata pale yatakapofikishwa bungeni kwa ajili ya maamuzi ambako idadi wa wabunge wa chama tawala ni wengi wanaweza kupitisha jambo ambalo si hitaji la Watanzania.

Ipo mifano mingi ambayo tume kadhaa ziliundwa na Rais Mstaafu Alli Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa ambazo mwisho wake ziliishia kuweka viraka kwenye katiba na hata mambo mengine ya umuhimu zaidi yalitupwa kapuni.

Mwaka 1991, iliundwa tume iliyokuwa chini ya uenyekiti wa marehemu Jaji Mkuu mshastafu Francis Nyalali, ambayo ilikusanya maoni namna ya Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi na hatimaye ikatoa mapendekezo ya kubadili Katiba ili iendane ya mfumo huo kwani iliyokuwapo ilikuwa ni ya chama kimoja tena ya kurithi kutoka katika serikali ya kikoloni.

Katika juhudi za kupata Katiba mpya Mwaka 1991, Tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa utawala wa vyama vingi vya siasa na kupendekeza kuwepo kwa Katiba mpya na si kurithi Katiba ya chama kimoja ambayo mhimili wake ulikuwa tofauti.

Hoja hizo hazikupewa majibu na vyama vingi vya siasa viliingizwa ndani ya Katiba ya mwaka 1977, kupitia mabadiliko ya Nane ya mwaka 1992, yaliyotungiwa Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya 1992.

Mwaka 1998 Kamati ya "White Paper" ilipoundwa chini ya Jaji wa Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Jaji Robert Kisanga, ambayo pia ilipendekeza umuhimu wa kuwa na Katiba mpya.

Tunajua Rais Kikwete, ana nia ya dhati ya kuundwa kwa Katiba mpya lakini ni vema jambo hili likafanyika kwa umakini mkubwa ili kuepusha nchi kuingia katika malumbano ambayo mwisho wake hautakuwa mzuri.

Tungependa mchakato huu ufanywe kwa taratibu zitakazokubaliwa na pande zote badala ya kufanyika kwa hila au upendeleo kwa misingi ya itikadi za vyama au maeneo fulani.

Tunakubaliana na Rais Kikwete kuwa jambo muhimu ni kujenga Tanzania moja yenye ushirikiano, lakini jambo hilo halitoweza kufanikiwa iwapo kasoro au maoni yanayotolewa na wadau hayatoweza kufanyiwa ipasavyo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Katiba ni muhimu kwa Watanzania wote, hivyo si muhimu kwa chama tawala au kile cha upinzani kujigamba au kufanya hila ili kionekane chenyewe ndicho chenye haki ya kudai au kuzima madai hayo kwa masilahi ya chama au kundi la watu fulani.

Zanzibar waliweza kufanya mabadiliko ya Katiba yao ili kuridhia serikali ya Mseto baina ya vyama vya CCM na CUF hivyo ni vema utulivu ulioonyeshwa visiwani humo uendelee hata kwa mchakato huu wa sasa.

Tanzania ni moja kila mtu ana mchango wake hivyo hakuna sababu ya kugombea fito, hakuna mtu aliyezaliwa ili amtawale mwingine au mwingine awe mnyonge dhidi ya mtawala.

Tuliamua kuwachagua watawala ili waweze kutuongoza kwa maslahi yetu na wala si kwa ajili ya kuweka mbele maslahi ya chama, mtu binafsi au kundi la watu fulani.

No comments: