Sunday, January 2, 2011

Slaa: JK anamiliki Dowans

• Asema hana nia ya kuunda Katiba mpya

na Mwandishi wetu
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willbrod Slaa amesema kuwa Rais Jakaya Kikwete ni dikteta.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Dk. Slaa, alisema kitendo cha Rais Kikwete, kutangaza kuwa ameunda tume ya kuanzisha mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya na atateua kiongozi na wajumbe kinaashiria kuendeleza udikteta wa uongozi.

Alibainisha kinachotakiwa kuanzishwa hivi sasa ni Constitutional Assembly au Baraza la Katiba (Bunge la Katiba) ambalo ndilo litakalokuwa na wajibu wa kuratibu kura za maoni ya wananchi juu ya uundwaji wa Katiba mpya.

Alisema kitendo cha Rais Kikwete, kutangaza kuunda tume ni kiini macho na kinadhihirisha hana nia ya kutaka kuundwa kwa Katiba mpya.

"Huyu Rais wetu haonyeshi kama yuko 'serious' katika uundaji wa Katiba mpya, anataka kuweka viraka ili aendelee kututawala kidikteta!" alisema.

Aliongeza kuwa kwa kawaida Baraza la Katiba ambalo hapa nchini halipo ndilo lenye jukumu hilo na linatakiwa lifanye mchakato huo kwa kuishirikisha serikali, Bunge, wadau na wananchi.

Alisema hakubaliani na tume ya kuratibu mchakato huo, kwani inaweza kufanya kazi kwa utashi wa aliyewateua na hata Bunge pia linaweza likatumbukia kwenye mtego wa kupitisha kitu kisichokuwa matakwa ya wananchi kwa sababu ya wingi wa wabunge wa chama kimoja.

Alisema katika nchi zote zilizoandika upya Katiba au kutengeneza zilipitia njia ya 'National Constitutional Congress au Convention' (Constitutional Assembly) ambapo ilikubaliwa kati ya serikali, Bunge, wadau mbalimbali na wananchi katika majukwaa yao.

"Constitutional Congress ni chombo kitakachoratibu maoni ya wananchi na wadau mbalimbali na siyo mtu aliyeteuliwa na Rais ambaye anafanya kazi kwa ajili ya kumfurahisha jambo ambalo ni kuendelea kuweka viraka" alisema.

Alisema baada ya chombo hicho kuundwa, maoni ya wadau, wananchi mbalimbali hukusanywa kwa njia itakayokubalika.

Dk. Slaa alisema kuwa 'Constitutional Congress hukaa tena kupitia maoni yote kipengele kwa kipengele na kukubaliana na siyo Rais Kikwete na tume atakayounda jambo ambalo liliwahi kutokea huko nyuma.

Alisema inawezekana Rais Kikwete, hafahamu au kwa makusudi amepuuza kilio cha wananchi ndiyo maana ameunda tume inayowajibika kwa maslahi yake.

Alisema kuwa Katiba siyo mali ya Rais wala ya serikali iliyoko madarakani, bali ni mali ya wananchi.

Dk. Slaa alisema wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa wanahitaji chombo chao ambacho kinaweza kuwekewa utaratibu na Bunge, baada ya kupitishwa na Azimio la Bunge, lakini siyo mtu au watu wa tume wanaochaguliwa na Rais.

"Tume hiyo haikubaliki kabisa tunachotaka tunajua hakitakubalika kwa maana hakuna serikali duniani itakayounda tume ya kujinyonga yenyewe, mabadiliko makubwa kwa vyovyote, hayakupendwa na serikali iliyoko madarakani" alisema.

Alisema ana imani kuwa tume hiyo haiwezi kuleta Katiba mpya hivyo kutoa nafasi kwa Rais Kikwete kuendelea kuongoza katika sura ya kidikteta kwa kupitia Katiba ya sasa iliyopitwa na wakati.

Dk. Slaa alisema kuwa inashangaza katika hili ambapo hata Zanzibar wamepiga hatua kwani waliweza kuruhusu kukusanya maoni ya uundaji wa serikali ya kitaifa na si kuundwa kwa tume.

Alisema Katiba mpya haiwezi kamwe kupatikana kwa njia ya tume hiyo (Constitutional Review Commission) kwani zilishawahi kutokea tume za aina hiyo na hakuna kilichofanyika.

Alibainisha kuwa jambo hilo halina tofauti na tume zilizowahi kuundwa na Rais Mstaafu Ally Hassan Mwinyi pamoja na ile ya Benjamin Mkapa ambapo matokeo yalikuwa ni kuweka viraka kwenye Katiba tuliyonayo hivi sasa.

"Uzoefu wa Tume za Mwinyi na Mkapa ni kuwa maoni yalikusanywa kwa upendeleo, hojaji zilipelekwa kwenye matawi ya CCM, halmashauri za wilaya vyombo ambavyo vyote ni vya CCM, hatimaye serikali ikatoa mapendekezo ya vifungu vya kurekebishwa na vingine kuachwa, alisema na kuongeza: "hatua hii inawezekana kwa kuwa tume ni ya Rais, na Rais kama alivyosema mwenyewe ndiye atakayepeleka marebisho kwa vyombo husika (Bunge) ambalo karibu lote ni la CCM bado wana wabunge wengi pamoja na kuwa wapinzani wameongezeka sana" alifafanua.

Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alisema ameshangazwa na kitendo cha Rais Kikwete kushindwa kufafanua kuhusu suala la kulipwa kwa Kampuni ya Dowans sh bilioni 185 na Shirika la UmemeTanzania (TANESCO).

Alisema fidia hiyo iliyoamriwa na mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya biashara (ICC) hivi karibuni kuwa TANESCO inapaswa iwalipe Dowans fedha hizo baada ya kuvunja mkataba wa kununua umeme.

Alisema kimsingi uvunjwaji wa mkataba huo na sakata zima ni uzembe ambao unapaswa uwekwe wazi na watu wachukuliwe hatua lakini Rais Kikwete haonyeshi kushtushwa na jambo hilo.

Alisema kutokana na majibu ya kiongozi huyo inaonyesha kuwa naye ni sehemu ya kampuni ya Dowans.

Alisema Rais anaonyesha udikteta kwa kuamua kulibeba shirika la umeme nchini (TANESCO) huku wananchi ambao ni walalahoi wakiendelea kunyongwa na upandaji wa gharama hizo.

"Hasemi kuwa kitendo cha kulipa kampuni hiyo kimesababishwa na uzembe wao wenyewe kwa kuleta mitambo ya Richmond iliyozaa Dowans huku yeye akiwa sehemu ya kampuni hizo ameamua kuficha uovu wao" alieleza.

Alisema wataendelea kuhamasisha maandamano pamoja na kupinga gharama kwa kuwa vyama vya upinzani havikusajiliwa kwa Rais bali vimekuwepo kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha vinakataa uozo unaofanywa na serikali.

Dk. Slaa alisema Rais Kikwete amesahau hali ngumu inayowakumba wananchi imetokana na maamuzi mabovu yaliyoanzishwa na wanasiasa wenzake kwa kukubali kufanya mchakato wa IPTL.

"Eti Rais Kikwete anasema upandaji wa umeme ni suala la kibiashara na wanasiasa wasilizungumzie kisiasa inawezekana hana uchungu na Watanzania wanaoshindwa kununua umeme kwa ajili ya kuendeleza biashara zao" alisema.

Alisema vyama vya upinzani vina haki ya kujadili masuala mbalimbali na siyo kama anavyodai kufanya hivyo ni kuendeleza malumbano na ikiwa hataki vyama vifanye hivyo basi hana budi kuvifuta.

Wakati huo huo Chama cha Wananchi (CUF), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete, kutekeleza kwa vitendo ahadi yake aliyoitoa juu ya kupata Katiba mpya itakayokuwa na maslahi ya Watanzania wote.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, bara, Julius Mtatiro, alisema kuwa kitendo cha Rais Kikwete, kukubali kuundwa kwa Katiba mpya kuendane na vitendo hasa kuiunda upya na sio kuifanyia marekebisho kama ilivyokuwa awali.

Alisema Tanzania imefanya marekebisho mara 14 lakini bado kumekuwa na malalamiko hali inayoweza kuleta machafuko nchini na kuipa nchi doa.

Alisema ni kipindi kizuri kwa Rais Kikwete kuiga mfano wa Rais wa Zanzibar wa awamu ya sita Amani Karume kwa kuridhia maridhiano yaliyoleta sura mpya ya Zanzibar.

Alisema suala la Katiba mpya limekuja wakati muafaka, kabla ya kutokea kwa misukosuko inayoweza kuchafua hali ya utulivu na amani ya nchi hatua itakayofanya kupoteza sifa hasa pindi amalizapo muda wake mwaka 2015.

Hata hivyo chama hicho kilimtahadharisha Rais Kikwete kuhakikisha anatembea katika kauli zake hasa kwa kuunda tume makini itakayokuwa huru na isiyokuwa na upendeleo au agenda ya kuibeba CCM, hasa kwa kufanya maamuzi ya upande mmoja.

Aidha katika hotuba yake Rais Kikwete aliahidi kuunda Tume Maalum ya Katiba (Constitutional Review Commission), itakayoratibu mchakato kwa kushirikisha wananchi wote ili waweze kutoa maoni yao juu ya yale wanayotaka yaingizwe katika Katiba mpya.

No comments: