Sunday, January 2, 2011

Viongozi wa dini waibana serikali

• Wataka mafisadi wasipewe nafasi 2011

na Waandishi wetu




UMOJA wa Makanisa Tanzania, umeionya serikali kutoruhusu watuhumiwa wa ufisadi kuingilia utendaji wa serikali ikiwemo mchakato wa uundaji wa Katiba mpya.

Onyo hilo limetolewa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) dayosisi ya Iringa na Dk. Owdenburg Mdegella, kwenye mkesha wa kitaifa wa kuukaribisha mwaka mpya.

Mkesha huo ambao uliandaliwa na Umoja wa Makanisa Tanzania, ulifanyika katika Uwanja wa Samora mkoani Iringa ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Kaimu Mkuu wa mkoa wa Iringa Evarista Kalalu.

Mdegella, alisema kuwa ili Tanzania iweze kupata Katiba mpya ambayo itamkomboa Mtanzania na kuwepo kwa chaguzi za kidemokrasia ni vizuri zoezi la mchakato mzima wa katiba hiyo kufanyika kwa umakini mkubwa bila kuwepo kwa mkono wa kiongozi yeyote kutafuta maslahi yake ama kundi lake.

"Sisi kama viongozi wa dini tunaomba asiwepo mtu wa kuingilia kuvuruga mchakato wa kuandaa Katiba yetu...tunataka iwe nzuri ambayo kila mmoja ataipenda kuchekelea hadi lionekane jino la mwisho la Krismasi."

Mdegella, aliomba uwepo umakini mkubwa katika kuandaa Katiba hiyo ili isije kuwa chungu kwa Watanzania na kuwa ili mchakato huo uweze kufanikiwa lazima kila mwananchi apate kushirikishwa katika mchakato huo hata kwa njia ya maombi.

Hata hivyo alisema kuwa mwaka 2010 ulikuwa ni mwaka uliotawaliwa na vitendo vya ufisadi na mauaji ya albino na vikongwe na kuwa si vema kwa taifa kuruhusu mambo hayo kuvuka mwaka huu 2011.

Askofu Mdegella alisema viongozi wa dini bado wana kazi kubwa ya kuendelea kuwaombea wale wote wanaotegemea ufisadi kuendesha maisha yao na wale wanaoendelea kufanya uchakachuaji wa bidhaa mbali mbali.

Alionya serikali kutoruhusu mijadala ya kukuza udini na ukabila kwa Watanzania.

Naye Kaimu Mkuu wa mkoa wa Iringa Kalalu, alisema serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na taasisi zote za dini bila kuzibagua.

Naye Askofu, Mkuu wa Kanisa la Full Gospile Bible Fellowship, lililoko Mwenge jijini Dar es Salaam, Zacharia Kakobe, alisema katika kipindi cha miaka mitano ya Rais Kikwete Watanzania hawana cha kumkumbuka kwa kuwa kumekuwa na malalamiko ya ufisadi, watu kuonewa, haki kukosekana na mengineyo.

Alisema kuwa Rais Kikwete anaweza kufuta mabaya hayo ya nyuma iwapo ataamua kuanzisha mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya pamoja na kupambana na ufisadi.

Kakobe alisema kuna viongozi wanapoondoka madarakani wananchi wanaendelea kuwakumbuka ambapo alimtolea mfano aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili Ally Hassan Mwinyi pamoja na mabaya yake lakini wananchi hadi sasa wanamkumbuka na sera yake ya 'ruksa'.

"Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere hadi leo tunamkumbuka kwa alivyochukia ubaguzi na kutufanya wote kuwa sawa ambapo aliweza kutuunganisha kwa lugha ya Kiswahili, alisema na kuongeza kuwa: "....hata aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa anakumbukwa kwa kutuachia barabara nzuri na daraja la Rufiji hata kama wapo wanaoamka na kumshambulia wakikumbuka hayo mema wanaacha na kukaa kimya" alisema.

Alisema Rais Kikwete anatakiwa kufahamu kuwa madaraka yana mwisho hivyo ni vyema akajiandaa sasa kuhakikisha wananchi wanatambua mchango wake kabla ya kuondoka.

"Lazima ujiulize ukitoka katika madaraka leo au hata kufa kwako Watanzania watakukumbuka kwa lipi, je kwa ukatili wako au kwa jinsi ulivyosababisha maisha magumu, basi kuna haja ya viongozi kufanya mambo ambayo hayatasahaulika" alisema.

Kakobe amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha anatumia fursa ya miaka michache iliyobaki kufanya jambo jema ambalo litawafanya Watanzania wamkumbuke pindi atakapoondoka madarakani.

Katika mkesha uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Askofu Godfrey Malasi, alisema kuwa rushwa imekuwa ni pigo la wanyonge kukosa haki katika nchi yao kwa kuacha wachache wakiendelea kujinufaisha.

Malasi alisema kuwa baadhi ya Watanzania wametekwa na dhambi ya kunyonya rasilimali za nchi kwa manufaa yao na kuacha Watanzania wakiendelea kuteseka kutokana na kukwapua haki zao.

Alisema ni vema serikali ikawabana na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wanaotumia rasilimali za taifa kwa maslahi binafsi ili wananchi wafurahie maisha.

"Tuombe dua ya kukomesha watu wanaotumia rushwa ambayo kwao ni sehemu ya maendeleo na kuwaacha Watanzania wakiwa na amani yenye mateso ya kuporwa rasilimali zao na wachache" alisema Malasi

No comments: