Tuesday, December 28, 2010

umuhimu wa malengo katika maisha

Ili uweze kufanikiwa maishani unatakiwa uwe na mipango ya maisha yako.Mara nyingi watu wengi wamekuwa ni hodari wa kupanga mipango ya harusi na mambo mengine madogo madogo lakini wanasahu kupanga mipango ya maisha yao. Kama huna mipango juu ya maisha yako si rahisi kupata mafanikio. Kuweka malengo ni mchakato wa kufikiria juu ya maisha yako ya baadaye na kuyabadili kutoka kwenye hali duni au hali uliyonayo kwa sasa na kuwa yenye mafanikio. Maisha ni safari ndefu hivyo ni vyema ukajua unakwenda wapi na utafikaje huko unapotaka kwenda.Kujua malengo yako kutakusaidia kuwa na muelekeo na kukusanya nguvu zako zote kwenye jambo unalolitaka. Mara nyingi huwa nawauliza watu swali hili ninapiojadili kuhusu malengo, Jee kama unasafiri na hujui unakokwenda ukifika kwenye kituo cha magari ya kubeba abiria utapanda gari la kwenda wapi? Wengi hunijibu kwamba utapanda gari lolote na kwa sababu hiyo, kwa vile hujui unakokwenda kwa hakika huwezi kufika huko. Huo ndiyo umuhimu wa kuweka malengo kwani ni sawa na msafiri anayejua anakokwenda hivyo akifika kituoni atajua apande gari gani na hakika atafika anakokwenda. Kwa hiyo si swala la ajabu kuona watu wengi wakihangaika kutafuta mafanikio bila kuchoka lakini hawafanikiwi kwa sababu ya kutojua siri hii.
Kutokuwa na malengo kumewafanya watu kufanya shughuli nyingi kwa wakati mmoja na vilevile kuziacha baada ya kuona kwamba ni ngumu.Watu hawa hufanya hivyo kwa kushawishiwa au kwa kuiga baada ya kuona wengine wakifanya biashara ya aina fulani. Ndiyo maana mtu mmoja akianzisha duka mtaani basi watu wengine nao wanaanzisha duka na hivyo unakuta maduka mengi katika mtaa huo mpaka mengine yanakosa wateja.Mimi mwenyewe nimewahi kukumbwa na tatizo hili, nimefanya biashara nyingi sana, nimewahi kufanya biashara ya mtandao kuuza bidhaa za makampuni kadhaa, ukandarasi, vyuma chakavu na kutengeneza chaki. Baada ya kutafuta ushauri nilifundishwa namna ya kujiwekea malengo ndipo nikaamua kutoa huduma ya ushauri wa biashara. Kwa sasa hivi kwa vile ninajua ninachokitaka na nimekwisha jiwekea malengo yangu siwezi kuyumbishwa na kujishughulisha na biashara nyingine.
Upangaji wa mipango na kuweka malengo hufanywa na Wafanyabiashara wakubwa, wanamichezo maarufu na wasanii maarufu. Utaratibu huu huwasaidia kuwapa muelekeo na malengo ya muda mfupi yaani mwaka mmoja, muda wa kati yaani miaka mitatu hadi mitano na na muda mrefu yaani miaka kumi na kuendelea. Pia huwasaidia kukusanya nguvu na maarifa ili kufikia malengo yao kwa urahisi. Malengo huanzia kwa kuwa na picha kubwa ya hali halisi unayoitaka kwa kujiuliza ni nini unachokitaka maishani mwako? Na kisha huvunjwa vunjwa kidogo kidogo . Maisha ya binadamu yamegawanyika klatika sehemu mbali mbali kama vile kiuchumi kiafya kisaikolojia na kiafya. Kwa mfano,mafanikio ya ya mwanafunzi hupimwa kwa maksi zake anazopata darasani lakini kiuchumi ni jinsi alivyo na pesa nyingi benki pamoja na vitegauchumi alivyonavyo pamoja na shughuli anayoifanya ambayo inamuingizia kipato. Mambo mengine ni mahusiano mazuri aliyonayo kwenye jamii na familia yake. Pia bila kusahau afya yake, kwani hakuna utajiri mkubwa kwa binadamu kuliko afya yake.
Mambo muhimu ya kujiuliza katika kupanga malengo ni yafuatayo;
Jee unataka kufanya kazi au shughuli gani maishani mwako? Jee ungependa kupata fedha kiasi gani kutokana na shuguli unayotaka kuifanya? Jee maarifa/elimu ipi ambayo ungependa kuipata ili kuweza kukusaidia kufikia malengo yako? Mtazamo gani au ni mabadiliko yapi ya tabia unayotakiwa kuyafanya ili ufikie malengo yako? Tafakari mambo haya . Wataalamu wa maswala ya biashara wanashauri ufanye biashara ambayo inaendana na kipaji au elimu yako, kwani kwa kufanya hivyo utapunguza muda wa kujifunza mambo mapya. Mara nyingi kuamua ufanye biashara gani ni suala gumu na mimi nimekuwa nikikutana na watu wakiwa na mtaji lakini hawajui wafanye biashara gani.

Baada ya kupanga mipango yako kama nilivyokueleza hapo juu unatakiwa kuanza utekelezaji mara moja. Ni vyema kila mwaka unapoanza uwe na mipango pamoja na malengo ya mwaka huo na inapofika mwisho wa mwaka unaangalia malengo yapi uliyoyatekeleza na yapi hukuyatekeleza. Pia ujiulize sababu zilizosababisha usitekeleze malengo hayo. Yale mambo/ malengo ambayo hukuyatekeleza mwaka uliopita unapaswa kuyatekeleza mwaka unaofuata. Katika utekelezaji si mambo yote unaweza kuyafanya kwa mara moja unaweza kuyapangia mipango kwa mfano kila siku unaweza kuorodhesha mambo utakayofanya kesho yake kuanzia saa 12 asubuhi saa mpaka saa 12 jioni jambo linaloshindikana leo unalipeleka kesho. Vivyo hivyo unaweza kupanga mambo utakayoyatekeleza ndani ya wiki moja na ndani ya mwezi mmoja.
Mwongozo wa namna ya kuweka malengo;
Malengo yaelezewe kwa njia chanya mfano tumia neno ninataka kuwa tajiri badala ya kuwa ninataka kupambana na umasikini. Unatakiwa kutaja ni kiasi gani cha pesa uunachokitaka na pamoja na muda gani/lini unataka upate pesa hizo. Unakiwa uweke vipaumbele kutokana na uzito wa malengo yako ili ujue unaanza na jambo lipi na kumalizia na jambo lipi. Malengo yako lazima yaandikwe na ili yasuisahaulike pia unapaswa kuyasoma mara kwa mara ili usiyasahau. Njia nyingine ya kukusaidia kukukumbusha kuhusu malengo yako ni kwa kutumia picha. Unaweza kukata picha ya kitu unachokitaka kwenye magazeti, kwa mfano kama unataka kununua gari ya aina fulani unaweza kukata picha hiyo na kuibandika sehemu ambayo unaiona kila mara kama vile kwenye kabati mlango wa chumbani au kwenye kabati. Unaweza kumweleza mtu unayemwamini kuhusu malengo yako mfano mkeo mwanao mkubwa au rafiki wa karibu ili aweze kukuhoji kama hutaweza kufikia malengo hayo. Malengo yako usimwambie kila mtu kwani watu wengine wanaweza kukufitini na kukukwamisha. Weka malengo ambayo yanawezekana au yanatekelezeka kufuatana na uwezo wako,kwa mfano usiweke malengo ambayo yako nje ya uwezo au mazingira yako kama vile katika biashara, kupanga mipango ambayo haiendani na sheria za nchi mfano kufanya biashara bila leseni.
Katika kufikia malengo yako furahia hali kama malengo uliyoyapanga yalikuwa magumu basi jipongeze. Kama yalikuwa mepesi basi jipangie magumu zaidi. Kama yalikuwa magumu sana yapunguzie makali. Kushindwa kufikia malengo si tatizo jizoeze kufanya utaratibu huu kwani unaweza kukusaidia kukufikisha mbali kimaisha. Ukishindwa kufikia malengo kipindi hiki jaribu kuyapeleka mbele mwaka ujao. Katika maisha usikate tamaa kwani ukikata tamaa ni sawa na kuwa mfu. Watu mashuhuri wamethibitisha kwamba unaposhindwa kufikia malengo hiyo ni kama shule ya maisha jaribu tena na tena mwisho utafanikiwa.
Jee umekwisha jiwekea malengo katika maisha yako? Kama hujafanya hivyo nakushauri uanze sasa hivi na utaona jinsi utakavyoanza kuyapata mafanikio kwa haraka.
CHARLES NAZI
Mwandishi wa makala hii ni Mshauri wa biashara na mtunzi wa kitabu cha Mbinu za biashara na maarifa ya kupata pesa na utajiri. Kwa Ushauri na mafunzo ya Ujasiriamali bila malipo kwa vikundi, piga simu namba 0755394701, barua pepe cnazi2002@yahoo.com

No comments: