Tuesday, December 28, 2010

Kakobe ambeba Lowassa

• Amshangaa Makamba kuendeleza siasa za kale, kupinga ukweli

na Mwandishi wetuASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) lililoko Mwenge, jijini Dar es Salaam, Zakaria Kakobe, ameshangazwa na kauli ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, kupinga kumpinga Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, aliyevitaka vyama vya CCM na CHADEMA kujadiliana kiungwana ili kuepusha uvunjifu wa amani katika mkoa wa Arusha.

Akizungumza katika ibada ya sikukuu ya Krismasi, Kakobe alisema Lowassa alikuwa sahihi kuona tatizo linaloweza kuifanya Arusha igeuke Ivory Coast, akasema mbunge huyo amefikia hatua ya kuhamasisha majadiliano ili kuepuka machafuko.

Kakobe alimbeza Makamba kwa kuamini katika matumizi ya mabavu bila kujali kuwa haki ndiyo huzaa amani.

Alibainisha kuwa Makamba anapaswa kufahamu kuwa kila jambo lina mwisho wake na kamwe matumizi ya nguvu hayawezi kuwa njia mwafaka ya kutatua matatizo ya watu wanaoamini kuwa haki yao imeminywa.

Askofu huyo aliongeza kuwa la msingi linalopaswa kufanywa ni kuzingatia ushauri wa Lowassa wa kuleta suluhu ya kudumu ili Arusha iendelee kuwa eneo la amani na Tanzania iendelee kupata sifa ya kuwa nchi ya amani, mshikamano na utulivu.

“Huyu ndugu yangu Makamba ananishangaza sana. Lowassa anatoa wito kwa kuwa ameona tatizo, lakini yeye anapinga, akijifanya hawezi kukaa meza moja ya majadiliano na CHADEMA akiamini kuwa matumizi ya magari ya maji ya kuwasha ndilo suluhisho…bado watu watapigwa na kuwa sugu wakitoka wanaendelea kutafakari unyanyasaji huo!” alisema.

Alibainisha kuwa matumizi ya nguvu na polisi yataleta usugu kwa wananchi kama ilivyo kwa Wapalestina na Waisraeli ambao mara kwa mara wamekuwa na mapigano yanayosababisha vifo, uharibifu wa mali na wengine kukimbia makazi yao.

Alisema kuwa iko siku wananchi watashambulia magari ya polisi na kuleta machafuko makubwa nchini ikiwa viongozi wataendelea kukubaliana au kusikiliza ushauri wa Makamba anayepinga mambo pasipo haki.

Hatua hiyo ya Kakobe kutoa kauli hiyo ambayo inaonekana kumkingia kifua Lowassa, inatokana na Makamba kutoa tamko la kupinga hatua ya mbunge huyo wa Monduli kutaka CCM na CHADEMA vikae meza moja kuzungumzia utata uliotokea kwenye uchaguzi wa meya wa Arusha Mjini.

CCM, ikishirikiana na mkurugenzi wa Arusha, ilifanya uchaguzi wa meya peke yake bila kuwashirikisha wabunge na madiwani wa CHADEMA, jambo lililopingwa na wana CHADEMA; nao polisi wakaingilia kati wakiisaidia CCM na kumpiga Mbunge wa Arusha, Godbless Lema.

Hali hiyo ilisababisha mvutano mkubwa wa kisiasa miongoni mwa wakazi wa Arusha, kiasi cha kuwafanya wananchi na viongozi wengine wa umma, wakiwamo Lowassa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kukemea ‘uhuni’ huo wa CCM, na kuvitaka vyama vikae meza moja kupata mwafaka.

Hata hivyo Makamba alikerwa na kauli ya Lowassa, akasema CCM haina cha kujadiliana na CHADEMA kwa sababu kilishinda kihalali kwenye uchaguzi huo ambao ulifanyika hivi karibuni, licha ya ukweli kwamba uchaguzi huo ulifanyika kinyume cha sheria.

Bila kujali kwamba Lowassa ni Mbunge wa Monduli mkoani humo, mwenye kuguswa moja kwa moja na shari inayotokea Arusha, na bila kujali kwamba ana haki ya kujadili suala lolote la kitaifa kwa kutumia haki na kinga aliyonayo kama mbunge, Makamba alimtaka Lowassa kutoa ushauri wake kwenye vikao vya juu vya chama kwa kuwa yeye ni mjumbe wa vikao hivyo badala ya kuzungumzia majukwaani.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamemuunga mkono Lowassa na kusema Makamba anaendekeza siasa za kale zilizoifikisha CCM mahali pa kuchukiwa na umma kwa sababu ya ubabe uliokithiri.

Akirejea mtafaruku huo, Askofu Kakobe alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuachana na siasa za udini na kwamba badala yake afanye tathmini ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu ambao kwa kiasi kikubwa ulitawaliwa na mazingira ya kuminywa kwa haki.

“Wakati na baada ya uchaguzi haki ilitoweka, jamii haikutendewa haki na hata wagombea mbalimbali nao walishuhudia jambo hilo, serikali ina jukumu ya kuhakikisha inarudisha haki hiyo.

“Hatupaswi kung’ang’ania masuala ya udini ambayo hayapo. Kinachotakiwa hivi sasa ni kupiga hatua kwenye maendeleo sambamba na kuzingatia zaidi haki za kila mtu,” alisema.

Alisema inashangaza kuona viongozi kila kukicha wakizungumzia udini na kudai nchi inanyemelewa na udini wakati wanafahamu fika kuna ushirikiano miongoni mwa jamii yote bila kuangalia ni wa dini au kabila gani.

“Watawala wenye akili wangekaa na kufanya tathmini ya uchaguzi na si kukaa na kuangalia nani alikuwa kinyume na chama tawala ili wamfukuze, maana hatua hiyo inadhihirisha kuwa kuna mahali wamepotoka na wanahitaji kurekebisha kabla ya huo mwamba haujatoboka ili kuinusuru nchi,” alisema.

Alisema kiongozi yeyote anayewanyima haki wananchi hatokani na Mungu maana yake anatokana na ibilisi ambaye huanzisha na kufurahia migogoro, machafuko na vita.

Akinukuu kifungu cha Biblia Waraka wa Yoh 5:17, “Kila tendo lisilotokana na haki ni dhambi.”

Alisema iwapo taifa linakosa amani ni lazima kuna jamii ambayo haitendewi haki akitolea mfano hata mfululizo wa migomo ya vyuo vikuu inayotokea imesababishwa na watawala kuwanyima haki wanafunzi ikiwemo kupata mikopo, chakula na malazi.

Alinukuu kifungu cha Biblia katika Isaya 32:17, “Haki na amani ni mapacha na pasipo haki hapana amani…Yesu ni Mfalme wa amani amesema mazao ya haki ni amani na utulivu hivyo lazima serikali ihakikishe haki inakuwepo miongoni mwa jamii.”

Alisema migogoro mingi inasababishwa na baadhi ya watawala kujipa haki huku wengine wakinyimwa na kujikuta wanaambulia kunyanyaswa na kukosa mahitaji muhimu.

Alisema kuwa kutokana na mfumo wa vyama vya siasa uliopo ili amani na utulivu vizidi kudumu kuna haja ya vyama vyote vya siasa kupata haki sawa.

“Mfumo wa vyama vya siasa unahitaji kila chama kupata haki sawa na kingine; lakini kwa kuwa wapo baadhi ya watu wanadhani bado tuko katika ule mfumo wa chama kimoja wanataka kuendeleza mfumo wa ‘Zidumu Fikra za Mwenyekiti’ hiyo ni kutaka kusababisha uvunjifu wa amani,” alisisitiza.

No comments: