Tuesday, December 28, 2010

Maandamano ya CUF yazimwa

• Polisi yasema yatahatarisha amani

na Waandishi wetu



JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limezuia maandamano ya Chama cha Wananchi (CUF), yaliyokuwa yafanyike leo kwa lengo la kuwakilisha pendekezo la Katiba mpya kwa Waziri wa Sheria na Katiba.

Uamuzi huo ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Kamishna wa Polisi Kanda Maalum, Suleiman Kova, ambapo alisema yanaweza kuleta uvunjifu wa amani.

Aliongeza kuwa viongozi wa CUF walimpelekea barua iliyokuwa ikionyesha nia yao hiyo lakini ile waliyoipeleka Wizara ya Sheria na Katiba haikueleza jambo hilo.

“Viongozi wa CUF, waliniletea barua yao yenye lengo la kuandamana, lakini wakati huo huo walipeleka barua tofauti kwa Wizara ya Sheria ambayo haikueleza juu ya maandamano yao,” alisema Kova.

Alisema wamesitisha maandamano hayo kwa mujibu wa sheria ya jeshi hilo, kifungu cha (43) sheria ya kwanza hadi ya 6, vifungu vinavyowapa mamlaka ya kufanya hivyo mara wanapohisi uvunjifu wa amani.

“Tumepata wasiwasi na maandamano ya CUF, kwa sababu ya utata wa barua zao, tunahisi hayatakuwa ya amani, tumeyafuta.

“Tunaomba wananchi na wafuasi wao wasishiriki kwa sababu ni batili, watakaokaidi tutapambana nao,” alisema Kova.

Kamanda Kova alionyesha barua iliyopelekwa kwake na ile ya Wizara ya Sheria na Katiba yenye kumbukumbu namba AK/DSM/NKM/B/001/AZ/2010/105, ya Desemba 21.

Aliongeza kuwa iliyopelekwa kwao na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatilo, yenye kumbukumbu AK/DSM/NKM/B/001/AZ/2010/104/, ilielezea juu ya lengo la kuandamana tofauti na ile iliyopelekwa wizarani.

Alisema kuwa ile iliyopelekwa kwao ilielezea kuwa chama hicho kitafanya maandamano kuanzia Buguruni kupitia barabara ya Kawawa, Morogoro na makutano ya barabara ya Bibi Titi kuelekea barabara ya Ohio na hatimaye Wizara ya Sheria na Katiba.

Aliongeza kuwa maandamano hayo baada ya kutoka wizarani hapo yangemalizia katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

“Kwa kuwa hawakutoa taarifa zao kwa waziri kama watawasilisha kwa maandamano, ni dhahiri asingekuwa huru na kungekuwa na uvunjaji wa amani, tumekaaa nao zaidi ya saa moja na kufikia muafaka na wametuelewa,” alisema Kova.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF bara, Julius Mtatiro, alisema leo watafanya maandamano yao ya amani kwa ajili ya kuwasilisha rasimu ya Katiba mpya kwa Waziri wa Sheria na Katiba.

Mtatiro, aliliambia Tanzania Daima, kuwa maandamano hayo yatafanyika leo hii licha ya Jeshi la Polisi nchini kuyazuia.

Alisema CUF, iliandika barua kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, ambayo iliweka wazi maandamano hayo lakini wanashangazwa na Jeshi la Polisi kuyazuia maandamano yao.

Aliongeza kuwa kamanda Kova, alimuita ofisini kwake na kumtaarifu zuio la kufanya maandamano hayo ambayo wao hawaoni kama yanaweza kuleta uvunjifu wa amani.

Alisema licha ya zuio hilo kwa CUF, wanachama wake na wapenzi wa mabadiliko wameshajiandaa kushiriki maandamano hayo.

“Maandamano yako palepale kuanzia saa mbili asubuhi; hilo ndilo tamko letu kwa sasa. Ni lazima Katiba mpya ipatikane na tunachopeleka kwa waziri ni draft ya Katiba hiyo,” alisema Mtatiro.

Wakati huohuo, Mwanasheraia Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, amesema hakuna haja ya kuwapo kwa Katiba mpya bali iliyopo ifanyiwe marekebisho.

Akizungumza na waandishi wa habari jana muda mfupi baada ya kuapishwa Jaji Mkuu, Mohamed Othman, kwenye viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam, Werema alisema marekebisho ya Katiba ni ruksa kwa kuondoa baadhi ya mambo ya zamani na kuweka mambo mapya.

Alisema mwaka 1994 yalifanyika marekebisho ya Katiba kwa kuingiza vipengele vinavyohusu haki za binadamu na kueleza kuwa mabadiliko hayo yalifanyika kutokana na matakwa ya wananchi.

“Marekani yamefanyika marekebisho Katiba yao mara ngapi? India nayo inafanyika marekebisho ya Katiba yao mara ngapi? Nadhani zaidi ya mara 50 na Marekani wanafanya mabadiliko yao kutokana na masuala ya maana yanayojitokeza,” alisema Jaji Werema.

Aliwataka wananchi kupeleka maoni yao na si kila mmoja kuzungumza kama bata.

“Kwa nini tulumbane? Tufanye marekebisho kwa kuwekwa mapya na kuondolewa ya zamani...kiraka sawa hata nguo si unaweka kiraka?” alihoji Jaji Werema.

Hata hivyo, alihoji upya wa Katiba ni nini na kutoa msemo kuwa ‘ukuukuu wa kamba si upya ya ukambaa’.

“Upya wa Katiba ni nini, unaweka kipya nini? Ukuukuu wa kamba si upya wa ukambaa. Nadhani hapa mmenielewa!” alisema.

Aidha, alisema hakuna haja ya kulumbana kama itafanyiwa marekebisho au mpya na kubainisha kuwa hali hiyo itategemea na matakwa ya Watanzania.

“Watu wana mawazo mazuri kuhusu suala hili na hata kijijini kwangu, tunaweza kutofautiana lakini si katika suala la Katiba. Suala hili tutalijadili,” alisema.

Alisema ajenda hiyo ni lazima iwe na mbebaji na kwamba anaweza kuwa mtu yeyote na chama chochote cha siasa.

“Sisi Wakurya tunasema vita ni vita, huwezi kumlaumu aliyebeba ajenda hii, kwani mtu yeyote angeweza kuibeba hata ikiwa ni vyama vyama vya siasa, kwani Katiba ni siasa.

No comments: